WADAU wa vyombo vya habari wameiomba serikali ya Mapinduzi Zanzibar kukamilisha mchakato wa marekebisho ya sheria za habari zilizotolewa maoni na wadau ili  kutoa mazingira rafiki kwa waandishi wa habari kutekeleza majukumu yao bila vikwazo.

Imeelezwa kwa muda mrefu licha ya wadau mbalimbali kutoa na kuwasilisha mapendekezo yao kuhusu mapungufu yaliyopo kwenye baadhi ya sheria hizo, lakini utekelezaji wake bado umekuwa wa kusuasua jambo linalopelekea mazingira magumu ya utendaji kazi wa vyombo vya habari nchini.

Mkurugenzi wa Chama cha Waandishi wa Habari Tanzania, Zanzibar (TAMWA ZNZ), Dkt. Mzuri Issa alieleza mchakato wa mabadiliko ya sheria za habari umekuwepo kwa miaka mingi lakini bado sheria hizo ambazo nyingi ni za muda mrefu zimekwama kurekebishwa.

"Sisi wengine tangu tuko waandishi chipukizi tunazungumzia kupata hizi sheria mpya za habari, tangu 2008 kwa kweli ni muda mrefu, tunahitaji kusimamia jambo hili kwa umoja wetu na hatimae tupate sheria mpya za habari Zanzibar," alieleza Dkt. Mzuri katika kongamano hilo.

Aliongeza wadau wa habari wamefanya mapitio ya sheria nane za habari ikiwemo Sheria ya usajili wa wakala wa habari, magazeti na vitabu namba 5 ya mwaka 1988 iliyofanyiwa marekebisho na sheria no.8 ya 1997, Sheria ya Tume ya Utangazaji Zanzibar namba 7 ya mwaka 1997  iliyorekebishwa na sheria namba 1 ya mwaka 2010 na kuwasilisha ripoti ya mapendekezo yao kwa mamlaka husika ikiwemo kukutana na Rais na waziri.

Aliongeza kuwa "tumewahi kuzungumza na Mhe. Rais kuhusu sheria hizi na Waziri pia, nadhani inabidi tupange kuzungumza nao tena ili tuone hili linakwendaje. Haitapendeza hata kidogo tumalize mwaka huu na bado hatujapata mabadiliko ya sheria za habari.”

Akigusia kuhusu uhuru wa vyombo vya habari na mabadiliko ya tabianchi, Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), Ernest Sungura, alieleza vyombo vya habari vitatekeleza kwa ufanisi wajibu wao katika kulinda mazingira iwapo waandishi watakuwa huru kupata na kutoa taarifa bila hofu kisheria.

Alieleza, “kaulimbiu ya kimataifa mwaka huu ilijikita katika uhifadhi wa mazingira. Lakini kwakweli bila kuwa na sheria nzuri za habari hatuwezi kutekeleza hayo tunayoyataka. Waandishi wa habari tunahitaji uhuru wa kupata taarifa ili tuweze kutekeleza uandishi wa habari mahususi. Hatuwezi kuyatekeleza hayo kama sheria hazitutengenezei mazingira ya kulinda uhuru wetu.”

Katika hatua nyingine alivitaka vyombo vya habari kubuni mbinu mpya za kukabiliana na changamoto za kiuchumi na kufikiria namna ya kuendana na kasi ya mageuzi ya masuala ya kiteknolojia ili kulinda uhuru wao.

"Sahizi changamoto kubwa inayoathiri uhuru wa habari ni masuala ya kiuchumi katika vyombo vya habari. Tunaitaji kuangalia upenyo ili kuona namna gani kile kinachosababisha madhara katika vyombo vya habari kinatatuliwa," alibainisha katibu mtendaji huyo.

Akifafanua kuhusu maendeleo ya mchakato wa mabadiliko ya sheria za habari Zanzibar, Katibu Mtendaji Tume ya Utangazaji, Suleiman Salim alieleza tayari mapendekezo ya sheria hizo yapo ofisi ya mwanasheria mkuu wa serikali kwaajili ya hatua zaidi.

"Kwa sasa mswada wa sheria ya habari ipo kwa mwanasheria mkuu, na tunaitegemea itakwenda baraza la wawakilishi kama mswada na tunawaomba walioko kule waichangie vizuri ili iweze kupita na tupate sheria mpya," Suleiman Salim, Katibu Mtendaji Tume ya Utangazaji aliwaambia wadau.

Aidha Suleiman alisema tayari serikali imekamilisha mchakato wa kuandaa Sera mpya ya habari Zanzibar na kuwatoa hofu wadau wa habari juu ya uwepo wa sera hiyo kuwa itazinduliwa muda sio mrefu.

Akichangia mdahalo kwenye maadhimisho hayo, Salim Said ambaye ni mwandishi wa habari mkongwe alieleza uwepo wa sheria bora ni muhimu katika kuwezesha mazingira bora ya waandishi wa habari kuwajibika.

"Vyombo vya habari ni washirika wa maendeleo, hivyo kuwa na sera na sheria bora itawawezesha waandishi wa habari kuwa na mazingira rafiki katika  kutekeleza majukumu yao," alifahamisha, mwandishi wa habari huyo mkongwe Zanzibar.

Maadhimisho ya siku ya uhuru wa vyombo vya habari 2024 yameandaliwa Baraza la habari Tanzania Ofisi ya Zanzibar (MCT ZNZ), Chama cha Waandshi wa Habari Tanzania Zanzibar (TAMWA,ZNZ) Jumuiya ya Waandishi wa Habari za Maendeleo (WAHAMAZA), Klabu ya Waandishi wa Wabari Zanzibar (ZPC) na Shirika la Commonwealth Foundation yakiambatana na kaulimbiu ya  “UHURU WA VYOMBO VYA HABARI NA MAGEUZI YA SERA NA SHERIA ZA  HABARI ZANZIBAR.”

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...