Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kinondoni, na Diwani wa Kata ya Mwananyama, Bw. Songoro Mnyonge amesema msaada wa madawati 1000 unaotolewa na Benki ya Biashara ya DCB, unaunga mkono juhudi za Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan za kuwaletea wananchi wake  maendeleo kupitia sekta ya elimu.

 Mstahiki Meya Songoro aliyasema hayo jijini Dar es Salaam jana, katika Shule ya Msingi Msisiri B, wakati akipokea msaada wa madawati 30 yalitolewa na DCB kwa ajili ya shule hiyo, huku madawati yaliyosalia yakitarajiwa kupelekwa katika shule  zenye uhitaji mkoani humo.

 

“Benki ya DCB mmeishika mkono serikali, tunawashukuru sana, serikali haiwezi kufanya kila kitu, ushirikiano kutoka kwa wadau ni jambo muhimu, leo benki hii imeanza, natoa wito kwa wadau wengine wajitokeze kuwekeza katika elimu ya watoto wetu ili tuweze kuwa na Taifa bora la baadae.

 

“Manispaa ilileta madawati 100, Mwananyama peke yake kila siku wanazaliwa watoto 100, hii ni Mwananyamala tu, bado maeneo mengine, maana yake kwa watoto wanaozaliwa sasa, baada ya miaka sita kutakuwa na mahitaji makubwa ya madawati, hivyo suala hili linapaswa kuwa endelevu”, alisema mstahiki meya.

 

Awali akizungumza kabla ya kukabidhi madawati hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya DCB, Bw. Sabasaba Moshingi alisema msaada huyo unaenda sambasamba na makusudi halisi ya kuanzishwa kwa benki hiyo, miaka 22 iliyopita ikiwa ni kuinua maisha ya watanzania wenye kipato cha chini.

 

“Mwaka uliopita DCB tulitoa madawati 1000 katika shule mbalimbali na kwa mwaka huu tumedhamiria kutoa tena madawati 1000, Shule ya Msingi Msisiri B imebahatika kuwa ya kwanza, benki yetu itaendelea kushirikiana na serikali yetu katika kutatua changamoto mbalimbali zinazojitokeza, hususan katika sekta ya elimu.

 

 “Mbali na hili DCB itaendelea kuboresha huduma zake za kibenki ili ziweze kwenda sambamba na mahitaji halisi ya watanzania, huku tukiunga mkono juhudi za mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan katika jitahada zake za kuhakikisha huduma za kibenki zinawafikia watanzania wengi zaidi na katika kila kona ya nchi”, alisema Bw. Moshingi.

 

 Benki ya Biashara ya DCB ilianzishwa mwaka 2002 na mwaka unaofuata kupewa leseni ya kujiendesha kama benki ya kijamii, ikijulikana kama Benki ya Watu wa Dar es Salaam ‘Dar es Salaam Community Bank’ ambayo wanahisa wake waanzilishi wakiwa ni Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam pamoja na Manispaa zake za Ilala, Kinondoni na Temeke. Wanahisa wengine ni Mifuko ya NHIF na UTT AMIS pamoja na wananchi wa kawaida.

 



Kuanzishwa kwa DCB kulitokana na maono ya Rais mstaafu wa awamu za tatu, Hayati Benjamin William Mkapa kutoka na kilio cha wananchi wenye kipato cha chini na cha kati kukosa mikopo ya mitaji katika benki za kibiashara kutokana na kutokidhi vigezo vilivyowekwa.

Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kinondoni na Diwani wa Kata ya Mwananyamala, Bw. Songoro Mnyonge ( wa tatu kushoto) na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Biashara ya DCB, Bw. Sabasaba Moshingi (wa tatu kulia), wakikata utepe kuashiria makabidhiano ya msaada wa madawati 30 kwa shule ya msingi Msisiri B yaliyotolewa na DCB, shuleni hapo, jijini Dar es Salaam leo. DCB inatoa madawati 1000 kwa mwaka huu kwa shule mbalimbali za msingi ikiwa ni jitihada za benki hiyo katika kusaidia uboreshaji wa sekta ya elimu.Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Bw. Songoro Mnyonge ( wa pili kulia) na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Biashara ya DCB, Bw. Sabasaba Moshingi wakishangilia pamoja na baadhi ya wanafunzi wa shule ya msingi Msisiri B katika hafla ya makabidhiano madawati 30 yaliyotolewa na DCB kwa shule hiyo, jijini Dar es Salaam leo.Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Biashara ya DCB, Bw. Sabasaba Moshingi akizungumza wakati wa hafla ya wakati wa hafla ya ya makabidhiano ya msaada wa madawati 30 kwa shule ya msingi Msisiri B yaliyotolewa na DCB, shuleni hapo, jijini Dar es Salaam leo.


Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kinondoni, na Diwani wa Kata ya Mwananyama, Bw. Songoro Mnyonge (wa pili kulia) akizungumza na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Biashara ya DCB, Bw. Sabasaba Moshingi ( kulia), na maofisa wengine wa benki hiyo, wakati wa hafla ya makabidhiano ya msaada wa madawati 30 kwa shule ya msingi Msisiri B yaliyotolewa na DCB jijini Dar es Salaam leo. Kutoka kushoto ni Mkurugenzi wa Biashara, Bw. Ramadhani Mganga na Mkurugenzi wa Fedha, Bw. Siriaki Surumbu.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...