NA FAUZIA MUSSA

WAZAZI na walezi wametakiwa kushirikiana na walimu wa madrasa kuwalinda watoto wao na vitendo vya udhalilishaji ambavyo bado  vinaonekana kuwepo nchini.

Mbunge wa Jimbo la Chaani, Juma Usonge Hamadi aliyasema hayo alipokuwa akizungumza na walimu, wazazi na wanafunzi wa madrasat Nuru-l-huda  wakati wa  ufunguzi wa madrasa  hiyo  uiyoambatana na kusherehekea  mazazi ya Mtume Muhammad S.A.W huko Muharitani Kinyasini Wilayani ya Kaskazini 'A' Unguja.

Alisema licha ya  Serikali  na wadau mbalimbali kukemea vitendo hivyo  na adhabu kutolewa kwa watendaji lakini bado  vinaonekana kujirejea siku hadi siku na kusema kuwa  ipo haja kwa jamii kuimarisha ulinzi  wa watoto ili kuepukana na vitendo hivyo.

 "Kutoka na hali ya utandawazi na mporomoko wa maadili, ni vyema kashirikiana  kuwajengea uwezo  watoto wetu, wa kujua na kujiepusha na vitendo vya udhalilishaji na ukatili wa kijinsia unaoweza kutokea popote  maisha  yao hata katika madrasa.” Alisema Usonge

Usonge aliwasisitiza walimu na wazazi kuendelea  kuwasimamia watoto kupata  elimu zote mbili, na kuwataka wanafunzi hao kusoma kwa bidii na kuwa na nidhamu kwani ni mambo ya msingi katika kufikia ndoto zao za maisha.

Mbali na hayo  aliwapongeza  walimu wa  madrasa hiyo kwa  kuwa wastahmilivu kipindi chote walichokuwa na  mazingira magumu  ya kufundishia hadi kufanikiwa kupata jengo hilo litakaloondoa changamoto ya ufinyu wa vyumba vya madrasa iliyokuwepo hapo awali.

Kwa upande wake Mwalimu Mkuu wa Madrasa hiyo Ustadh Ali Khamis Foum, alisema suala la udhalilishaji na ukatili wa kijinsia likemewa katika  dini zote, hivyo ni vyema  jamiii ikasimamia makatazo hayo ili kukomesha  vitendo vya udhalilishaji nchini.

 Alibainisha kuwa kupatikana kwa  jengo hilo lenye vyumba vitatu vya kujifunzia, kutaondosha mrundikano wa  wanafunzi wengi katika darasa moja, jambo ambalo alilitaja lingeweza kuhatarisha afya zao.

Vilevile alisema ongezeko la vyumba hivyo  pia kutaondoa changamoto ya kuchanganya wanafunzi wa jinsia mbili katika chumba kimoja, jambo ambalo alilitaja lingechochea  wanafunzi kudhalilishana wao kwa wao kama halikutatuliwa.

“ Kabla ya jengo hili baadhi ya wanafunzi walilazimika kusoma nje ya chumba kimoja kilichokuwepo, kupata vyumba hivi itasaidia wanafunzi wetu wote kusoma  ndani” alisema mwalimu huyo

Hata hivyo aliwataka wazazi na walezi kuwa karibu na walimu kwani kukose  mashirikiano  kunazorotesha maendeleo ya elimu kwa wanafunzi.

Baadhi ya wazazi wa wanafunzi wa madrasa  hiyo waliwaomba wadau na wahisani kuwasaidia kuongeza vyoo katika madrasa hiyo ili kulinda afya za wanafunzi.

"mwanzo madrasa hii ilikuwa na vyoo viwili na sasa ina vyoo vinne lakini bado havitoshelezi kutokana na wingi wa wanafunzi na walimu waliopo katika madrasa hii" walisema

Madarasa hiyo ilionzishwa mwaka 1995, ina  wanafunzi  257 wakiwemo wanawake158 na wanaume 99,  pamoja na walimu 7 Wanawake  4  na wanaume 3  ambapo katika hafla ya ufunguzi wa madrasa hiyo,  mbunge  Usonge alikabidhi kiasi cha  shilingi laki mbili kwaajili ya vikalio na kuahidi kutoa vitabu, vijuzuu na misahau kwa wanafunzi hao.

MBUNGE wa Jimbo la Chaani, Juma Usonge Hamadi, akikata utepe kuashiria ufunguzi wa Madrasat Nuru-l-huda iloyopo Muharitani Kinyasini Wilaya ya Kaskazini 'A' Unguja. (PICHA NA MPIGA PICHA).

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...