Mtandao wa Polisi wanawake (TPF-Net) Mkoa wa Songwe umeikumbusha jamii na taasisi za kiserikali na zisizo za kiserikali kuwa na utamaduni wa kuwasaidia watoto na wanafunzi wenye mahitaji maalum pindi wanapotembelea shuleni kwa ajili ya kutoa elimu ya masuala mbalimbali.

Kauli hiyo imetolewa Machi 06, 2024 na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Theopista Mallya ambaye ni Mwenyekiti wa mtandao huo Mkoani Songwe alipotembelea Shule ya Msingi Nyerere iliyopo Wilaya ya Ileje akiwa ameambatana na Maafisa, Wakaguzi na Askari wa vyeo mbalimbali kutoka Idara mbalimbali zilizo chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa ajili ya kutoa msaada wa vitu mbalimbali kwa wanafunzi wa Shule.

“Dhumuni la msaada huu ni kuwaweka watoto wenye mahitaji maalum wawe sawa na wenzao kimuonekano wawapo shuleni hapa, pia kuwajengea upendo ambao utapelekea wasome kwa bidii na kufanikiwa kwenye masomo na maisha yao ya baadae” alisema Kamanda Mallya.

Aidha, Kamanda Mallya alisisitiza na kuikumbusha jamii na makundi ya watu mbalimbali kuona umuhimu wa kusaidia wanafunzi na watoto wenye mahitaji maalum na wanaoishi kwenye mazingira magumu ili kuwaepusha kufanyiwa vitendo vya kikatili na kutojiingiza kwenye makundi ya kihalifu.

Naye, Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo Jonas Kajiba akiongea kwa niaba ya wanafunzi hao amemshukuru Kamanda Mallya na askari wote walioitembelea Shule hiyo na amesema tukio hilo litabaki kuwa kumbukumbu kubwa maisha mwao ambalo halitaweza kusahaulika.

Aliongeza kuwa, tukio hilo litaleta chachu kwa wanafunzi wa Shule yao kusoma kwa bidii na kufanya vizuri katika mitihani yao na masomo kwa ujumla wake.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...