MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango ameagiza kuangaliwa upya kwa sheria zinazohusu uhifadhi wa mazingira ili kuliwezesha Baraza la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) na Halmashauri kuwa na nguvu ya kuchukua hatua kali dhidi ya uharibifu wa Mazingira.

Makamu wa Rais ametoa maagizo hayo wakati akifungua Kongamano la Wadau wa Mazingira lililofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere Dar es Salaam.

Amesema uchafuzi wa mazingira katika Majiji, Miji na Halmashauri bado ni tatizo huku uharibifu wa misitu ukiendelea kuwa changamoto licha ya kuwepo kwa vyombo vya kuishauri Serikali juu ya masuala ya utunzaji wa misitu na mazingira pamoja na kuwepo kwa Sheria ndogo katika ngazi ya Serikali za mitaa.

Aidha Makamu wa Rais amewasihi Watanzania kuacha mazoea ya kukata miti na kutupa taka hovyo na kuziagiza Mamlaka za Serikali za Mitaa zihakikishe kuwa Kampuni zinazopewa kazi ya kuzoa taka ziwe na uwezo wa kufanya kazi hizo kwa ufanisi.

Vilevile Makamu wa Rais ameiagiza Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia, Wizara ya Kilimo na Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuhimiza wataalamu katika vyuo hapa nchini na taasisi za utafiti kufanya utafiti mahususi kwa ajili ya kupambana na kuenea kwa jangwa kwa kutumia teknolojia na ubunifu.

Ameutaka uongozi wa mikoa inayokabiliwa na kuenea kwa jangwa ikiwa ni pamoja na Halmashauri kuchukua hatua za ziada kupanda miti pamoja na mazao yanayostahimili ukame kama mitende.

Makamu wa Rais ametoa wito kwa Watendaji wote wa Wizara, Wakuu wa Mikoa, Mamlaka za Serikali za Mitaa na wadau wengine, kuhamasisha na kutoa elimu kwa Wananchi juu ya utunzaji wa mazingira ili kukabiliana na madhara yanayosababishwa na mabadiliko ya tabianchi.

Amesema ni vema kuelimisha umma kuachana na mila potofu zinazoharibu misitu, vyanzo vya maji na uoto wa asili na kuhimiza matumizi ya Nishati safi ili kupunguza matumizi ya kuni na mkaa.

Halikadhalika Makamu wa Rais ametoa rai ya matumizi ya lugha ya kiswahili katika machapisho yote ya utunzaji wa mazingira ili walengwa ambao ni wananchi wa Tanzania waweze kuelewa juu ya masuala ya mazingira kirahisi.

Kwa upande wake Waziri Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira Dkt. Selemani Jafo amesema Kongamano hilo linafanyika wakati muhimu ambapo madhara makubwa ya uharibifu wa mazingira yanaonekana hapa nchini na maeneo mengine Barani Afrika.

Amesema nchi za Mashariki mwa Afrika zinakabiliwa na mvua kubwa na mafuriko huku nchi za Kusini mwa Afrika zikishuhudia kiwango kikubwa cha ukame.

Aidha Waziri Jafo amesema Wizara imesimamia zoezi la upandaji miti kufikia azma ya miti milioni 276 kwa mwaka ambapo mpaka hivi sasa jumla ya miti milioni 266 imepandwa nchi nzima na miti milioni 211 sawa na asilimia 79 inaishi.

Pia amesema Wizara inaendelea na mradi wa shilingi bilioni 26 wa urejerezaji wa maeneo yalioharibiwa katika mikoa ya Iringa, Njombe, Mbeya, Songwe, Rukwa na Katavi.

Akitoa taarifa ya Kongamano hilo Mkurugenzi wa Baraza la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Dkt. Immaculate Semesi amesema Taasisi hiyo itaendelea kujitathimini, kujiimarisha na kujiboresha zaidi katika kutimiza majukumu ya kuishauri serikali katika usimamizi wa mazingira nchini.

Amesema NEMC itaendelea kufumbua, kutetea na kuelimisha juu ya uhifadhi na usimamizi wa mazingira na kuhakikisha uwepo wa kanuni imara zaidi na kuongeza ufahamu kwa jamii.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akizindua Chapisho la Hali ya Mazingira ya Pwani na Bahari ya Tanzania Bara wakati wa Kongamano la Wadau wa Mazingira lililofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere Dar es Salaam tarehe 31 Mei 2024.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akionesha tuzo iliyotolewa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwa kinara wa katika kulinda na kuhifadhi mazingira iliyotolewa wakati wa Kongamano la Wadau wa Mazingira lililofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere Dar es Salaam tarehe 31 Mei 2024. (Kushoto ni Waziri Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira Dkt. Selemani Jafo)

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akihutubia wakati akifungua Kongamano la Wadau wa Mazingira lililofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere Dar es Salaam tarehe 31 Mei 2024.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akishiriki Kongamano la Wadau wa Mazingira lililofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere Dar es Salaam tarehe 31 Mei 2024.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akisalimiana na Viongozi mbalimbali wakati akiwasili katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere Dar es Salaam kufungua Kongamano la Wadau wa Mazingira tarehe 31 Mei 2024.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akisikiliza maelezo kutoka kwa Mwandishi wa Vitabu kwaajili ya watoto katika uhifadhi wa Mazingira na Wanyama Bi. Annastella Mtoka wakati akikagua mabanda ya maonesho katika Kongamano la Wadau wa Mazingira lililofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere Dar es Salaam tarehe 31 Mei 2024.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akisikiliza maelezo kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Usimamizi wa Mazingira nchini (NEMC) Dkt. Immaculate Semesi wakati akikagua mabanda ya maonesho katika Kongamano la Wadau wa Mazingira lililofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere Dar es Salaam tarehe 31 Mei 2024.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akizindua Chapisho la Hali ya Mazingira ya Pwani na Bahari ya Tanzania Bara wakati wa Kongamano la Wadau wa Mazingira lililofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere Dar es Salaam tarehe 31 Mei 2024.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...