*Yapongezwa kwa kuunga mkono shughuli za jamii, Elimu yatakiwa kuwa msingi wa usalama barabarani na ulinzi binafsi wa wanafunzi

KAMPUNI Ya TotalEnergies Marketing Tanzania imezindua rasmi msimu wa tatu wa programu ya 'Via Road Safety' mahususi kwa ajili ya usalama barabarani kwa wanafunzi huku ikielekezwa kuwa elimu hiyo iende sambamba na usalama wao kijinai kwa kuhakikisha wanafunzi hawarubuniwi na yeyote pindi wanapotumia barabara.

Akizungumza leo katika Shule ya Msingi Makuburi jijini Dar es Salaam wakati akizindua msimu wa tatu wa programu ya 'Via Road Safety' iliyodhaminiwa na Kampuni ya TotalEnergies Marketing Tanzania pamoja na Nafasi Art Space mahususi kwa ajili ya elimu ya usalama barabarani kwa wanafunzi; Mkurugenzi wa Sheria kutoka Kitengo cha Usalama Barabarani SSP. Deus Sokoni ameishukuru Serikali kupitia Taasisi ya Elimu kwa jitihada za kuona kunakuwa na mtaala wa elimu ya usalama barabarani kwa wanafunzi wa shule za Msingi na Sekondari.

"Ni jitihada za ziada ambazo Serikali inafanya kuona kundi hili la watoto linalindwa wanapotumia barabara. Mwezi wa pili Taasisi ya Elimu ilikuwa inapitia vitabu mbalimbali ambavyo vitatumika kufundisha kuanzia ngazi ya Chekechea hadi Sekondari lengo ni kuwajengea msingi wa usalama Barabarani na wadau TotalEnergies wamekuwa wadau wa kuunga mkono jitihada hizo katika kuhakikisha wanafunzi wanakuwa salama." Amesema.

SSP Sokoni amesema, Elimu ni muhimu zaidi kwa makundi yote ya barabara hususani kundi la wanafunzi ambalo linatakiwa kupewa elimu zaidi ili wakue katika kutambua misingi ya usalama barabarani na kuwa mabalozi kwa wengine.

Ameipongeza TotalEnergies Marketing Tanzania kwa kuendelea kuwa wadau muhimu katika kuhakikisha kundi la wanafunzi linakuwa salama na kuwataka wadau hao kwenda mbali zaidi kwa kuwafikia watoto waliopo mikoani.

Aidha amewataka watoto kujiepusha na tabia hatarishi kutoka kwa watu wengine kwa kukataa zawadi na lifti kutoka kwa watu wasiowafahamu.

" Katika mashindano haya watoto wapate elimu ya kufahamu elimu ya usalama barabarani kwa ujumla na vishawishi vyote vinavyoweza kuwapata pindi wanapotumia barabara...Walimu wajengewe uwezo wa kuwafundisha watoto masuala ya usalama barabarani." Amesema.

Akimwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa TotalEnergies Tanzania, Mkurugenzi wa Sheria na Uhusiano wa Kampuni ya TotalEnergies Marketing Tanzania Getrude Mpangile amesema; mradi huo ni matokeo ya madhara ya ajali za barabarani zinazohusisha watoto na kuwaacha na madhara ya kudumu ikiwemo ulemavu hali inayokwamisha kutimiza ndoto zao katika elimu.

"Kutokana na sababu hizo TotalEnergies Foundation kwa kushirikiana na TotalEnergies Marketing Tanzania tulianzisha mradi huu wa elimu ya usalama barabarani unaotambulika kama 'Via Road Safety' ili kuchangia katika kupunguza madhara yanayotokana na ajali za barabarani kwa kuwaelimisha watoto wetu kutumia barabara kwa uangalifu na kufuata kanuni na sheria." Amesema.

Getrude amesema, Mpaka sasa watoto zaidi ya kumi na sita elfu wamenufaika na mradi huo tangu ulipoanza na kwa mwaka huu wanatarajia kuwafikia watoto elfu sita katika shule sita za Mkoa wa Dar es Salaam.

" Tunaishukuru Serikali ya Tanzania kwa kuhakaikisha usalama barabarani unazingatiwa hususani kwa watoto tunaunga mkono jitihada hizo. Mradi huu pia unatarajiwa kuanzisha klabu za mabalozi wa usalama barabarani na mwaka huu tunatarajia kupata mabalozi 120 wenye umri wa miaka tisa hadi kumi na nne ambao watasaidia mradi huo kuwa endelevu kwa kuwafundisha wenzao na kufanya elimu hiyo kuwa endelevu." Ameeleza.

