Na Mwandishi wetu, Mirerani
Kampuni ya uchimbaji madini ya Tanzanite Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, Heroes Mining Camp imetoa msaada wa vyakula kwa yatima waliopo eneo hilo.

Msaada huo wa vyakula kwa watoto yatima walio chini ya miaka 14 ikiwemo mchele, sukari, majani ya chai na mafuta ya kupitia umegharimu kiasi cha shilingi milioni 2.

Mkurugenzi wa kampuni ya Heroes Mining Camp Basil Roman Njau akizungumza wakati akitoa msaada huo amesema hawajaanza kupata uzalishaji wa madini ila wametoa msaada huo ili iwe sadaka kwao.

"Mimi na mke wangu tumetoa kiasi hicho kwa ajili ya sadaka ya kusaidia yatima na endapo madini yatatoka mgodini kwetu tutawasaidia zaidi," amesema Njau.

Mwenyekiti wa shirika lisilo la kiserikali la Saidia Wanajamii Tanzania (SAWATA) Mohamed Issa Mghanja amesema Mkurugenzi wa kampuni ya Heroes Mining Camp, Basil Roman Njau ana moyo wa ukunjufu wa kusaidia jamii.

Amesema kwenye msaada huo wamewashirikisha wenyeviti wa vitongoji vyote ili kupata yatima wenye uhitaji halisi hivyo wakawachukua wale wenye hali ngumu kabisa.

Amesema katika ugawaji huo wameshirikisha kaya 67 yenye watoto yatima 111 ambapo kwenye lita 140 za mafuta kila mmoja atapata lita moja, kila mtoto atapata kilo moja na nusu ya mchele na kilo moja na nusu ya sukari na paketi ya majani ya chai.

"Wajane wengine wana watoto wawili au watatu au wanne na kila mmoja atapata shea yake na mama zao watakula hapo hapo kupitia watoto wao," amesema Mghanja.

Amesema yatima wengi wa Mirerani wametokana na baba zao kufariki dunia kutokana na vumbi walilolipata kwenye shughuli za uchimbaji madini migodini.

Ofisa mtendaji wa mamlaka ya mji mdogo wa Mirerani (TEO) Isack Mgaya ameipongeza SAWATA kwa kusimamia zoezi hilo kwa uwazi na ushirikishwaji.

"SAWATA tumefanya nao kazi kwa muda mrefu bado ni asasi mahiri yenye uadilifu kwani kazi zao hazina kona kona zimenyooka na zinaaminika," amesema Mgaya.

Mmoja kati ya waliopatiwa msaada huo Elizabeth John ameishukuru kampuni hiyo kwa kuwasaidia yatima hao ambao wengi wao wamewapoteza baba zao.

"Kiasi hicho cha chakula kitawasaidia yatima hawa kwa muda wa siku kadhaa na tunawashukuru mno kwa moyo wa upendo mkubwa Mungu awabariki," amesema.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...