Berega, Kilosa

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema kiasi cha Shilingi bilioni 1.2 zilizobaki wakati wa ujenzi wa Daraja la Berega zitumike kuboresha barabara ya Berega - Kinyolisi - Makuyu kwa kujenga daraja moja la mawe lenye urefu wa Mita 45 (stone arch-bridge), Ma-boksi Kalavati. 

Fedha hizo pia zitajenga Madrifti 6, na kuweka changarawe katika maeneo korofi ili barabara hiyo iweze kupitika katika majira yote ya mwaka ambapo kazi hiyo ya maboresho ya barabara imeanza.

Dkt. Samia aliyasema hayo jana wakati akiongea na wananchi wa Berega ikiwa ni muendelezo wa ziara yake Mkoani Morogoro.

Alisema barabara hiyo ya kiwango cha changarawe itaanzia ng’ambo ya daraja hilo mpaka Kijiji cha Makuyu Km. 18.7 inapounganika na barabara ya Gairo -Kilindi inayohudumiwa na TANROADS.

“Injinia amesema hapa wamefanya matumizi mazuri sana ya fedha kwenye ujenzi wa daraja hili na zimebaki Shilingi bilioni 1.2 ambazo zinakwenda kutumika kuboresha barabara ya kiwango cha changarawe, kujenga madaraja sita na makaravati 15, hivyo kuifanya iweze kupitika wakati wote.

Aidha, alisema anaamini barabara hiyo itaweza kupitika misimu yote na kurahisisha usafiri wa binadamu na bidhaa zao.

Naye, Mtendaji Mkuu wa TARURA Mhandisi Victor Seff alisema kwamba daraja hilo limesanifiwa kuwa na uwezo wa kubeba tani 120 kwa wakati mmoja na kudumu kwa miaka isiyopungua 100.

Aliongeza kusema kuwa daraja hilo limejengwa kwa zege na nondo na linabebwa na nguzo mbili za pembeni (aburtments) na nguzo sita za katikati (Piers),”nguzo zote zimejengwa juu ya msingi wa nguzo ndefu 67 (piles) zenye kina cha wastani wa mita 15 kutoka usawa wa kitanda cha mto”.

Hata hivyo alisema ujenzi wa daraja hilo umehusisha pia kazi za kuzuia mmomonyoko wa udongo pembezoni mwa mto. 

Daraja la Berega lina urefu wa mita 140 na upana wa mita 10.5, mita 7.5 kati ya hizo ni kwa ajili yakupitisha magari na mita 3.0 yaani mita 1.5 kila upande ni mabega ya daraja kwa ajili ya usalama wa watembea kwa miguu na waendesha baiskeli. 


-Mwisho-

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...