Na Mwandishi wetu, Simanjiro

DIWANI wa Kata ya Loiborsoit, Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, Siria Baraka Kiduya, amesoma taarifa ya utekelezaji wa ilani ya uchaguzi wa CCM kwa kipindi cha Novemba mwaka 2020 hadi Novemba mwaka 2023.

Diwani Siria akisoma taarifa hiyo kwa wajumbe wa Halmashauri kuu ya CCM kata ya Loiborsoit, amewashukuru wana CCM na wataalam na wananchi wote ndani ya kata kwa namna wanavyompa ushirikiano katika kutatua kero na changamoto mbalimbali.

“Ndugu Mwenyekiti wa CCM, naomba nichukue fursa hii kukishukuru chama changu (CCM) kwa kuniamini kupitia vikao mbalimbali na kupitisha jina langu kugombea nafasi ya udiwani wa kata ya Loiborsoit,” amesema Siria.

“Pia ndugu Mwenyekiti wa CCM wa Kata ya Loiborsoit na wajumbe kwa ujumla naomba niwashukuru ninyi kwa moyo wa unyenyekevu mkubwa kwa namna mlivyojitoa kwa namna moja au nyingine ili kupambana na kuhakikisha CCM inaendelea kushika dola na kuongoza Taifa hili kwa kipindi cha miaka mitano hadi 2025,” amesema.  

Amewashukuru wataalam wote ndani ya Kata kwa namna wanavyopambania kutatua kero na changamoto mbalimbali ambazo zipo ndani ya kata hivyo itoshe kusema anawashukuru mno na kazi iendelee.

“Ndugu Mwenyekiti wa CCM Kata ya Loiborsoit, naomba nichukue fursa hii kumpongeza Mama yetu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dokta Samia Suluhu Hassan kwa kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa CCM kwa kura zote asilimia 100 na kwa namna anavyolipambania Taifa, tunamuombea Mungu ili aweze kutimiza majukumu yake vizuri na salama,” amesema.

Amesema Kata ya Loiborsoit ni miongoni mwa kata 18 zinazounda Wilaya ya Simanjiro ina wakazi wapatao 11,204 yenye vijiji viwili vya Loiborsoit B chenye vitongoji vitatu vya Engurash, Mazinde na Oltibu na kijiji cha Ngage, ambacho kina vitongoji vitatu vya Ngage A, Ngage B na Ndepesi.    

Ametaja utekelezaji uliofanyika kwa  kipindi cha Novemba 2020 hadi Novemba 2023 ni kumalizia chumba kimoja cha maabara cha shule ya sekondari Loiborsoit kilichogharimu shilingi milioni 30.

“Tumefanikiwa kujenga chumba kimoja cha darasa na ofisi moja ya walimu, iliyogharimu shilingi milioni 29 ambapo shilingi milioni 20 ilitoka kwenye pochi ya mama na shilingi milioni 9 ni michango ya wananchi wa vijiji vyote viwili vya Loiborsoit B na Ngage,” amesema Diwani Siria.

Amesema wamefanikiwa kujenga chumba kimoja cha darasa kwenye shule hiyo ya sekondari lililogharimu shilingi 27 ambapo UVIKO 19 ilitoa shilingi milioni 20 na michango ya wananchi wa vijiji vyote viwili ni shilingi milioni 7.

Amesema kwenye shule ya msingi Mazinde walipata madarasa nane ya wavulana na matundu nane ya vyoo ya wasichana, yaliyofadhiliwa na shirika la ECLAT FOUNDATION na nguvu ya wananchi.

“Kwenye shule ya msingi Ndepesi tumefanikiwa kujenga ofisi ya walimu iliyogharimu shilingi milioni 9 fedha ambazo zilitolewa na halmashauri ya wilaya ya Simanjiro,” amesema Diwani Siria.

Amesema pia wamefanikiwa kujenga nyumba ya walimu iliyogharimu kiasi cha shilingi milioni 10 fedha zilizotolewa na Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro.

