Na Kassim Nyaki, Ngorongoro.

Mamlaka ya Hifadhi ya eneo la Ngorongoro (NCAA) leo tarehe 20 Mei,2024 imehitimisha kilele cha wiki ya  maadhimisho ya siku ya Makumbusho duniani katika bonde la Makumbusho ya olduvai kwa kutoa mafunzo kwa wanafunzi wa shule za Sekondari kuhusu utafiti wa malikale, urithi wa utamaduni, miongozo inayotumika kufanya utafiti na uchimbaji wa masalia ya malikale (excavation).

Katika maadhimisho hayo Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro Kanali Wilson Sakulo ameupongeza uongozi wa NCAA kwa kutekeleza kwa vitendo kauli mbiu ya Maliasili na Utalii ya tumerithishwa, tuwarithishe kwa kutoa mafunzo ya utafiti wa uchimbaji wa malikale kwa wanafunzi wa shule za Sekondari ambao ndio watafiti wa baadae.

“Nawapongeza NCAA kwa kuwa kauli mbiu ya tumerithishwa tuwarithishe imefanyika kwa vitendo, nimeona zaidi ya wanafunzi 60 wakiwa na uelewa wa kutosha kuhusu dhana za utafiti wa malikale ambazo wamezielezea kwa ufasaha kupitia onesho walilofanya katika makumbusho ya Olduvai” ameongeza kanali sakulo.

Kanali Sakulo ameupongeza uongozi wa NCAA kwa uboreshaji wa miundombinu ya Bonde la olduvai ikiwemo ujenzi wa makumbusho ya kisasa, njia za kutembea (walking trail), mtandao wa internet, kituo cha maelezo (information centre), ujenzi wa vyoo vya kisasa na uboreshaji wa makumbusho ya kihistoria ya Dkt. Marry Leakey.

Kaimu Kamishna wa Uhifadhi Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro Vicktoria Shayo ameeleza kuwa katika kuadhimisha siku hii NCAA imeendelea kujenga mazingira wezeshi kwa watafiti mbalimbali wanaokuja kufanya utafiti katika bonde la Olduvai smbamba na kutembelea shule mbalimbali zilizoko ndani hifadhi na nje ya hifadhi ili kuwajengea uwezo wanafunzi kujua masomo ya historia, malikale, chimbuko la binadamu na shughuli za tafiti katika bonde la olduvai.

Kamishna Shayo amebainisha kuwa maboresho ya miundombinu katika vituo vya malikale sambamba na kutangaza maeneo hayo kumechangia ongezeko la wageni ambapo katika eneo la Olduvai pekee wageni wanaotembelea hilo wameongezeka kutoka 9,799 mwaka 2020 hadi kufikia wageni 24,290 mwaka 2023.

Kaimu meneja wa Idara ya Urithi wa utamaduni na mambokale Dkt. Agness Gidna amebainisha kauli mbiu ya maadhimisho ya mwaka huu ni Makumbusho, Utafiti na elimu ambapo Shirika la Kimataifa la Makumbusho (ICOM) huratibu tukio hilo na zaidi ya makumbusho 160 duniani zimeadhimisha siku hii kwa lengo la kuongeza ufahamu wa mambo ya urithi wa utamaduni unaoonekana na usioonekana pamoja na mazingira yake kwa madhumuni ya elimu na utalii.

Dkt. Gidna amefafanua kuwa Mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro inasimamia makumbusho tatu (3) ambazo ni Makumbusho ya Olduvai Gorge (inayoonesha asili  na chimbuko la binadamu), Makumbusho ya  Dk. Mary Leakey (inayoonesha  historia ya watafiti, nyumba na vifaa vya kisayansi vilivyotumika katika utafiti miaka ya 1930) na  Makumbusho ya Kimondo cha mbozi (iliyohifadhi historia ya jamii za mikoa ya nyanda za juu Kusini)

Kwa upande wake katibu mtendaji wa UNESCO tawi la Tanznaia Profesa Hamis Malebo ameeleza kuwa eneo la Hifadhi ya Ngorongoro ni eneo la kipekee duniani kwa kuwa ni hifadhi pekee la Urithi wa dunia yenye hadhi tatu (03) ikiwemo tabaka hai la Kimataifa (Biosphere reserve), Urithi mchanganyiko wa Dunia (Mixed world heritage site) na Jiopaki ya Ngorongoro Lengai (Ngorongoro Lengai UNESCO Global geopark) ambayo ni ya pili pekee kwa nchi za Afrika.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...