KATIBU Tawala wilaya ya Kibaha , mkoa wa Pwani, Moses Magogwa amewaasa wananchi kujiepusha na ukataji miti kiholela na badala yake wajenge tabia ya kupanda miti na kuitunza kwani ndio jawabu la kupambana na uharibifu wa mazingira.
Ameeleza hayo wakati Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kibaha kwa kushirikiana na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) ilipofanya maadhimisho ya siku ya upandaji miti kata ya Kikongo, wilayani humo.
Magogwa akimuwakilisha Mkuu wa wilaya hiyo, Nickson Simon John alieleza, kampeni ya kupanda miti Tanzania zilianza tangu mwaka 1999 , ambapo ilionekana hali na kasi ya ukataji miti inaongezeka.
"Maana yake nini, kama jitihada hizi zisingewekwa mapema hali ingekua mbaya sana leo hii, na ndio maana leo tupo hapa kuendelea kuwa sehemu ya upandaji miti ili dunia yetu ibaki salama ," alisisitiza Magogwa.
Magogwa anaeleza, misitu ni ubunifu inabidi tutumie nishati mbadala ili kuachana na kuharibu mazingira.
"Mfano nikitazama mkoa wa Dar es salaam ndio Jiji linaloongoza kwa utumiaji wa mkaa huku bidhaa hizo zikitokea mkoa wa Pwani, tutaanda utaratibu maalum ikiwezekana Serikali ione haja ya kuongeza kasi kupeleka njia za mbadala mbalimbali ili maeneo mengine yasalimike katika kutunza misitu" alieleza Magogwa.
"Tunawajibu wa kupanda miti na kuifuatilia, hivyo ubunifu wetu ni kutafuta energy mbadala ili misitu yetu isiharibike, wenyeviti wote wa vijiji msiuze maeneo bila kufuata utaratibu, endeleeni kupokea maombi ila taarifa zifike ofisi ya Mkurugenzi, atume wataalamu ili kujiridhisha"
Alieleza kwa utaratibu huo utasaidia kupunguza pia matatizo ya migogoro ya ardhi na ufyekaji wa maeneo ya misitu ambayo bado haipo kwa uangalizi wa TFS.
Hata hivyo, Magogwa aliipongeza TFS kwa kazi nzuri wanayofanya na wilaya itaendelea kuwapa ushirikiano ili kuhakikisha misitu inabaki salama kwa manufaa ya nchi.
Kwa Upande wake Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Kibaha Vijijini, Mkali Saidi Kanusu aliwataka wanaccm na wananchi kuiga mfano huo bora ambao umeonyeshwa kwa vitendo na Ofisi ya mkuu wa Wilaya pamoja na TFS.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...