*Mbio za kupitia vikwazo (Obstacle Adventure Racing)

Na Mwandishi Wetu, Michuzi TV
WASHIRIKI wa mafunzo ya ualimu hatua ya kwanza ya mchezo mpya wa kimataifa wa mbio za kupitia vikwazo (World Obstacle Adventure Racing) unaoanzishwa hapa nchini wamesema mafunzo waliyoyapata ya mchezo huo yatawasaidia kuufundisha mchezo huo ili kuwafikia watu wengi zaidi.

Wakiongea kwa nyakati tofauti katika mbuga ya Pande (Pande Game Reserve) iliyopo Mabwepande jijini Dar es Salaam baada ya kukabidhiwa vyeti vyao vya ufaulu wa mafunzo, washiriki hao kutoka michezo mbalimbali wamesema kuwa wamejifunza sheria na taratibu za mchezo huo na namna unavyochezwa.

“Kilichobaki ni sisi sasa kwenda katika maeneo yetu ya kazi na kuangalia namna ya kuanzisha mafunzo kwa watu wengine wakiwemo watoto wadogo ili kuwa na wachezaji mahiri,” amesema Gozbert Boniface, mmoja wa wakufunzi wa mpira wa kikapu aliyeshiriki mafunzo hayo.

Amewataka wanamichezo kujifunza mchezo huo ambao unajumuisha michezo mbalimbali ukiwemo wa riadha na kuwafanya wachezaji kuwa wavumilivu na kuwapa mazoezi ya kutosha.

Mshiriki mwingine wa mafunzo hayo Esther Joshua amesema mafunzo aliyoyapata yanamuwezesha pia kutafuta vipaji vipya vya mhezo huo.

“Kiukweli nimeupenda sana mchezo huu na nitatafuta wadau kuangalia namna ya kuendeleza vipaji vipya wakiwemo wanafunzi kutoka shuleni,” alisema Esther, ambaye anashiriki michezo ya mpira wa kikapu na baiskeli.

Naye Issa Issa ambaye ni mwalimu wa michezo Green Park amesema ni vema waliopata mafunzi haya wakaufundisha kwa watu wengine ili kuueneza kwa haraka zaidi.

“ Utakuwa moja ya michezo pendwa hapa nchini kwa sababu mazingira ya mchezo huu yanavutia sana ikiwemo mbungani, hivyo kwa namna nyingine ni mchezo wa kiutalii na wenye kufundisha ustahamilivu,” amesema Issa.

Akiongea na washiriki wa mchezo huo, Kamanda wa Pori la Akiba la Pande ( wakiwa sehemu ya wafadhili) Doroth Massawe amesema mchezo huo utachochea ukuaji wa utalii, akiwataka waandaaji wa mafunzo hayo kuutumia vema kuitangaza nchi kiutalii.

Mchezo huu umekuwa ukijipatia umaarufu duniani ikiwemo katika bara la Ulaya ambapo kuna michuano mbalimbali inafanyika.

Mratibu wa mafunzo hayo kutoka Scope Event, Abdallah Chapa amesema mchezo huu unajizolea umaarufu na ni moja ya michezo shindani katika michuano ya Olimpiki.

Moja ya vikwazo pendwa ya mchezo huu inayoonekana katika televisheni ni mchezaji kuparamia juu ya miti au bomba maalumu na kuvuka eneo ambalo akishindwa anaaungukia chini ya maji.

Amesema Tanzania kuna wachezaji wenye vipaji ambao wana nafasi nzuri ya kujifunza sheria na taratibu za mchezo huu na kufanya vizuri.

Amewashukuru wadhamini Rand Apartment, Gulamalis , Well Mark Legal, Kilimanjaro Fresh, The Green Sports Park, Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyapori ( Tawa) na Adventure Races kwa kufanikisha mafunzo hayo.

Mmoja wa wadhamini hao Kelvin Kabengula kutoka Kilimanjaro Fresh amesema wameona haja ya kusapoti mafunzo hayo ili kusaidia kuenea kwa haraka mchezo huo.

Washiriki wa mafunzo hayo walishiriki michezo mbalimbali katika mbuga ya Pande iliyopo Mabwepande ukiwemo wa riadha, kupanda juu ya mti kwa kutumia kamba na kuruka uzio.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...