Na Mwandishi wetu
TUME ya Utumishi wa Mahakama
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania na Kamishna wa Tume ya Utumishi wa Mahakama Mhe. Mustapher Siyani amewataka Wasajili wapya wa Mahakama kuendeleza maboresho yanayofanywa ndani ya Mhimili wa Mahakama.
Akizungumza na Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Eva Kiaki Nkya na Msajili wa Mahakama Kuu Mhe. Chiganga Mashauri Tengwe mara baada ya viongozi hao kuapishwa jana, Jaji Kiongozi alisema maboresho yote yanayofanywa na Mahakama ya Tanzania yanalenga kuboresha huduma ambazo Mahakama inazitoa kwa Wananchi.
”Kwa nafasi mlizonazo sasa mna fursa nzuri zaidi ya kuwatumikia watanzania kwa kuwa Wasajili ndiyo injini au Moyo wa Mahakama ya Tanzania”, alisema Jaji Kiongozi.
Alisema Mahakama ya Tanzania imepiga hatua kubwa katika matumizi ya mifumo ya kielektroniki ili kurahisisha utoaji wa huduma zake kwa wananchi hivyo haitarajiwi viongozi hao kurudisha nyuma juhudi zilizofanyika. Aliwataka kusimamia kikamilifu utendaji kazi wa Mahakama zote nchini.
”Kufikia Mwaka 2025, Mahakama ya Tanzania itakuwa ikitoa huduma zake zote kwa mtandao, na tayari safari hiyo imeshaanza hivyo ninyi mnapaswa kuwa madereva wetu wazuri”, alisema Jaji Kiongozi.
Kuhusu ufanisi katika kazi zao, Mhe. Siyani aliwashauri Viongozi hao wapya kuwa na utamaduni wa kujipima wenyewe utendaji kazi wao kwani kujipima wao wenyewe ni vizuri kuliko kusubiri kukosolewa au kusikia malalamiko.
Awali akizungumza wakati wa hafla ya kuapishwa kwa Msajili wa Mahakama Kuu, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es salaam Mhe. Salma Maghimbi aliwataka Wasajili hao kuongeza kasi ya usimamizi wa kazi za Mahakama kwa kuwa Mahakama tayari imepiga hatua kubwa kiteknolojia.
Alisema Usimamizi wa kazi za Mahakama hauna budi kuwa mzuri ili mafanikio ya kiteknolojia yaendane na uwekezaji mkubwa uliofanywa na Mahakama ya Tanzania.
Wasajili wapya walioapishwa ni Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Eva Kiaki Nkya ambaye aliapishwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Chiganga Mashauri Tengwe aliyeapishwa na Jaji Kiongozi Mahakama Kuu ya Tanzania.
Chiganga Mashauri Tengwe akila kiapo cha kuwa Msajili wa Mahakama Kuu Tanzania mbele ya Jaji Kiongozi Mustapha Siyani. Hafla hiyo imefanyika leo Mahakama Kuu katika ofisi ya Jaji Kiongozi. Wanaoshuhudia, (wa pili kulia) ni Mtendaji Mkuu wa Mahakama, Ole Gabriel na Projestus Kayoza Naibu Msajili wa Mahakama kuu.
Jaji Kiongozi wa Mahakam Kuu Tanzania, Mustapha Siyani akiwa katika picha ya pamoja na watendaji wa mahakama Kuu mara baada ya kumuapisha Msajili wa Mahakama Kuu, Chiganga Mashauri Tenngwa (wa kwanza kushoto.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...