Aidha amesema, Mradi huo utatoa fursa ya elimu kwa wanafunzi za Msingi za Umma na kwa kushirikiana na wadau wakiwemo Nafasi Art Space ambao wamekuwa wakiwafundisha watoto juu ya usalama barabarani kupitia ubunifu wa nyimbo, mashairi na maigizo ambayo yamekuwa yakipeleka ujumbe kwa ufanisi zaidi kwa wanafunzi hao.

Mpangile amesema; Uzinduzi wa mradi huo na mashindano kupitia 'Via Road Safety' kwa msimu huu wa tatu: katika mashindano ambayo washindi hupata zawadi mbalimbali na fursa ya kushiriki mashindano Barani Afrika na baadaye Ulimwenguni kwa mwaka huu kipekee zaidi mshindi atapata zawadi ya kutatuliwa tatizo lililooneshwa.

"Kwa miaka hii tuliyofanya mradi huu watoto wamekuwa wakiibua matatizo mbalimbali kuhusiana na Usalama barabarani.....Shule hii ya Makuburi mwaka jana walionesha changamoto ya kutokuwepo kwa ukuta kwenye sehemu ya shule hali iliyopelekea usalama finyu kutokana na pikipiki kukatiza katika maeneo ya shule kwa mwaka huu mshindi atapatiwa fedha ya kutatua changamoto aliyoionesha." Amesema.

Mathalani amewataka watoto hao kuzingatia elimu wanayopewa na kuwa mabalozi kwa wanafunzi wenzao kuhusu usalama wa barabarani na hiyo ni pamoja na kuzingatia mashindano hayo kwa kuwa wabunifu zaidi ili kushiriki katika ngazi za juu zaidi.

Pia Mkurugenzi wa Nafasi Art Space Lilian Hipolyte amesema kuwa; Wamejikita kutoa elimu kupitia Sanaa na mradi huo wa kutoa elimu ya usalama Barabarani kupitia Sanaa utawasaidia wanafunzi kuwa salama wakati wa matumizi ya barabara na kuwa mabalozi kwa wanafunzi wenzao.

Amesema kupitia ubunifu na kujieleza kwa njia ya Sanaa kutahamasisha wanafunzi na jamii kwa ujumla kukumbuka kuishi kwa usalama kwa kutumia barabara na miundombinu yake.

Ameeleza kwa mwaka huu hamasa imeongezeka ambapo Shule sita zitapata mafunzo na kuwa klabu maalum za usalama barabarani pamoja na mabalozi wa mradi huo, huku shule zitakazonufaika ni Shule za Msingi Makuburi, Buza, Jangwani Beach, Ungindoni, Ubungo NHC na Sinza Uzuri ambazo zimejumuisha Wilaya zote za jiji la Dar es Salaam.

Pia Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Makuburi Mohamed Athumani amesema, madawati 70 yaliyotolewa yakakidhi upungufu wa madawati katika shule hiyo na kuondoa kero ya wanafunzi kukaa chini.

Ameishukuru TotalEnergies Marketing Tanzania kwa kushiriki katika shughuli za kijamii hususani katika suala la usalama barabarani kwa ustawi wa elimu kwa wanafunzi.

Machi 28 mwaka huu Kampuni ya TotalEnergies ulimwenguni ilitimiza miaka 100 na katika kusherekea maadhimisho hayo wamejizatiti katika kusaidia jamii ikiwemo kuboresha elimu na katika kutekeleza hilo wamekabidhi madawati 70 kwa shule ya Msingi Makuburi.

Mkurugenzi wa Sheria na Uhusiano wa Kampuni ya TotalEnergies Marketing Tanzania Getrude Mpangile (kushoto,) akikabidhi moja ya dawati kwa Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Makuburi Mohamed Athumani (kulipa,) katikati ni Mkurugenzi wa Sheria kutoka Kitengo cha Usalama Barabarani SSP. Deus Sokoni.
Mkurugenzi wa Sheria na Uhusiano wa Kampuni ya TotalEnergies Marketing Tanzania Getrude Mpangile akizungumza wakati wa uzinduzi huo na kueleza kuwa; mradi huo ni matokeo ya madhara ya ajali za barabarani zinazohusisha watoto na kuwaacha na madhara ya kudumu ikiwemo ulemavu hali inayokwamisha kutimiza ndoto zao katika elimu.



Matukio mbalimbali wakati wa hafla hiyo.
 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...