MAENDELEO Ya Uchumi wa Tanzania umeendelea kukua licha ya athari kubwa za mlipuko wa UVIKO-19 duniani pamoja na vita za Urusi na Ukraine pia Mashariki ya Kati. Matatizo haya yaliutikisa uchumi wa Tanzania uliokuwa umefikia wastani wa ukuaji wa zaidi ya 7% na kuushusha hadi 4.2% mwaka 2020. Hata hivyo, hivi sasa ukuaji umefikia 5.2% kutokana na
uongozi thabiti wa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan.

Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo) na Msemaji Mkuu wa Serikali Mobhare Matinyi amevieleza vyombo vya habari na kusema kuwa Tanzania imeendelea kuwa katika kundi la nchi zenye uchumi wa pato la kati, ikimaanisha pato la wastani la kila mwananchi kwa mwaka (GNI per capita) ambapo ingawa mwaka 2019 ilikuwa kiasi cha dola 1,080, lakini mwaka 2022 ni dola 1,200.

“Serikali pia imeendelea kudhibiti mfumuko wa bei ambapo kwa sasa ni chini ya 4% - kiwango ambacho ni miongoni mwa viwango bora katika nchi za jumuiya za kikanda ambazo Tanzania ni mwanachama, kama Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC). Vile vile, akiba ya fedha za kigeni imeendelea kuwa toshelezi ambapo katika kipindi chote cha miaka mitatu hadi Desemba 2023, nchi ilikuwa na akiba inayotosha kuagiza bidhaa kutoka nje ya nchi kwa miezi 4.5, ikiwa ni kiwango cha juu ya lengo la miezi 4. Akiba hiyo ni sawa na dola za Marekani bilioni 5.4.” Amesema.

Kuhusu ukusanyaji wa mapato Matinyi amesema, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imeendelea kufanya vizuri katika kipindi cha miaka mitatu kwa kufuata mwongozo wa Rais wa kujenga uhusianomzuri na wafanyabiashara na
kujali changamoto wakati wa kukusanya kodi.

“Makusanyo yamefikia shilingi trilioni 24.14 kwa mwaka 2022/23 kutoka shilingi trilioni 18.15 mwaka 2020/21. Hili ni ongezeko la shilingi trilioni 5.99. Aidha, kwa mwezi Desemba 2023, TRA ilivunja rekodi ya ukusanyaji ya kila mwezi baada ya kufanikiwa kukusanya shilingi trilioni 3.05 licha ya kuwa wastani kwa mwaka huu hadi sasa ni shilingi trilioni 2.13. Ni vema kufahamu kwamba hadi kufikia tarehe 20 Machi, 2024, TRA
ilikuwa imeshakusanya kiasi cha shilingi trilioni 19.21, ikiwa ni dalili mkwamba itavuka kiasi
cha mwaka uliopita.” Ameeleza.

Katika sekta ya uwekezaji kwa kipindi cha mwezi Machi 2021 hadi Machi 2024 Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kimefanikiwa kusajili jumla ya miradi 1,188 ambayo ilikadiriwa kuwekeza kiasi cha mtaji wa dola za Marekani milioni 15,041 na kutoa jumla ya ajira 345,464. Kati ya miradi hiyo asilimia
35 inamilikiwa na Watanzania, asilimia 41 ni ya Wageni na asilimia 24 ni ya ubia kati ya Watanzania na Wageni.

Aidha amesema Kamati ya Kitaifa ya Kusimamia Uwekezaji (National Investment Steering Committee - NISC) ilitoa idhini ya kusainiwa mikataba ya utekelezaji kwa miradi 16. Miradi hiyo yenye hadhi ya mirahi mahiri ni pamoja na Mradi wa Bagamoyo Sugar Limited; Mradi wa Kagera Sugar Limited; na Mradi wa Mtibwa Sugar Estate Limited;. Vile vile, NISC iliridhia miradi mingine nane ambayo ilisaini mikataba ya utekelezaji na TIC.

Pia amesema thamani ya uwekezaji katika taasisi zinazosimamiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina imeongezeka kutoka shilingi trilioni 70 mwaka 2021 hadi kufikia shilingi trilioni 76 mwaka 2023 - sawa na ongezeko la 8.6%. Sababu ya ongezeko hili ni Serikali ya Awamu ya Sita kuongeza mitaji kwa kiasi cha shilingi trilioni 5.5 katika mashirika ya kimkakati kwa maslahi ya Taifa.

