Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa kushirikiana na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Tarehe 21 Machi, 2024 wameingia kwenye ubia ili kuanza utekelezaji wa Awamu ya Pili ya Mradi wa kusambaza umeme kwenye nyumba 5,000 katika kijji cha Msomera, Saunyi na Kitwai B, wilayani Handeni, mkoani Tanga ambapo Mradi huo utagharimu kiasi cha shilingi bilioni 48.

Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga amesema, Mradi huo utakuwa endelevu na kuongeza kuwa licha kuwafikishia Wananchi huduma ya umeme katika vijiji hivyo lakini pia utawaunganisha Wananchi na huduma ya umeme (Wiring) moja kwa moja kwenye nyumba zao bila ya wao kulipia huduma hiyo.

“Nyumba 5,000 zitasambaziwa umeme pamoja na kufanyiwa “wiring”. Lengo la Serikali ni kuhakikisha Wananchi katika vijiji hivyo, mnapata umeme lakini pia mnaishi vizuri na kufanya shughuli zenu za kiuchumi”. Amesema Naibu Waziri Kapinga.

Naibu Waziri Kapinga amewaambia, wakandarasi wanaotekeleza Mradi huo kuongeza kasi katika kazi hyo pamoja na kutanguliza weledi (Professionalism) katika majukumu yao.

“Tekelezeni Mradi huu kwa wakati ili Wananchi wapate umeme kwa wakati, tunawategemea mfanye kazi kwa weledi, (Sisi) Viongozi wa Wizara ya Nishati, tupo pamoja nanyi ili kuhakikisha Miradi hii yote, inakamilika kwa wakati”. Amekaririwa Naibu Waziri, Kapinga.

Mradi huo mkubwa utatekelezwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kupitia mkandarasi, kampuni ya China Railways Construction and Electrification Bureau Group Company Ltd (CRCEBG) kwa kushirikiana na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kupitia kampuni yake tanzu ya ETDCO.

Katika mkabata huo, kampuni ya CRCEBG itajenga miundombinu ya umeme katika maeneo ya Mradi wa ujenzi wa nyumba 5,000 kwa shilingi bilioni 14.2 ambapo, mkandarasi huyo atajenga umeme wa msongo wa kati wenye urefu wa kilomita 281 pamoja na kufunga mashine umba (Transformer) 190.

Kwa upande wa kampuni ya ETDCO, nayo itajenga miundombinu ya katika maeneo yaliyobaki ya Mradi huo pamoja na kuwaunganishia Wananchi na huduma ya umeme (Wiring) kwa nyumba hizo 5,000 kwa gharama ya shilingi bilioni 33.8 na kufanya jumla ya shilingi bilioni 48 kwa Mradi wote.

Katika taarifa yake ya awali kwenye hafla hiyo; Mkurugenzi wa Umeme Vijijini, kutoka REA, Mhandisi, Jones Olotu amesema katika kijiji cha Msomera, REA imekuwa ikitekeleza Mradi wa REA III (Mzunguko wa Pili) ambapo kupitia mkandarasi huyo huyo, kampuni ya CRCEBG, imejenga miundombinu ya umeme wa msongo wa kati wa kilomita 49.4, msongo mdogo wa kilomita 146 pamoja na kuunganisha Wateja wa awali 557 ambapo jumla ya shilingi bilioni 3.7 zimetumika kugharamia Mradi huo na kuongeza kuwa Mradi utakamilika, Tarehe 31 Machi, 2024.

“Mkandarasi anaendelea kuunganisha umeme kwenye nyumba 375 ambazo hapo awali hazikuunganishwa (Wiring), mpaka sasa amejenga “line” ya umeme ya msongo mdogo ili kuunganisha nyumba 340 kati ya nyumba 375”.

“Mkandarasi, anataraji kukamilisha kazi ya kuunganisha umeme kwenye nyumba zote 375 mwezi Machi, 2024”. Amesema, Mhandisi, Olotu.

Nao wananchi wa kijiji cha Msomera wameipongeza Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa kuwafikishia huduma ya umeme, wakiongea katika nyakati tofauti, wamesema kuhamishwa kutoka eneo la hifadhi ya Ngorongoro na kumewafungulia fursa ya kuanza maisha mapya na mazuri tofauti na hapo kabla.

“Naishukuru Serikali kwa kutuhamisha kutoka Ngorongoro na kuja hapa Msomera, hapa Mimi na familia yangu, tunatumia umeme kwa matumizi, tofauti na nilipokuwa Ngorongoro, kule nilikuwa natumia vibatali, kwenye eneo la hifadhi hauruhusiwi kutumia umeme, ila hapa natumia umeme nyakati za usiku, natumia umeme kupata taarifa kwa njia ya televisheni”. Amesema Mama, Veronica Mathulda, mkazi wa kijiji cha Msomera.

Naye Bwana Yamati Masinde amesema umeme kwenye kijiji cha Msomera ni fursa kwake na kuahidi kuutimia kwa ajili ya kujiletea maendeleo.

“Ngorongoro tulikuwa hatuwashi umeme, hata umeme wa kutumia mionzi ya jua (Solar), nilikuwa siruhusiwi, kule hatukuwa na fursa ya umeme kabisa ila hapa, tuna umeme, nitautumia umeme kwa ajili ya maendeleo yangu”. Amesema Bwana Masinde.Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...