WIZARA ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar imetembelea vyuo vya Maendeleo ya Wananchi nchini (FDC's) kwa lengo la kujifunza namna vyuo hivyo vinavyotoa mafunzo na ujuzi kwa vijana hususani kwa wanawake vijana waliokatiza masomo kutokana sababu mbalimbali ikiwemo ujauzito na hali ngumu ya maisha.
Akizungumza leo jijini Dar es Salaam mara baada ya kutembelea chuo cha Maendeleo ya Wananchi Kigamboni FDC, Naibu Katibu Mkuu Taaluma wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Dr. Mwanahamisi Ameir amesema kuwa lengo la ziara hiyo ni kujifunza zaidi kutoka katika vyuo hivyo na kuboresha vituo vya mafunzo mbadala Zanzibar.
"Vyuo hivi Tanzania Bara vipo 54 na vinatoa mafunzo kwa vijana mbalimbali ambao hawapo katika mfumo rasmi, Tumeangalia mafunzo gani yanatolewa na tumejifunza program zinazotolewa ambayo pia itasaidia kuboresha vituo vyetu vya mafunzo mbadala." Ameeleza.
Amesema Shirika lisilo la Kiserikali la Karibu Tanzania Organization (KTO,) ambao pia wamedhamini ziara hiyo ni wadau wakubwa katika sekta ya elimu kwa kuhakikisha watoto wa kike hawabaki nyuma katika suala la elimu na kupitia miradi ya Elimu haina Mwisho, Mpira Fursa na program ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Mtoto ni hatua nzuri katika kujenga Taifa bora na kuwataka wakufunzi kuthamini jitihada hizo kwa kufanya kazi kwa bidii, kutumia rasilimali kwa usahihi na kuchukua changamoto kama fursa.
Aidha ameeleza kuwa; Zanzibar kupitia Mamlaka ya Mafunzo ya Amali wanatoa elimu mbadala katika vituo vya Raha Leo na Pemba katika kuhakikisha vijana wanapata elimu na ujuzi na kupitia ziara hiyo watachukua baadhi ya mambo ili kuboresha zaidi vituo vya elimu mbadala na kuwaalika wakufunzi na wadau wa FDC'S kutembelea vituo hivyo ili kuendelea kubadilishana ujuzi utakaoleta tija kwa jamii.
"Nimejifunza jambo hapa wananchi kutokuwa na taarifa juu ya vyuo hivi tunatakiwa kuendelea kuhamasisha ili wananchi wapate taarifa na kutumia fursa ya kupata mafunzo na ujuzi.....Tunaipongeza Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa kuweka nguvu katika hili tumeona miundombinu rafiki pia KTO kwa kuwa wadau wakubwa na muhimu katika kusukuma gurudumu hili." Amesema.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa KTO Maggid Mjengwa amesema, ujio wa ujumbe huo kutoka Zanzibar umezidi kuleta hamasa na chachu ya uelewa wa vyuo vya Maendeleo ya Wananchi Tanzania na kufikia 2025 Falsafa ya muasisi wa vyuo hivyo Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliyoianzisha mwaka 1975 vyuo vya FDC'S vitatimiza miaka 50 kwa mafanikio makubwa ya wananchi kupata ujuzi na elimu.
" Asilimia kubwa ya watanzania ni vijana ambao wanakumbana na changamoto ya ajira kupitia vyuo hivi vijana wengi wamenufaika kwa kupata mafunzo ya nadharia na vitendo ikiwemo ufundi na wameweza kutengeneza ajira kwa wengine na kujiajiri wenyewe, Na kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia KTO tuna program tatu za Elimu haina Mwisho mahususi kwa wanawake vijana waliokatisha masomo kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ujauzito na umaskini ambao hupata fursa ya kumaliza elimu ya Sekondari na ujuzi mbalimbali ikiwemo ufundi, ya pili ni Program ya Mpira Fursa mahususi kwa ajili ya kuendeleza Soka la wanawake pamoja na program ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Mtoto iliyotoa mafunzo ya walimu wa Chekechea." Amefafanua.
Pia Mkuu wa Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Kigamboni FDC Eng. Ramadhan Simba amesema ujio wa viongozi hao umewapa ari zaidi ya kuwahudumia vijana hao pamoja kuongeza ubunifu zaidi kwa manufaa ya Taifa.
Aidha amewataka wananchi hususani vijana kutokata tamaa na kutumia kutumia fursa hizo zinazotolewa katika vyuo vya Maendeleo ya Wananchi 54 nchini kupata elimu na ujuzi na hatimaye kuendelea na ngazi nyingine za Elimu.
Awali Mwenyekiti wa Bodi ya KTO Shaban Lugome amesema ziara hiyo imekuwa na manufaa hususani katika utoaji wa elimu kwa vijana na KTO wamekuwa wakishirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia katika kuhakikisha vijana wanapata elimu na ujuzi utakaoleta tija kwa jamii kwa kupunguza changamoto ya ajira.
Ujumbe huo wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar utatembelea vyuo vya Maendeleo ya Wananchi Kigamboni FDC, Ikwiriri FDC na Kilwa Masoko FDC.
Naibu Katibu Mkuu Taaluma wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Dr. Mwanahamisi Ameir akikagua baadhi ya shughuli zinazofanywa na chuo cha Maendeleo ya Wananchi Kigamboni FDC na kueleza kuwa lengo la ziara hiyo ni kujifunza zaidi kutoka katika vyuo hivyo na kuboresha vituo vya mafunzo mbadala Zanzibar. Leo jijini Dar es Salaam.
Naibu Katibu Mkuu Taaluma wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Dr. Mwanahamisi Ameir akikagua baadhi ya shughuli zinazofanywa na chuo cha Maendeleo ya Wananchi Kigamboni FDC na kueleza kuwa lengo la ziara hiyo ni kujifunza zaidi kutoka katika vyuo hivyo na kuboresha vituo vya mafunzo mbadala Zanzibar. Leo jijini Dar es Salaam.
Naibu Katibu Mkuu Taaluma wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Dr. Mwanahamisi Ameir akisikiliza mada mbalimbali mara baada ya kufanya ziara katika chuo cha Maendeleo ya Wananchi Kigamboni FDC na kueleza kuwa lengo la ziara hiyo ni kujifunza zaidi kutoka katika vyuo hivyo na kuboresha vituo vya mafunzo mbadala Zanzibar. Leo jijini Dar es Salaam.
Matukio mbalimbali wakati wa ziara hiyo.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...