Makamu wa Rais Dkt.. Phillip Mpango akikabidhi tuzo kwa Meneja Uhusiano na Mawasiliano wa ALAF Limited, Hawa Bayumi (kushoto) wakati wa Tuzo za Rais Kwa Wenye Viwanda (PMAYA) Jijini Dar es Salaam hivi karibuni. Kulia ni Afisa Uhusiano na Mawasiliano, Theresia Mmasy.
Na Mwandishi Wetu, Michuzi Tv
UONGOZI wa kampuni ya ALAF Limited umesema kuwa mafanikio yake ya hivi karibuni katika Tuzo za Rais za mzalishaji Bora wa Mwaka (PMAYA) umetokana na pamoja na mambo mengine uthabiti na uwekezaji mkubwa katika ubora uliofanywa na kampuni hiyo.
Akiongelea mafanikio hayo Meneja Uhusiano na Mawasiliano wa Alaf, Hawa Bayumi amesema kuwa uwekezaji bora umeiwezesha kampuni hiyo kushinda tuzo za PMAYA kwa mwaka wa 18 mfululizo.
Amesema mwaka huu, kampuni hiyo imefanikiwa kupokea tuzo tatu kuu ambazo ni pamoja na muonyeshaji bora katika maonyesho ya TIMExpo2024, mshindi katika sekta ya uzalishaji wa bidhaa katika sekta ya uzalishaji chuma hiyo ikiwa ni mara ya 15 mfululizo na mshindi wa pili katika kitengo za mzalishaji bora wa mwaka wa 2024.
Mgeni rasmi katika hafla ya PMAYA mwaka huu, alikuwa ni Makamu wa Rais Dkt. Phillip Mpango ambaye, aliongozana na viongozi wengine wa Serikali na Uongozi wa juu wa shirikisho la Viwanda Tanzania (CTI), ambao ndio waandaaji wakuu wa Tuzo hizo zilizofanyika hivi karibuni kwenye Ukumbi wa Superdome, Masaki jijini Dar es Salaam.
Amesema Tuzo hizo zinatambua kazi nzuri zinazofanywa na wazalishaji mbalimbali nchini Tanzania jambo ambalo linatoa mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa Taifa.
"Malengo ya tuzo hizo ni matatu: kutambua ubora katika viwanda, kuhimiza ubunifu na kukuza ushirikishwaji, ambapo swala hili hushirikisha wazalishaji wote walioko hapa nchini”, amebainisha.
Aidha amesema ALAF ambayo ni kampuni kongwe hapa nchini, itaendelea kuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha inaendelea kuwa kinara katika kukuza sekta ya ujenzi hapa nchini ili wananchi wapate bidhaa bora ambazo zinaakisi thamani ya fedha wanazotoa wakati wa kununua bidhaa za ujenzi yakiwemo mabati ya kuezekea.
“Katika kuweka msisitizo wa dhamira yetu, kiwanda chetu cha mabati ya rangi kiko tayari na kinatarajiwa kuanza uzalishaji Desemba,l mwaka huu; hii ina maana hakutakuwa na haja ya kuagiza mabati yenye rangi nje ya nchi”, amesema.
Kwa mujibu wa Hawa, wahandisi vijana 30 tayari wamepitiwa mafunzo ya namna ya kuendesha mtambo huo wa kutengenezea mabati ya rangi na kwamba mtambo huo utaendeshwa na wafanyakazi wa wa Kitanzania kwa asilimia 100.
Pia ameushukuru uongozi wa CTI kwa mchango mkubwa kwa kampuni ya ALAF ambao hauna kikomo, ambapo pia ameupongeza uongozi huo kwa kuandaa tuzo hizo zimazowahamasisha wazalishaji kuzalisha bidhaa zilizo bora hapa nchini.
Kampuni ya ALAF Limited (ALAF) ni kampuni inayoongoza kwa utengenezaji wa mabati ya kuezekea pamoja na bidhaa zingine za chuma hapa nchini, ambayo ilianzishwa mwaka wa 1960.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...