Na Said Mwishehe, Michuzi TV-Makambaku

UKWELI ni kwamba Bohari ya Dawa (MSD) imedhamiria kuhakikisha inaendeleza mkakati wake wa kuzalisha bidhaa za afya ikiwemo mipira ya mikononi maarufu ‘glaves’.

Ukiwa katika kiwanda chake cha kuzalisha glaves kilicopo eneo la Idofi Halmashauri ya Makambako mkoani Njombe utashuhudia kiwanda hicho ambacho ujenzi wake ulianza Oktoba 4, 2020 kikiendelea na uzalishaji ulioanza rasmi Februari mwaka huu na hadi sasa jozi milioni mbili za glaves zimeshatengenezwa.

Ni wazi MSD chini ya uongozi mahiri wa Mkurugenzi Mkuu wake Mavere Tukai imeamua kubeba kwa vitendo dhamira ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha kiwanda cha Gloves Idofi kinazalisha mipira ya mkono na hatimaye kuokoa fedha ya serikali iliyokuwa ikitengwa kuagiza mipira hiyo nje ya nchi.

Akizungumza na wahariri kutoka vyombo mbalimbali vya habari waliotembelea kiwanda hicho, Mhandisi Shiwa Mushi ambaye ni Kaimu Meneja Kiwanda cha Glovu MSD Idofi anaeleza hatua kwa hatua kuhusu sababu za kuanzishwa kwa kiwanda hicho na uzalishaji unaoendelea kwa sasa.

HISTORIA YA KIWANDA

Kwa mujibu wa Mhandisi Mushi, kiwanda hicho kinamilikiwa na MSD na kilianza kujengwa Oktoba 4, mwaka 2020 na dhumuni la kujengwa kwake ni kutokana na changamoto ya ugonjwa wa Uviko-19 mwaka 2019.

“Wakati wa janga la Korona miongoni mwa changaoto tulizozipata kama taasisi na nchi kwa ujumla ni uingizaji wa vifaa tiba nchini, kutokana na vizuizi na uagizaji wa dawa ilikuwa changamoto kubwa.

“Kwa hiyo nchi ikaona kuna haja pia kuanza kuanzisha viwanda vyake hasa kutokana na somo ambalo tumelipata na tukaona kiwanda cha aina ya glaves ni muhimu tukaanza nacho kwasababu tumekwenda kwenye changamoto ya upungufu wa vifaa tiba nchini.

“Na ukiweza kuvaa glaves utaweza kuwahudumia wagonjwa hata kama ni wa Korona kwa usalama zaidi. Kwa hiyo tukaanza na kiwanda cha gloves ambacho kimejengwa Idofi, Makambako katika eneo lenye ukubwa wa ekari 38 na MSD inalimiki kisheria na ililitwaa kutoka kwa wananchi wa Idofi, tumewalipa na sasa eneo hili lina hati.”

MAJENGO YALIYOPO

Mhandisi Mushi anaeleza katika eneo hilo la kiwanda kuna majengo mengi yanayotoa picha ya kiwanda hicho na jengo hilo la kiwanda lina urefu wa mita 130 na upana mita 124 kwa maana kwamba ukiangalia mita za mraba 3,120.

Anasema katika hayo majengo lipo jengo la malighafi kwa ajili ya uzalishaji na majengo mawili mengine wamepanga yatakuwa kituo cha kiwanda cha gloves na wakiendelea na uzalishaji vizuri na kufanya biashara watajenga majengo mengine.

“Kwa upande wa kulia kwenye michoro yetu kuna majengo ambayo kwa sasa yapo kwa ajili ya uhifadhi wa bidhaa,” anafafanua.

AINA MBILI ZA GLOVES

Pamoja na hayo anasema mikakati ya kiwanda ni kuzalisha aina mbili za glaves ambazo ni Surgical glove (zinatomika kuvaa kwenye upasuaji) na Examination glave (Glavu zinazovaliwa wakati wa uchunguzi wa awali).

KIMEBAKISHA SEHEMU MBILI

Akitoa maelezo zaidi ya kiwanda hicho, Mhandisi Mushi anasema kimebakisha sehemu mbili katika mkakati wa uzalishaji huku akifafanua kuwa kinakwenda kuzalisha pisi 20,000 ambazo ni sawa na pea 10,000 na hiyo ni kama kinazalisha katika hali yake ya kawaida.

“Na kiwanda hiki ukifanya mahesabu kitaalamu inaonesha kwa mwaka kitazalisha jumla ya glaves jozi milioni 86.4, ambazo ni sawa na asilimia 86.34 ya mahitaji ya nchi.

