Mmoja wa wachezaji ambaye pia ni Rais wa Chama cha Gofu kwa wanawake ( Tanzania Ladies Golf Union- TLGU) Queen Siraki akiwa mazoezini kujiandaa na michuano maarufu ya Tanzania Ladies Open Championship itakayoanza jijini Arusha Ijumaa wiki hii
Wachezaji wa gofu wakiwa tayari kwa ajili ya michuano ya Tanzania Ladies Open Championship itakayoanza Arusha Ijumaa wiki hii
Na Mwandishi Wetu, Michuzi TV
MICHUANO maarufu ya mchezo wa gofu kwa wanawake inayojulikana kama Tanzania Ladies Golf Open inaanza Ijumaa wiki hii jijini Arusha na kuvutia wachezaji mbalimbali wa kitaifa na kimataifa.
Kwa mujibu wa Rais wa chama cha gofu cha wanawake hapa nchini ( Tanzania Ladies Golf Union-TLGU) Queen Siraki, maandalizi yamekamilika, huku baadhi ya washiriki kutoka nchi jirani za Kenya na Uganda wakitarajiwa kuingia nchini muda wowote kuanzia sasa.
“Tungependa kuwajulisha Watanzania na wapenda mchezo wa gofu kuwa ile michuano yao maarufu ya ‘Tanzania Ladies Open Championship’ kwa mwaka huu 2024 imekaribia,”
“Hivyo, tunawaomba watu mbalimbali kujitokeza, yakiwemo makampuni, taasisi, watu binafsi na wafanyabiashara kwa ajili ya kutuunga mkono na kusaidia ukuaji wa mchezo huu hapa nchini,” amesema Siraki.
Amesema mchezo huu umekuwa kwa kasi hapa nchini na baadhi ya taasisi, zikiwemo benki zimekuwa zikijitokeza na kuunga mkono jitihada za Serikali za kukuza michezo hapa nchini.
Amezitaja taasisi hizo zilizojitokeza kudhamini michuano ya mwaka huu kuwa ni pamoja na Benki ya Taifa ya Biashara (NBC), Kampuni ya Bia ya Tanzania (TBL), Benki ya NCBA, Dorgen Group Limited na Kukunde.
“Tunawashukuru wadhamini wote kwa msaada wao wa thamani, ambao umekuwa muhimu katika kuinua kiwango cha gofu ya wanawake nchini Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla,”, amesema Siraki, akitoa wito wito kwa wadau wengine kutumia fursa ya michuano hii kujitangaza.
Michuano hii ya mashimo 54 itakayofanyika kwa siku tatu, mbali na shindano kuu la wanawake, pia litajumuisha mashindamo ya ziada kwa wanaume na vijana, yaliyogawanywa katika Divisheni A, B, na C.
Aidha, kutakuwa na zawadi kwa mshindi wa mpigo mrefu ( Longest Drive) na mshindi wa kupiga karibu na shimo (Nearest to Pin).
“Hii ni moja ya matukio makubwa ya mchezo wa gofu kwa wanawake kwenye kalenda ya kimataifa ya mchezo huu, yakivutia wachezaji zaidi ya 100 maarufu wanaoshindania tuzo mbalimbali,” alisema Siraki.
“Kinachofanya tukio la mwaka huu kuwa la ushindani zaidi ni kwamba wachezaji wa nyumbani walifanya vizuri kwenye mashindano ya wanawake ya Kenya na Uganda yaliyopita.
“Hivyo, wachezaji wageni wamejipanga kulipiza kisasi,” aliongeza.
Siraki alisema kwamba wachezaji wa ndani wamekuwa wakijiandaa kwa bidii kuhakikisha wanashinda tuzo nyumbani.
Miongoni mwa wachezaji wanawake maarufu wanaotegemewa kushiriki ni Ayne Magombe, Neema Olomi, Madina Iddi, Hawa Wanyeche, na Vicky Elias.
Siraki alisema kuwa wachezaji hawa wa nyumbani wamekuwa wakijitayarisha kwa zaidi ya wiki moja mkoani Arusha, tayari kutoa ushindani kwa wachezaji wageni.
“Mashindano haya ni moja ya matukio makubwa yanayovutia wachezaji wa kimataifa na watazamaji,” alisema Siraki.
“Ni mashindano muhimu pia kwa kuandaa wachezaji wa nchi za Afrika Mashariki kwa matukio makubwa ya kimataifa, ikiwa ni pamoja na Kombe la All Africa Golf Challenge linalopangwa kufanyika mwezi Novemba nchini Morocco.”
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...