Na Mwandishi Wetu
WANAWAKE wa Kata ya Toangoma, Manispaa ya Temeke, jijini Dar es Salaam, wameanzisha kikundi cha ushonaji cha kuwapa wanawake na mabinti mafunzo ya ujuzi ili waweze kujiajiri na kuajiriwa.

Akizungumza kwa niaba ya Ofisa Maendeleo kata ya Toangoma, Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Masuliza, Aziz Mwinyimkuu, amesema uanzishwaji wa kikundi cha HOREG ni hatua kubwa katika kuwakomboa wanawake wa kata hiyo.

“Sisi viongozi wenu tunawaunga mkono, tunatambua thamani ya kazi mliyoianzisha. Nimeona mnahitaji vyerehani na vitu vingine ili kufikia malengo, niwaombe wadau wote wawaunge mkono ili safari ya kumwinua mwanamke kiuchumi ifanikiwe,” amesema.

Amezitaka taasisi na kampuni zikisaidie kikundi hicho kwa vifaa vya kazi ili wanawake na mabinti waweze kupata ujuzi stahiki.

Mwenyekiti wa HOREG, Fausta Ndunguru, amesema nia ya kuanzisha kikundi hicho ni kutoa ujuzi kwa wanawake ili wapate ajira zenye staha.

“Tunajua wanawake tuna uwezo wa kufanya mambo makubwa kama tukiamua. Niwaalike wote wenye uhitaji wa ujuzi waje wajifunze, zaidi sana nawaomba wadau wa maendeleo watushike mkono ili lengo la kumkomboa mwanamke kiuchumi litimie,” amesema.

“Nitumie fursa hii kuwatia moyo wanawake popote walipo kwamba wasikate tamaa lakini niwakumbushe kwamba ujuzi ni muhimu ili tuwe kwenye ajira za heshima,” amesema.

Fausta amesema kikundi hicho kilisajiliwa Oktoba mwaka 2022, kikiwa na malengo manne ya kuwainua wanawake kiuchumi kwa kuwapa mafunzo ya ushonaji, mapambo na mapishi pamoja na kupigania utunzaji wa mazingira kwa kupanda miti.

Katibu wa Kikundi hicho, Restuta James, amesema kikundi kimefanikiwa kutoa mafunzo kwa wasichana wanne ambao watatu wameajiriwa na mafundi wengine na mmoja ameajiriwa katika ofisi za HOREG.

Amesema kikundi kinakabiliwa na upungufu wa vyerehani, nyuzi na zana nyingine za kujifunzia, kwa kuwa baadhi ya wanafunzi wanafadhiliwa na HOREG kutokana na mazingira magumu ya kifedha yanayowakabili.

“Tunaomba ufadhili wa nyuzi, vyerehani, vitambaa vya kawaida kwa ajili ya mafunzo na ufadhili wa wanawake wanaohitaji ujuzi lakini hawana uwezo. Nia yetu ni kuwainua wanawake ili wawe na ajira zenye staha,” amesema.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...