“Kwa hali hii unaweza kuona kiwanda hiki ni kikubwa kwa kiasi gani, na sasa tumebaki na uzalishaji wa Examinationa glaves, ambapo katika kuzalisha kunahitajika malighafi.”

MALIGHAFI INAYOTUMIKA

Wakati huo huo anasema kuwa malighafi mama inayotumika kutengeneza gloves ni utomvu ambao hutokana na mti wa zao la mpira na kinachofanyika huvunwa ule uteute kama maziwa na kisha huchanganywa na baadhi ya kemikali ili kufikia viwango vya kuzalisha.

Anasema utomvu unapopatikana unakuwa kwenye utayari na hutumika kama malighafi kwenye uzalishaji. Katika kuzalisha kuna hatua kadhaa ambazo gloves hupitia ili kuwa bidhaa bora na salama.

HATUA ZA UZALISHAJI

Mhandisi Mushi anasema katika uzalishaji wa gloves kuna hatua mbalimbali kwa sababu bidhaa ya afya inahitaji umakini na usafi wa hali ya juu. Hatua ya kwanza ni kusafisha na kuna sampuli za mikono ambazo husafishwa na huingizwa kwenye maji ikiwamo Acid (kemikali) ambazo huandaa mikono kwa ajili ya kupokea malighafi.

Baada ya hapo zinaingizwa kwenye malighafi yenyewe ya mikono ambapo kuna taratibu kadhaa hufanyika ikiwamo kuzikausha.Kisha zinakwenda kwenye kemilika mingine ya Rich Process ili kuondoa madhara na hutumika saa moja kwenye mchakato wa ukaushaji wa mipira ya mikono.

Ukishamilika hatua inayofuatia ni uvuaji na kwa upande wa Surgical zina mtambo wa uvuaji kwa sababu Surgical ni proces (mchakato). Zikishavuliwa zinapelekwa maabara kwani inafahamika bidhaa za afya zinahitaji umakini sana kwasababu zinatumika katika mwili wa binadamu.

SABABU ZA KUINGIA MAABARA

Mhandisi Mushi anasema gloves inaingia maabara kwasababu ya kuangalia ubora na kuhakikiwa na baada ya hapo zinakaushwa na kisha zinaingizwa sehemu nyingine ya pili clean room (chumba kisafi). Hiyo maana yake ni sehemu ambayo hakuna vijidudu.

“Kwa hiyo bidhaa inaingia kule inajaribiwa na baada ya kujaribiwa huwekwa kwenye vifungashio (Parckage Material). Inapelekwa sehemu maalum ikiwemo ya kuhifadhia ambayo huitwa Karantini ambapo watalaam wanakagua kama mzigo upo vizuri.

“Na baada ya hapo huchukuliwa kwa ajili ya kuingia sokoni. Kwakifupi mpaka tunatoa glaves kama nilivyosema Batch moja ya uzalishaji inahitaji karibia saa moja. Kiwanda hiki kinafanya hivyo.

UZINDUZI RASMI

Pamoja na maelezo hayo, kiwanda hicho kilizinduliwa rasmi Februari 12 mwaka huu na Makamu wa Rais Dk. Philip Mpango huku Mhandisi Mushi akifafanua kilianza uzalishaji baada ya baada ya kupata vibali vyote vya mamlaka kikiwemo kibali cha ubora kutoka TMDA.

“TMDA wamekuja mara kadhaa kutukagua na tukawa tunafanyia kazi ushauri na maelekezo yao na baada ya kuridhika wakatupa kibali cha Certificate of Compliance na pia tukapewa na kibali cha usajili wa bidhaa.

“Pia tukapewa vibali na Jeshi la Zimamoto na Ukoaji ambao walikagua na wakatoa cheti, pia tulikaguliwa na GSLA ambao waliangalia matumizi na udhbiti wa kemikali kama tupo sawa.”

BAADA YA VIBALI

Kwa mujibu wa Mhandisi Mushi anasema baada ya kupata vibali hivyo kiwanda kilianza uzalishaji Februari mwaka huu na mpaka sasa wamezalisha jozi milioni mbili za gloves(mipira ya mkono).

UZALISHAJI MARA TATU KWA WIKI

Katika wiki wameamua kuwa na uzalishaji kwa siku tatu ambazo ni Ijumaa, Jumamosi na Jumapili kwa sababu hutumia malighafi ya utomvu na kemikali. Wanafanya uzalishaji kwa siku tatu ili kutoa nafasi ya kufanya matengenezo makubwa na madogo ya mitambo.






Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...