MKURUGENZI wa Shirika la Msichana Initiative, Rebeca Gyumi, amesema katika kipindi hiki ambacho vikao vya bunge vinaanza, kuna haja kwa wadau wa kutetea haki za wasichana na wanawake kuendelea kupaza sauti na kuwakumbusha wabunge wasipitishe kifungu cha 10(b) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ya Ngono.

Kwa mujibu wa Rebeca, kifungu hicho kinahalalisha na kuendeleza matumizi mabaya ya madaraka kwa kutaka yule anayeomba na anayetoa rushwa hiyo ya ngono wote wahukumiwe.

“Suala la rushwa ya ngono linahusu mamalaka, kwa maana ya watu wanaotumia mamlaka vibaya kunyima au kuminya haki ya wale ambao wako chini, na hapa nchini ni moja ya changamoto kubwa inayochangia wasichana na wanawake wasijitokeze kugombea katika nafasi mbalimbali za uongozi,” alisema Rebeca.

“Sisi kama watetezi wa haki za wasichana na wanawake hatukubaliani na hayo mapendekezo kwa sababu tunaamini yataendeleza suala la rushwa ya ngono badala ya kutoa msukumo wa kulimaliza suala hilo, hivyo inabidi wote tupaze sauti kwa sababu tunaona kwamba hata ile tafsiri ya rushwa ya ngono yenyewe inataka kutolewa.”

Akizungumza katika hafla ya kuhitimisha mradi wa kuwawezesha wasichana viongozi unajulikama kama Sauti Yetu, Nguvu Yetu, uliochini ya Shirika Msichana Initiative, Rebeca alisema wanaongeza nguvu zaidi kuwapa mbinu wasichana ambao wameonesha nia ya kutia nia katika chaguzi zijacho namna ya kushinda vikwazo vinavyotokana na rushwa hiyo ya ngono.

“Kupitia mradi wetu wa Sauti Yetu, Nguvu Yetu ambao tumefikia wasichana 200 katika mikoa minne, kati ya hao wapo ambao wameonesha nia ya kutia nia katika nafasi mbalimbali za uongozi kwenye chaguzi zijazo, kwa hiyo tumewapa mbinu ya kupambana na kuiishinda rushwa hiyo ya ngono, hatutaki iwakatishe tamaa na washindwe kutimiza ndoto zao,”alisema Rebeca.

“Tunataka wafahamu kwamba rushwa ya ngono ni kinyume cha Katiba ya nchi, kwa hiyo wanaopoona wanaombwa wawe na nguvu ya kuripoti.”

Baadhi ya wasichana viongozi wanaotarajia kugombea katika chaguzi hizo za zerikali za mitaa na uchaguzi mkuu, walisema wako tayari kupambania nafasi za uongozi ili waongeze nguvu ya kutafuta  haki za wasichana.

“Katika maeneo mengi niliyotembea nimegundua kwamba wasichana bado wako nyuma sana na wanaogopa kuingia kwenye vinyang`anyiro vya uongozi hasa kwenye siasa, wanaogopa vikwazo vilivyopo hasa suala la kuombwa rushwa ya ngono, kwa hiyo mimi nimeamua nijikaze niingie na ninaamini kushinda kupitia uwezo wangu binafsi,”alisema Loveness Athuman kutoka Nzega Tabora.

“Inabidi wasichana tujitokeze safari hii tuwe wengi tukiamini kwamba hata kama kuna ambao watashindwa lakini wapo baadhi watafanikiwa na itakuwa ndiyo nafasi ya kufikisha ajenda za kutetea wenzetu wengi ambao wanakandamizwa katika maeneo mbalimbali.”

Mwajuma Hima, kutoka Ubungo, aliwaomba wasichana hao,  kujitokeza kwa wingi kugombea nafasi mbalimbali za uongozi katika chaguzi zijazo akiwataka wasiogope vikwazo vya rushwa ya ngono isipokuwa wawe na uthubutu wa kuwaripoti wale wanaowaomba rushwa hiyo kwa mamlaka husika.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...