Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya Nyasa mkoani Ruvuma Khalid Halif akitoa taarifa ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo iliyotekelezwa na Halmashauri hiyo kwenye kikao cha Baraza la madiwani kilichofanyika jana.
Na Mwandishi Wetu, Nyasa
HALMASHAURI ya wilaya Nyasa mkoani Ruvuma,imefanikiwa kuvuka lengo la makusanyo
ya mapato yake ya ndani baada ya kukusanya Sh.bilioni 1.824 sawa na asilimia
104 kati ya lengo la kukusanya Sh.bilioni 1.7 kwa mwaka wa fedha ulioisha
tarehe 30 Juni 2024.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Khalid Khalif alipokuwa
akitoa taarifa ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo kwa kipindi cha
robo ya nne Julai 2023 hadi tarehe 30 Juni 2024 katika kikao cha Baraza la
madiwani.
Alisema,kwa mwaka 2023/2024 Halmashauri ya wilaya Nyasa ilipokea
Sh.bilioni 9,018,973,000.00 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo
kati ya fedha hizo Sh.bilioni 4,664,725,000.00 ni fedha za ndani na Sh.bilioni
4,364,248,000.00 ni fedha za nje.
Kwa mujibu wa Khalif Sh.milioni 181,120,000.00 sawa na asilimia 20 zimetengwa
kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo kutoka mapato ya ndani ya
Halmashauri hivyo kufanya jumla ya fedha zilizotengwa kuwa Sh.bilioni
9,200,093,000.00.
Aidha alisema,kwa mwaka wa fedha 2024/2025 Halmashauri imeongeza ukomo wabajeti
ya makusanyo ya ndani kwa zaidi ya asilimia 50 kufikia Shilingi bilioni 2.4.
Alieleza kuwa, shughuli ya ukusanyaji kwa mwaka husika imeanza vizuri kwani katika
kipindi cha mwezi Juni hadi Agosti tayari asilimia 15 ya bajeti nzima imeshakusanywa.
Hata hivyo, Khalif ametoa wito kwa wakusanyaji wote wa Halmashauri kusimama
imara kuhakikisha mianya ya uvujaji wa mapato inazibwa kikamilifu ili lengo la
makusanyo ya mwaka liweze kufikiwa ipasavyo.
Alisema,kupitia bajeti hiyo wananchi wa wilaya ya Nyasa wanakwenda kufaidika
kupitia utekelezaji na ujenzi wa miradi ya maendeleo kwenye maeneo yao ikiwemo
mapato ya asilimia 10 kwa makundi ya vijana,wanawake na wenye ulemavu
yaliyotengewa Sh.milioni 240.
Alisema kuwa,katika bajeti hiyo wametenga asilimia 20 ambayo itakwenda
kutumika kutekeleza miradi ya maendeleo ambapo mkakati wa Halmashauri ni
kuendelea kuongeza nguvu kwenye ukusanyaji wa mapato yake ili iweze
kufikia malengo yaliyokusudiwa kwa ajili ya kutoa huduma bora za kijamii kwa
wananchi..
Katika hatua nyingine, Khalif alieleza,katika kipindi cha Julai 2023 hadi
Juni 2024 cha mwaka wa fedha 2023/2024 Halmashauri ya wilaya Nyasa imetumia
kiasi cha Sh.bilioni 9,127,738,685.05 sawa na asilimia 67.8 ya fedha zilizopokelewa
na bakaa.
Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Nyasa Peres Magiri alisema,kwa mwezi Agosti
2024 Halmashauri hiyo ilipaswa kukusanya Sh.milioni 200 lakini kutokana na
usimamizi mbovu wa vyanzo vya mapato ilikusanya Sh.milioni 108.
Magiri alisema kuwa
hayo ni matokeo ya uzembe wa baadhi ya watumishi kutosimamia ipasavyo
ukusanyaji wa Maputo ya ndani.
Alisema,hali hiyo imetokana na baadhi ya wataalam na watendaji wa vijiji na kata kushindwa kuwajibika ambapo ameitaka menejimenti ya Halmashauri
kuwachukulia hatua watumishi wanaoshindwa kutekeleza majukumu yao
hususani kwenye usimamizi wa makusanyo ya mapato ya ndani.
Magiri alisema,wilaya ya Nyasa ina vyanzo vingi vya mapato ikiwemo zao maarufu
la kahawa lakini baadhi ya watendaji hawawajibiki ipasavyo na wengine
wamesababisha mashine zinazotumika kukusanya mapato (Pos) kuharibiwa na
kupelekea kukosekana kwa taarifa sahihi ya fedha zinazokusanywa kama
mapato ya halmashauri.
‘’Kwa hili la ukusanyaji wa mapato katika katika Halmashauri yetu kuwa na hali
mbaya mmenisikitisha sana,sasa nawaagiza viongozi wenzangu pamoja na madiwani
,Mkurugenzi ,watalaamu na watendaji ni lazima tuchukue hatua za pamoja
kusimamia makusanyo ya mapato na kwa wale watakaobainika kwenda kinyume na
maagizo haya wachukuliwe hatua za kisheria ikiwemo kuwasimamisha kazi bila
kuwaonea haya’’ alisema Magiri.
Amewaagiza wataalam katika Halmashauri hiyo kujitathimini juu ya
utendaji wao wa kazi,na kuwataka kufanya mapitio ya kodi ,tozo ushuru na
utunzaji wa kumbukumbu na kuimarisha mfumo wa ukusanyaji kupitia mfumo wa
kielektroniki ili kudhibiti upotevu wa mapato.
Akizungumza kwa niaba ya madiwani wenzake,Diwani wa kata ya Kilosa Elias
Katulu,amehaidi kwenda kutekeleza maagizo yote yaliyotolewa na Mkuu wa wilaya
yenye lengo la kuimarisha mfumo wa ukusanyaji wa mapato ya Halmashauri yao.
Baadhi ya Wakuu wa idara za Halmashauri ya wilaya Nyasa mkoani Ruvuma,wakimsikiliza Mkuu wa wilaya hiyo Peres Magiri(hayupo pichani)alipokuwa akitoa salamu za serikali kwenye kikao cha Baraza la madiwani kilichofanyika jana katika ukumbi wa Halmashauri hiyo.
Baadhi ya madiwani wa Halmashauri ya wilaya Nyasa mkoani Ruvuma,wakifuatilia taarifa ya utekelezaji wa miradi na shughuli za maendeleo kutoka kwa Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Khalid Halif(hayupo pichani)kwenye kikao cha Baraza la madiwani kilichofanyika jana katika ukumbi wa Halmashauri hiyo.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...