Mathalani katika sekta ya Kilimo Bajeti imeongezeka kutoka shilingi bilioni 294.16 mwaka 2021/2022 hadi kufikia shilingi bilioni shilingi bilioni 970.78 mwaka wa fedha 2023/2024. Matumizi ya mbolea yameongezeka kutoka tani 320,233 kwa mwaka wa fedha 2020/21 hadi kufikia tani 580,628 kwa mwaka wa fedha 2022/23.

Amesema bajeti ya maendeleo ya umwagiliaji imeongezeka kutoka shilingi bilioni 46.5 mwaka 2021/22 hadi shilingi bilioni 361.5 mwaka 2023/24 ambapo wataalam wa kilimo 320 wameajiriwa na kusambazwa katika ofisi za umwagiliaji zilizopo katika wilaya 139. Mitambo 15 na magari 53 vimenunuliwa kwa ajili ya shughuli za umwagiliaji. Eneo la umwagiliaji limeongezeka kutoka hekta 694,715 mwaka 2020/2021 hadi hekta 727,280.6 mwaka 2022/2023.

“Serikali inaendelea kukamilisha ujenzi wa skimu za umwagiliaji zenye hekta 95,000 zilizoanza mwaka 2022/2023 pamoja na kuanza skimu mpya zenye ukubwa hekta 95,000 kwa mwaka 2023/2024, ambapo kukamilika kwake kutaongeza eneo la umwagiliaji kufikia hekta 917,280. Programu ya Vijana ya Jenga Kesho Iliyo Bora (Build Better Tomorrow-BBT). Mradi
unashirikisha vijana 688, ambao wameanza kilimo biashara katika shamba la Chinangali II.” Amefafanua.

Akieleza kuhusu na sekta ya Utalii Matinyi amesema kuwa sekta hiyo kwa sasa inaongoza kuiletea nchi fedha za kigeni ambapo sasa zimefikia dola za Marekani bilioni 3.37 (zaidi ya shilingi trilioni 8).

“Kimsingi sekta hii imemrejeshea shukurani Mhe. Rais kwa juhudi zake binafsi za kutoka ofisini na kwenda kushiriki katika utengenezaji wa filamu ya "Tanzania: The Royal Tour" Katika kipindi cha miaka mitatu idadi ya watalii nchini imeongezeka kutoka 922,692 mwaka 2021 walioipatia nchi mapato dola za Marekani bilioni 1.31hadi watalii 1,808,205 mwaka 2023 walioingiza dola bilioni 3.37. Kwa kuongeza idadi ya watalii wengi baada ya mlipuko wa UVIKO-19 Tanzania sasa inashika nafasi ya pili barani Afrika baada ya Etiopia; na kwa kuongeza mapato makubwa inashika nafasi ya tatu baada ya Moroko na Mauritius.” Amesema.

Kuhusiana na usafiri wa anga, Matinyi amesema, Serikali iliendela kuliimarisha Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) kwa kuwekeza zaidi ikiwemo kununua dege ili kulifanya limudu kutoa huduma na kuchochea ukuaji wa sekta
zingine za kiuchumi na kwa miaka mitatu Serikali imenunua ndege tano zikiwemo tatu za masafa ya kati ambazo ni Airbus A220 mbili; Boeing 737 Max9; Boeing 767-300F ya mizigo na Dash 8 Q-400 na zote zinaendelea kutoa huduma. Ndege mbili zaidi, Boeing 737 Max9 (iko katika hatua ya makabidhiano) na moja ya masafa marefu aina ya Boeing 787-8 (katika hatua ya uundwaji) tayari zimeshanunuliwa na zinatarajiwa kuwasili chini mwezi Machi na Aprili mwaka huu.

Pia kuhusiana na usalama wa raia amesema;  Jeshi la Polisi linafanya kazi kwa weledi likiwa na vitendea kazi.

“Mhe. Rais aliongeza bajeti yake kutoka shilingi bilioni 565 mwaka 2020/21 hadi shilingi bilioni 798 kwa mwaka 2023/24. Hivyo basi, magari 290 na pikipiki 105 zilinunuliwa na sasa zinatumika. Aidha, jumla ya vituo 18 vya polisi na ofisi kumi za makamanda wa polisi wa mikoa nazo zimejengwa na majengo 20 ya madawati ya jinsia na watoto. Katika kupambana na tatizo la ukatili wa kijinsia na unyanyasaji dhidi ya watoto, jeshi la polisi limeanzisha madawati 420 nchini kote.

Aidha tatizo la uzagaaji wa silaha ndogondogo na nyepesi Jeshi la Polisi limefanikiwa kupokea silaha 1,785 na risasi 262 zilizosalimishwa na pia silaha 11,438 zimeteketezwa.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...