NA MWANDISHI WETU,PEMBA.

Chama Cha Mapinduzi(CCM) Zanzibar,kimewasihi wananchi visiwani humo kufuata maelekezo na wito unaotolewa na Serikali juu ya kuacha kula nyama ya kasa wanaodhaniwa kuwa na sumu.

Nasaha hizo zimetolewa na Katibu wa Kamati Maalum ya NEC,Idara ya Itikadi,Uenezi na Mafunzo Khamis Mbeto Khamis alipokwenda kutoa pole na kuzifariji familia za watu tisa waliofariki dunia hivi karibuni kwa ulaji wa kasa Kisiwa Panza Mkoa wa Kusini Pemba.

Alisema Chama Cha Mapinduzi Zanzibar kimepokea kwa huzuni na masikitiko makubwa taarifa za misiba hiyo ya wananchi na kwamba Chama na Serikali zitakuwa karibu na familia za marehemu hao kwa kuhakikisha wanapata huduma muhimu za kijamii kama zilivyo familia zingine nchini.

Alisema Serikali haipendi kuona wananchi wake wanapoteza maisha kwani kila mtu ana mchango wake katika ustawi wa maendeleo ya familia yake na Taifa kwa ujumla.

Katika maelezo yake Mbeto,amesema wananchi hasa wavuvi wanatakiwa kuacha kuvua kasa kwani tayari ameonekana sio samaki salama kwa matumizi ya binadamu.

Alieleza kuwa Zanzibar imebarikiwa kuwa na bahari yenye samaki wa aina mbali mbali wanaofaa kuliwa na binadamu hivyo ni muhimu wananchi kujali afya zao kwa kuacha kula kasa wenye sumu.

“Nimekuja kutoa pole kwa niaba ya Makamu Mwenyekiti ambaye pia ni Rais wa Zanzibar Dk.Hussein Mwinyi anawapa pole na kuwasihi muendelee kuwa wavumilivu kwa kipindi hiki kizito cha misiba hii.”,alisema Mbeto.

Amefafanua kuwa miaka ya hivi karibu Serikali ilipiga marufuku na kuwataka wavuvi kuacha kuvua kasa kwa kile kilichoelezwa kuwa viumbe hao kutokuwa salama kutokana na mabadiliko ya vyakula wanavyokula na kusababisha sumu ya mwili na kuhatarisha uhai kwa binadamu anayekula nyama husika.

Alisema utafiti mdogo uliofanywa umebaini kwamba kasa wamekuwa wakila chakula aina ya majani yenye mchanganyiko wa sumu ambayo binadamu akila nyama yake husababisha kifo.

Pamoja na hayo pia Katibu huyo wa NEC Mbeto,aliwatembelea wananchi walionusurika vifo kutokana na ulaji wa kasa huko Hospitali ya Abdallah Mzee Pemba na kuutaka Uongozi wa Hospitali hiyo kuendelea kuwapatia matibabu ili wapone na kuendea na majukumu yao.

Inadaiwa watu hao waliokula kasa walianza kupata matokeo ya kuumwa na tumbo kwanzia siku chache ,walioathirika na ulaaji huo na kupelekea kupata dalili za Kulegea mwili ,kutapika, kuharisha na tumbo kuuma hadi kupelekea vifo 9 kwa watoto chini ya miaka 10 na wengine 34 wanaendelea kupatiwa matibabu.

KATIBU wa Kamati Maalum ya NEC,Idara ya Itikadi,Uenezi na Mafunzo Khamis Mbeto Khamis,akizungumza na Wananchi wa Kisiwa Panza mara baada ya kuzifariji familia zilizopata misiba ya kufariki watu tisa waliokula nyama ya kasa Mkoa wa Kusini Pemba.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...