Na Karama Kenyunko Michuzi Tv

Wafanyakazi 10 wa zamani wa kampuni ya Security Group of Africa (SGA) wamehukumiwa kutumikia kifungo cha miaka miwili gerezani baada ya kukiri kutenda kosa la wizi wa sh. milioni 780 mali ya benki ya NMB.

Mahakama pia  imetaifisha mali na fedha ambazo washitakiwa hao walikamatwa nazo  ama walizipata kutokana na wizi huo.

Washitakiwa wamesomewa adhabu hiyo leo Februari 26, 2024  na Hakimu Mkazi Rahim Mushi wa mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu baada ya washitakiwa hao kuingia makubaliano ya kukiri kosa na Mkurugenzi wa Mashitaka Nchini (DPP)

Washitakiwa hao ni Menjestu Mselema, Tulipo Mwankiusye, Bernard Macheba, Joseph Mwatonoka, Juma Mbulinda, Joseph Mpondo, Englibert Masane,  Beda Mmali, Kaisi Nasibu  na Oswald Mselema.

Akisoma hukumu hiyo, hakimu Mushi amesema, amezingatia maombi ya washtakiwa kupitia wakili wao Albert Kikuli kwamba washtakiwa ni wakosaji wa mara ya kwanza na pia wapo mahabusu miaka minne sasa.

"Pia nimezingatia hoja kwamba washitakiwa hawajaisumbua mahakama na pia waliingia makubaliano hayo na DPP kwa hiyari yao wenyewe" amesema Hakimu Mushi.

Hakimu amesema kutokana na hali hiyo, washtakiwa hao wanahukumiwa kulingana na mkataba wa maridhiano waliyoingia ikiwemo kifungo cha miaka miwili gerezani na kurejesha fedha na mali zote walizokamatwa nazo ambazo zilitokana na wizi huo.

Katika kesi hiyo, washitakiwa hao walikuwa wakikabiliwa na mashtaka matatu ambayo ni kula njama ya kutenda kosa la wizi, wizi na utakatishaji fedha.

Ilidaiwa kwamba kati ya Juni mosi  hadi 8 mwaka 2020 jijini Dar es Salaam, washitakiwa hao walikula njama ya kutenda kosa la wizi.

Ikadaiwa, Juni 8 mwaka 2020 eneo la NMB tawi la Mbezi Beach washtakiwa waliiba Sh. milioni 780 mali ya NMB.

Katika shitaka la tatu, washitakiwa hao wanadaiwa kwamba , katika tarehe tofauti kati ya Juni mosi hadi 30 mwaka huo huo, washtakiwa walitakatisha fedha hizo kwa kununua vitu mbalimbali wakati wakijua fedha hizo zilitokana na kosa la wizi.



 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...