Na Nasra Ismail

MJUMBE wa Mkutano Mkuu Taifa wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Sango Kasera Gungu ambaye pia ni mdau wa maendeleo Wilaya ya Rorya mkoani Mara amedai kushindwa kuendelea na mpango wa ugawaji wa madawati kwenye shule 132 ambazo zimekuwa na changamoto ya uhaba wa madawati kwa madai ya kuzuiliwa na Mkuu wa Wilaya hiyo akishirikiana na Mwenyekiti wa CCM wilayani humo.

Akizungumza wakati wa kusitishwa kwa msaada huo kutokana na kukosa ushirikiano kutoka kwa watendaji,Sango amedai kushangazwa na kitendo hicho kwani jambo alilokuwa analifanya ni msaada wa kunusuru watoto kukaa chini na kuunga mkono jitihada za Rais Samia Suluhu Hassan za kuwajenga mazingira bora ya kujifunzia wanafunzi.

“Zoezi hili tumeanza mwezi mmoja uliopita kwa kufuata taratibu zote kwa kuandika barua kwa Mkuu wa Wilaya,Katibu wa CCM Wilaya ya Rorya, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Rorya na Mwenyekiti wa Chama lakini nimesikitika baada ya Mkuu wa wilaya kunipigia simu na kuniambia nisitishe ugawaji wa msaada...

"Kwani majukumu ya kuleta maendeleo ni ya Serikali na sisi tulikuwa tunafanya kwa nia nzuri tu kwasababu tunaamini maendeleo yanaletwa na sisi wana Rorya na mimi sijafanya peke yangu nina marafiki zangu wanafanya kazi zao kwenye wilaya ya Roryar ambao wamekuwa wakiniunga mkono kwa kutoa vitu kwani hawatoi fedha,”Sango.

Aidha ameongeza kuwa awali zoezi hilo lilizinduliwa na Mkuu wa Wilaya ya Rorya Juma Chikoka ambaye alitoa ridhaa ya kumruhusu kuendelea na shughuli nzima ya ugawaji lakini hatima ya mwisho baada ya kugawa kata mbili ndipo alipigiwa simu ya kukatazwa kwa madai yawezekana akawa anajipalilia kupata ubunge mwaka 2025.

“Ninaomba kumuondoa wasiwasi Mkuu wa wilaya na Mwenyekiti wangu wa Chama kwani mimi sitoi msaada kwa kujionesha au kwa kutaka kitu fulani kama wao wamekuwa wakidhani nataka ubunge sina mpango wa ubunge wala udiwani.

"Ninachofanya ni kuwasaidia wadogo zetu ambao wapo shuleni na wala sio kutafuta madaraka au sifa yoyote hile kwenye jamii yangu” Sango Kasera Gungu Mjumbe wa Mkutano Mkuu Taifa wa Chama cha Mapinduzi (CCM)

“Nasikitika Pia hata Mwenyekiti amekuwa akiwapigia wajumbe na wanachama wa CCM wasije kwenye makabidhiano, nimekabidhi kata ya Chigunga.Mkuu wa wilaya nilimuita na kumuomba awepo akasema hayupo atatuma mwikilishi ambaye ni ofsa elimu,"amedai.

Ameongeza kwamba lakini kilichoendelea alizuiliwa asikabidhi msaada huo ,hivyo amesikitishwa,

Kutokana na madai haya kumuelekezea Mkuu wa Wilaya hiyo, Juma Chikoka yeye amesema wilaya anayoiongoza haijazuia wadau wa maendeleo kutoa misaada ya kielimu na mingine jambo la msingi ni wao kufuata utaratibu wa kukabidhi misaada wanayoitoa kwenye mamlaka na sio kwenda kukusanya watu pasipo kufuata utaratibu wa unaotakiwa.

“Kwanza nimpongeze Mjumbe wa Mkutano Mkuu Taifa Sanga Kasera anachokifanya ni jambo zuri na ndicho ambacho serikali inahamasisha na kuwaomba wadau mbali mbali wajitokeze kuongeza nguvu na kuunga jitihada za Rais za kutaka kuona maendeleo kwenye sekta ya elmu yanakua kwa kasi kubwa.

"Tumepokea misaada mbalimbali ya madawati na vitanda lakini hawa wote wamekuwa wakifuata utaratibu wa kuja na kukabidhi ofisini kwa Mkuu wa wilaya kwa maana ninapopokea na mimi nampatia Mkurugenzi yeye anajua wapi kwenye shida na mwisho wa siku anagawa msaada huo”Juma Chikoka.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Rorya Ongujo Wakibara amesema wao jukumu lao ni kusimamia utekelezaji na kukagua utekelezaji wa Ilani na yeye anauwezo wa kumzuia mtu yoyote."Kinachotakiwa ni mtu au taasisi zinazotaka kutoa msaada kufuata taratibu zilizowekwa kwa mujibu wa Sheria."



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...