TIMU za Kamba za Wanaume na Wanawake pamoja na Timu ya Netiboli kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii zimefuzu hatua ya 16 bora katika Mashindano ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI), 2024 yanayoendelea mkoani Morogoro.
Timu ya Kamba ya wanawake imefuzu kwa kumaliza nafasi ya kwanza katika kundi A, na kuzipiku Timu za Ras Geita, Uwekezaji pamoja na Timu ya Wizara ya Mambo ya Ndani. Timu ya Kamba ya wanaume imemaliza nafasi ya pili, ambapo nafasi ya kwanza imeshikwa na Uchukuzi katika kundi F. Kwa upande wa Timu ya Netiboli, nayo imemaliza nafasi ya pili, ikitanguliwa na timu ya Ukaguzi katika kundi F.
Akizungumza mara baada ya kufuzu, Mwenyekiti wa Timu hiyo, Gervas Mwashimaha, amezipongeza timu hizo kwa mafanikio yao na kuwataka wachezaji kuendelea kutangaza utalii kupitia michezo na kupambana kuhakikisha wanafika fainali.
"Hongereni sana timu zote kwa ushindi. Mmetuheshimisha sana, hii ndiyo maana halisi ya kuutangaza utalii wa michezo. Pongezi kwenu kwa kupambana na kuhakikisha mnaleta ushindi. Tusisahau hili, viongozi wetu wanataka tushinde na kupeleka vikombe Wizarani, hakika tutavipeleka," amesema Mwashimaha.
Kwa upande wake, Mwenyekiti Msaidizi wa timu hiyo, ambaye pia ni mchezaji wa Kamba (Ke), Bi Sharifa Dunia, amesema wachezaji wote wana ari ya kufanya vyema, jambo linalopelekea matumaini ya kuwa mwaka huu ni mwaka wa maliasili kupata vikombe.
"Ari ya kupambana ni kubwa sana. Wachezaji wanamwako na wamedhamiria makubwa. Ninaamini mwaka huu ni mwaka wa Wizara ya Maliasili na Utalii kuleta makombe," amesema Sharifa.
Timu hizo zinatarajia kuchuana vikali na timu pinzani kwenye hatua ya 16 bora kuanzia kesho, tarehe 25 Septemba 2024, kwenye ufunguzi wa mashindano hayo yanayotakiwa kufunguliwa hapo kesho.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...