Waandishi wa Habari wametakiwa kuzidisha juhudi katika kuandika habari na makala kuhusu Sheria za habari zinazokinzana na Uhuru wa vyombo Habari ili ziweze kufanyiwa maboresho.
Hayo yamesemwa na Mwandishi Mkongwe Visiwani Zanzibar Bi. Haula Shamte wakati akiwasilisha mada juu ya Sheria kinzani dhidi ya uhuru wa Habari katika Ofisi za Tamwa Kisiwani Pemba ambazo ni Sheria ya Usajili wa Wakala wa Habari, magazeti na vitabu namba 5 ya mwaka 1988 iliyofanyiwa marekebisho na Sheria namba 8 ya mwaka 2010, Sheria ya Tume ya Utangazaji namba 7 ya mwaka 1997 iliyofanyiwa marekebisho na Sheria namba 1 ya mwaka 2010.
"Tukiangalia Sheria zote hizo tatu zinakinzana na falsafa ya Uhuru wa vyombo vya habari na Waandishi wa Habari kama ilivyoolezwa katika sura ya tatu ibara ya 18 ya katiba ya Zanzibar, hivyo basi ni jukumu letu wanahabari kuhakikisha tunaandika habari zaidi na makala mbali mbali Ili kuongeza ushawishi kwa vyombo vya kutunga Sheria katika kuzifanyia maboresho Sheria hizo" alisema


Aidha amewataka Waandishi hao kuzifahamu Sheria zinazowaongoza katika utekelezaji wa majukumu yao na zile zenye mapungufu Ili waweze kuzifanyia kazi ipaswavyo.


Alisema "Fani ya habari ni kama fani nyengine inaongozwa kwa Sheria na kanuni mbali mbali hivyo munapaswa kuzifahamu Sheria na kanuni hizo sambamba na kuzitambua vyema zile Sheria na ibara zinazokwenda kinyume na uhuru wa vyombo vya habari Ili muweze kutekeleza majukumu kwa ufanisi zaidi pamoja na kuongeza uchechemuzi kwe zile Sheria ambazo sio rafiki katika muhimili wa Habari ziweze kufanyiwa maboresho"


Mwandishiwa Habari kutoka Klabu ya Waandishi wa Habari Pemba (PPC) Amina Ahmed, alisema bado Waandishi wa Habari Kisiwani Pemba wanakabiliwa na changamoto kadhaa katika utekelezaji wa majukumu yao ikiwemo kupata vitisho kutoka kwa viongozi wa Serikali.


"Waandishi wa Habari Pemba kwasasa tunapitia wakati mgumu sana yani ukiandiga chochote kinachohusiana na kuiwajibisha taasisi au mamlaka fulani ghafla unapokea simu ya vitisho kutokana na habari hiyo na kutakiwa uifute haraka laa si hivyo utakutwa matatizo fulani hali hii inatunyima uhuru sana Waandishi"


Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Uchechemuzi na Utatezi kutoka Tamwa Zanzibar Bi. Shifaa Said Hassan, amesema endapo Waandishi Habari watatumia kalamu zao vizuri watasaidia kwa kiasi kikubwa katika kuchochea kufanyiwa maboresho Sheria hizo.


"Tumeamua kushirikiana na nyinyi Waandishi wa Habari katika kuongeza Kasi ya Uchechemuzi na Utatezi juu ya Sheria hizi kandamizi kwa vyombo vya habari na Waandishi wa Habari kwa ujumla kwa kuamini kuwa sauti zenu na kalamu zenu zinafika mbali sana na kwa haraka zaidi, hivyo basi ni wajibu wenu kuhakikisha munatumia kalamu zenu vizuri katika kuhakikisha munaandika Habari na makala mbali mbali juu ya Sheria hizi kusudi zifanyiwe maboresho" alisema Bi. Shifaa Said Hassan


Wakitoa neno baada ya kumalizika kwa mafunzo hayo Waandishi hao wameahidi kuandika habari na makala zaidi juu ya Sheria hizo zenye mapungufu kufanyiwa marekebisho Ili waweze kutekeleza majukumu kwa ufanisi.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...