MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), imekutana na wadau kutoka sekta mbalimbali nchini ili kujipanga na Utabiri wa Msimu wa VULI 2024 katika ukumbi wa PSSSF, jijini Dodoma, tarehe 19 Agosti, 2024.
Akifungua mkutano huo, Mwenyekiti wa Bodi ya TMA, Jaji Mshibe Ali Bakari, aliwahimiza wadau kutoka sekta mbalimbali walioshiriki katika mkutano huo kutoa maoni yao sambamba na kutekeleza maazimio ya mkutano yatakayoafikiwa.
”Tunapoelekea kutoa utabiri wa mvua za Vuli (Oktoba hadi Disemba), 2024 ninawahimiza wadau kutumia jukwaa hili katika kutoa michango ya maoni yenu kikamilifu ili kuleta tija kwa sekta mbalimbali nchini pamoja na kutekeleza maazimio yatakayofikiwa”. Alisema Jaji Mshibe.
Jaji Mshibe alisisitiza kuwa matumizi sahihi ya taarifa za hali ya hewa ni muhimu hususani katika kipindi hiki ambapo dunia pamoja na nchi yetu inakabiliwa na changamoto za mabadiliko ya hali ya hewa.
“Ninapenda kutoa msisitizo kwenu, katika majadiliano ya mvua za Vuli ya mwaka huu, 2024, mjikite katika kujadili namna ya kuimarisha matumizi ya utabiri wa hali ya hewa mtakaopewa na kushauri hatua stahiki za kuchukua”. alisisitiza Jaji Mshibe.
Akizungumza awali Makamu mwenyekiti wa Bodi TMA, Dkt Emmanuel Mpeta” ameipongeza TMA kwa kazi nzuri ya kuimarisha ubora na usahihi wa utabiri hususan katika kipindi hiki ambacho Dunia inakabiliwa na mabadiliko ya hali hewa, na kuwaomba wadau wa sekta mbalimbali kuwasilisha maoni yao ya kuimarisha ushauri kwa sekta na jamii.
Wakati akimkaribisha mgeni rasmi, Kaimu Mkurugenzi Mkuu, TMA na Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Mabadiliko ya Sayansi ya Hali ya Hewa na Tabianchi, Dkt.Ladislaus Chang’a aliishukuru Serikali kwa kuendelea na uwekezaji katika miundombinu ya hali ya hewa hapa nchini, alisema kupitia jitihada hizo, Mamlaka imeendelea kuboresha na kuimarisha huduma za hali ya hewa ikiwemo kutoa taarifa za utabiri wa maeneo madogo madogo kwa wilaya zote 86 za mikoa iliyopo katika ukanda unaopata mvua za Vuli na hivyo kusaidia katika kufanya maamuzi stahiki kwa lengo la kuongeza tija na kupunguza madhara ya hali mbaya ya hewa inapojitokeza.
“Niishukuru serikali na wadau wa maendeleo kwa kuendelea kuwekeza katika miundombinu ya hali ya hewa hapa nchini” Alisema Dkt. Chang’a.
Dkt. Chang’a aliendelea kusema kuwa mvua za Vuli ni mahsusi kwa maeneo yanayopata misimu miwili ya mvua kwa mwaka ambayo ni pwani ya kaskazini, nyanda za juu kaskazini mashariki, na ukanda wa Ziwa Victoria zenye mchango mkubwa katika sekta mbalimbali zikiwemo kilimo, nishati, maji n.k.
Aidha, ilielezwa kuwa taarifa sahihi za hali ya hewa pamoja na athari zake ni muhimu kupatikana kwa wote na kwa wakati ili kuwezesha jamii na wadau kujipanga na kuandaa shughuli za kiuchumi na kijamii katika maeneo yao.
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania, inatarajia kutoa taarifa rasmi ya msimu wa mvua za Vuli tarehe 22 Agosti 2024.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...