Imeelezwa kuwa mradi wa kufua umeme kwa nguvu za maji wa Rusumo unaotekelezwa kwa ushirikiano wa Nchi tatu za Tanzania, Rwanda na Burundi utazinduliwa Februari 2025.
Hayo yameelezwa leo Novemba 16, 2024 na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko wakati akizungumza na vyombo vya habari mara baada ya kikao cha Mawaziri wa Nchi hizo tatu wanaohusika na usimamizi wa mradi huo. Kikao kimefanyika eneo la Rusumo, wilayani Ngara Tanzania.
"Tulipata mapendekezo ya kuzindua mwezi wa 12 lakini muda huo mfupi kuweza kuwapata wakuu wa Nchi, tunapeleka maombi kwa wakuu wa Nchi uzinduzi uweze kufanyika mwakani mwezi wa pili." Amesema Dkt. Biteko
Ameongeza kuwa, utekelezaji wa mradi wa Rusumo umefikia asilimia 99.9 na upo katika hatua za umaliziaji vitu vidogo vidogo.
"Kukamilika kwa mradi huu unaiwezesha kila Nchi kupata megawati 27 katika gridi yake ya Taifa." Amesema Dkt.Biteko
Dkt. Biteko amesema Nchi inahitaji umeme mwingi na mahitaji ya umeme kwa sasa ni megawati 1,800 huku uwezo wa kuzalisha umeme ukifikia megawati 3,070.
Amesema manufaa yaliyopatikana ukiacha upatikanaji wa umeme ni pamoja na ajira, miradi ya maendeleo katika Halmashauri ya Ngara pamoja na kuboreshwa kwa huduma za kijamii.
Ameongeza kuwa, mradi wa Rusumo utakuwa kichocheo kikubwa cha uchumi kwa kuiunganisha Tanzania na Nchi za Burundi na Rwanda katika biashara ya umeme.
Amesisitiza kuwa, uwepo wa vyanzo vingi vya kuzalisha umeme utasaidia kukuza uchumi wa Nchi na maendeleo ya mtu mmoja mmoja.
Kuhusu matumizi ya umeme kwa siku nchini amesema asilimia 52 ya umeme inatumiwa na wananchi na asilimia 48 inatumika kwa ajili ya viwanda.
Aidha, ametoa wito kwa jamii kuhifadhi mazingira ikiwa ni msisitizo pia uliotolewa Mawaziri wa nchi hizo tatu kwa kuwataka wasimamizi wa mradi kupanda miti maeneo ya mradi ili uweze kudumu.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...