*Awashangaa kumchonganisha Rais Samia kwasababu tu ni Mzanzibar

*Apangua hoja Kuhusu madai Katiba mpya,Sheria mpya ya uchaguzi


Na Said Mwishehe, Dodoma


MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana ameshauri wananchi kutokubali hoja za kejeli, chuki na kugombanisha watu zinazotolewa na CHADEMA.

Pia Kinana amesema viongozi wa CHADEMA kwa katika mikutano yao ya hadhara wamekuwa wakieneza chuki na kumchanganisha Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa hoja dhaifu kwamba anatoka Zanzibar na amekuwa anaihujumu Bara.

Akizungumza leo Mei 5,2024 Wana CCM pamoja na wananchi alipokuwa katika mkutano maalumu wa CCM Mkoa wa Dodoma, Kinana amesema CHADEMA katika mizunguko yao wameituhumu CCM, Serikali na Rais kwa hoja za uongo.

"Hatukatai kukoselewa, hatukatai kusahihishwa, lakini hatukubali kuzuliwa au kushutumiwa kwa mambo ambayo hayapo. Kubwa ambalo wamefanya ni kujenga chuki miongoni mwa Watanzania, kujenga mifarafakano.

"Wakaenda mbali zadi wakaanza kuzusha jambo ambalo wanataka kuifanya ajenda, wanasema nchi ina Rais ambaye ni Mzanzibari na anaihujumu Bara, lakini ajenda hiyo imeshindwa."

Ameongeza CHADEMA wanazungumza kuhusu Rais Samia ni Mzanzibar, hana huruma na Bara, hana jema analofanya kwa Bara, hana msaada.

“Wanataka kumtenganisha Rais na Watanzania, nani amekataa kwamba Rais Samia sio Mzanzibari. Ni Mzanzibari na ametokana na Katiba ambayo inaeleza mgombea urais akitoka Zanzibar basi mgombea mwenza anatoka upande wa pili…

“Ndivyo tulivyokubaliana na huyu ni mgombea mwenza ana nafasi sawa na mgombea urais. Ikitokea mgombea mwenza hayuko uchaguzi unaahirishwa. Mwaka 2005 uchaguzi uliahirishwa kwa sababu mgombea mwenza wa CHADEMA alifariki dunia.

“Halafu leo wanakejeli kiongozi kutoka Zanzibar, wametafuta namna ya kushughulika na Rais (Dk. Samia) lakini wakiangalia barabara zinajengwa, bwawa la mwalimu Nyerere limefika pazuri, ujenzi wa mji wa Dodoma unaendelea kwa kasi.

“Reli ya mwendo kasi sasa imefika Dodoma na ujenzi unaendelea sasa wanakosa hoja wanakuja na maneno ya kuzusha kwamba Rais hafai kwa sababu anatoka Zanzibar. Rais Samia ni Rais wa katiba amechukua uongozi baada ya Rais Dk. John Magufuli kufariki dunia,” alisema.

Ameongeza kwamba “Rais Samia alikuwa Mgombea Mwenza akawa Makamu wa Rais, na awamu ya pili Magufuli akamteua tena lakini oooh… huyo Mzanzibar ili watu baadae polepole waanze kusema tunatawaliwa na Mzanzibari.”

Amewaomba Watanzania kupuuza uzushi huo na kushauri wasimame na Rais Samia kwani anafanya kazi nzuri.

"Tangu awamu mbalimbali zilizopita kuna sera iliyoanza baada ya Mzee Mwinyi kuchukua nchi kwa kuanzisha sera ya sekta binafsi kushiriki kukuza uchumi.

“CHADEMA wanasema Rais Samia anauza kila kitu, kauza nini?. Awamu ya Tatu Rais mstaafu Benjamin Mkapa alibinafsisha mashirika zaidi ya 200 kwani alikuwa Mzanzibar?

“Wakati TICS wanapewa bandari ya Dar es Salaam nchi haikuuzwa, lakini baada ya kupewa DP World nchi inauzwa. Hivi mnaamini kweli Rais anaweza kukaa na kufanya jambo ambalo halina nia njema na nchi yetu.

“Rais haamui peke yake kuna vyombo ambavyo vinakaa na kuangalia mambo na kisha vinamshauri Rais. Kataeni juhudi zinazofanyika za kujenga chuki dhidi ya Rais. Kuna wakati Shirika la Reli Tanzania (TRC) lilikabidhiwa kwa RITES (kampuni) kutoka India? Alikabidhi Rais Samia?”

Kinana amesema hayo mambo yanafanyika kwa malengo na hasa kuleta tija na ufanisi, hivyo Watanzania wasikubali kusikiliza hoja rejareja, hoja za msimu.

Pia amesema Rais Samia ambaye wanamsema ndiye ameleta uhuru wa kusema, kushutumu, kuandamana. Mikutano ya hadhara wanaweza kusema iko katika Katiba lakini huko nyuma wakati wananyimwa kwani haikuwepo kwenye Katiba?.

“Katiba ilikuwepo, uhuru ulikuwepo lakini walikatazwa kwenda barabarani. Amekuja Rais muungwana ameondoa kifungo. Akisema kuanzia leo hakuna maandamano, watafanya? Wanamkejeli na kumtuhumu Rais amekaa kimya.

“Waamuzi ni wao. Wana CCM dawa yao kwenye sanduku la kura, wenzetu wanatafuta nguvu katika sanduku la kura. Watanzania hawapendi kejeli. Nina uhakika adhabu watakayopata watajutia.

Kuhusu hoja ya Katiba, sheria mpya ya uchaguzi na muungano Kinana amesema kwamba ukisikiliza kwa makini utabaini wanataka kuleta mfarakano kati ya bara na Zanzibar.

“Wamekuwa wakizunguka na ajenda ya kuligawa taifa katika majimbo, hii ni sera ambayo wamekuwa nayo kwa muda. Msimamo wa CCM Watanzania tusikubali kugawanywa kwa namna yoyote,” amesema Kinana.

Akizungumzia Katiba mpya ,Kinana amesema kulifanyika mazungumzo kwa mwaka mzima baina ya CHADEMA na CCM na kwa maoni yao walisema si ajenda yao ya sasa, lakini Kamati Kuu baada ya ushawishi wakakubali.

“Kimsingi Katiba hatukatai lakini wenzetu wanataka Katiba ipatikane leo, katika kile kikao walituambia tunaelewa Katiba hii haitakuwa leo lakini tunawasihi mkubali uwepo wa Katiba, tukatoa tamko na muda mwafaka tutakubaliana.

“Wenzetu wanasema wanataka Katiba sasa, katika mkutano uliofanyika ukumbi wa Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam Rais alisema Katiba mpya haiwezi kuwa ya vyama vya siasa peke yao,”amesema.

Ameongeza Katiba ya sasa imefanyiwa marekebisho mara 14 na sababu ukiangalia sio mambo yaliyohusu wananchi bali ni Siasa, madaraka na uchaguzi.








Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...