Amesema walipokea madawati 75 kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro, ambayo yapo kwenye shule hiyo ya msingi Ndepesi, yanayotumiwa na wanafunzi.

Amesema kwenye shule ya msingi Loiborsoit B wamefanikiwa kujenga choo chenye matundu saba ya wasichana kilichogharimu shilingi milioni 3.4 ambapo TAWA walichangia shilingi milioni 2.850 na wananchi walichangia shilingi 600,000.

“Kwenye shule ya msingi Ngage tumefanikiwa kujenga choo cha matundu saba ya wasichana iliyogharimu shilingi milioni 15 zilizotolewa na Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro,” amesema Diwani Kiduya.

Amesema kwenye shule hiyo ya Ngage, wamefanikiwa kujenga vyoo viwili vya walimu, ambapo walimu wa kiume choo kimoja na walimu wa kike choo kimoja vilivyogharimu shilingi milioni 5 zilizotolewa na Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro.

Diwani huyo amesema pia wamefanikiwa kumalizia chumba cha kompyuta kwenye shule ya msinig Ngage, chenye thamani ya shilingi milioni 5.

Amesema matarajio ya mwaka 2024/2025 kwenye suala la elimu ni umaliziaji wa shule shikizi zote mbili za Songoyo na Ngage B.

“Ndugu Mwenyekiti wa CCM kata ya Loiborsoit, kwenye suala la afya, kata yetu ina zahanati mbili zilizopo kila kijiji ambapo kijiji cha Ngage kina zahanati yake na kijiji cha Loiborsoit B, pia kina zahanati yake,” amesema Diwani Siria.

Amesema kwenye zahanati ya Ngage wamefanikiwa kufanya ukarabati kwenye chumba cha kujifungua wakiwa mama na kujenga choo chenye matundu manne na mabafu mawili, kujenga choo cha watumishi na hivyo vyote vimejengwa kupitia mradi wa WARSH kwa gharama za shilingi milioni 34.

Amesema kwenye zahanati ya Loiborsoit wamefanikiwa kufanya ukarabati wa chumba cha kujifungulia wakina mama na kujenga choo chenye matundu manne na mabafu mawili na vyoo vya watumishi vilivyogharimu shilingi milioni 35 kupitia mradi wa WARSH.

“Hata hivyo, tupo kwenye mchakato wa uanzishwaji wa kituo cha afya Loiborsoit kwani kwenye kata yetu hatuna kituo cha afya zaidi ya zahanati hizo,” amesema Diwani Siria.

Amesema kuhusu usalama wana mpango wa ujenzi wa kituo cha polisi Loiborsoit na miundombinu ya barabara kuna mpango wa upatikanaji wa daraja la kuunganisha wilaya za Simanjiro na Same mkoani Kilimanjaro kupitia kijiji cha Ngage.

“Katika miundombinu ya nishati ya umeme usambazaji unatarajiwa kufanyika katika vitongoji vyote vilivyobaki vya Mazinde, Ngage A,Ndepesi na Endurashi,” amesema Diwani Siria.

Amesema usambazaji wa maji katika vitongoji vyote vilivyobaki vya kijiji cha Loiborsoit B vya Mazinde na kijiji cha Ngage vitongoji vya Ngage A na Ndepesi na usambazaji wa majumbani na maeneo yote yaliyobakia.   

Amesema katika kilimo kuna uendelezaji wa uchimbaji wa mfereji wa Songoyo hadi mashamba mapya ya Ngage B Lesurenge mpaka nguzo za umeme.
 
Amesema kwenye sekta ya mifugo kuna uanzishwaji wa majosho mawili ya Mazinde na Songoyo.

“Kwenye hitimisho namshukuru Mwenyekiti wa CCM Kata ya Loiborsoit, Katibu Kata, wajumbe wote, wanachama na wataalam wote pamoja na viongozi kidini, kimila (malaigwanani) na wananchi wote,” amesema Diwani Siria.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...