Na Mwandishi wetu, Simanjiro
WANAFUNZI 5,383 wa Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, wameanza mitihani ya kuhitimu elimu ya msingi kwa darasa la saba kwa mwaka 2024 hivyo kuungana na wanafunzi wenzao wanaofanya mitihani nchini.


Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro, Gracian Max Makota amesema wanafunzi 5,692 wanatarajia kufanya mtihani wa kuhitimu darasa la saba Septemba 11 na Septemba 12 mwaka 2024.


Makota amesema kati ya wanafunzi hao wanaofanya mitihani wa kuhitimu darasa la saba, watahiniwa 2,838 ni wasichana na watahiniwa 2,854 ni wavulana.


"Halmashauri ya wilaya ya Simanjiro ina shule 93 ambapo 83 ni shule za serikali na 10 ni shule binafsi ambapo shule za msingi Ormotoo, Tumaini, Lengijape na Lengungumwa zinafanya mtihani kwa mara ya kwanza," amesema.


Mwalimu mkuu wa shule ya awali na msingi New Light ya mji mdogo wa Mireran wilayani Simanjiro, Israel Singano amesema wanafunzi wake 72 wamejiandaa vyema kuanza mitihani yao.


Mwalimu Singano amesema wamewaandaa kisaikilojia wanafunzi hao kwa kuwatoa hofu na kuwasihi wafanye mtihani wao kwa utulivu huku wakimtanguliza Mungu.


Mwalimu mkuu wa shule ya msingi Mirerani Tunusia Katukuru amesema wanafunzi 159 wa shule hiyo watafanya mtihani wa kuhitimu darasa la saba.


"Wanafunzi wote wamejipanga vyema kuanza mtihani wao na tunamuomba Mungu awasimamie wafanye vyema na wafaulu kuendelea na elimu ya sekondari," amesema mwalimu Katukuru.


Mwalimu mkuu wa shule ya msingi Jitegemee, kata ya Endiamtu, wilayani Simanjiro, Godwin Mollel amesema wanafunzi 168 wakiwa na furaha wanatarajia kufanya mtihani huo.


Mwalimu Mollel amesema wanafunzi hao wamejiandaa vyema wakitarajia kufanya mitihani yao na kufaulu ili waendelee na elimu ya sekondari.


Mwalimu wa shule ya awali na msingi Glisten ya mji mdogo wa Mirerani, Kennedy Omondi ameeleza kuwa wanafunzi 36 wa shule hiyo wanatarajia kufanya mtihani wa kuhitimu darasa la saba.


Mwalimu Omondi amesema wanafunzi hao wameshafanya mitihani ya majaribio zaidi ya 55 ndani ya shule hiyo na wanatarajia kufaulu vyema, zaidi ya mwaka jana.


Mwalimu mkuu wa shule ya awali na msingi Tarangire ya Wang'waray mjini Babati, Juma Ama amesema wanafunzi 28 wa shule hiyo, wamejiandaa vyema kufanya mtihani wa kuhitimu darasa la saba.


Mwanafunzi wa darasa la saba wa shule ya awali na msingi, New Light, Andrew Lyimo amesema amejiandaa kufanya mtihani wa kuhitimu darasa la saba ili kuanza safari nyingine ya shule ya sekondari.


"Namshukuru Mungu kwa kunipa uzima, nawashukuru wazazi wangu kwa malezi yao, nawashukuru walimu wangu kwa kunisomesha, tunatarajia tutafaulu mitihani yetu kwa uwezo wa Mungu," amesema Lyimo.


Mmoja kati ya wanafunzi wa shule ya msingi Jitegemee anayefanya mtihani wa kuhitimu darasa la saba, Amina Said amesema wamejiandaa vyema na wanafuraha kubwa kufanya mtihani wao.


"Tumeamka tukiwa wazima wa afya na tunamshukuru Mungu kwa hilo, tumeajiandaa vizuri kuanza mitihani yetu ya kuhitimu darasa la saba na tunatarajia tutafaulu kwenda sekondari," amesema Amina.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...