Hospitali ya Taifa Muhimbili -Mloganzila imeanzisha huduma mbili mpya za ubingwa bobezi kwa wagonjwa wa kisukari, huduma hizo ni pamoja na huduma ya matibabu ya magonjwa ya miguu yatokanayo na ugonjwa wa kisukari pamoja na huduma ya kliniki maalum ya kisukari kwa vijana wenye umri wa miaka 18 hadi 25 maarufu huduma ya mpito.

Kuanzishwa kwa huduma hizo hospitalini hapa ni mwendelezo wa Serikali wa kuboresha huduma za afya nchini ikiwemo kuanzisha matibabu ya ubingwa bobezi ambayo hayapatikani hapa nchini ikiwa ni mkakati wa kuwapunguzia usumbufu wananchi na gharama za kutafuta huduma hizo nje ya nchi.

Akizindua kliniki hizo kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji, Mkuu wa Kitengo cha Mafunzo, Utafiti na Ushauri wa Kitaalam MNH ambaye pia ni Daktari Bingwa Mbobezi wa Magonjwa ya Kisukari na Homoni Dkt. Faraja Chiwanga amesema huduma hizo zitaongeza wigo wa huduma hospitalini hapa ili wananchi waweze kunufaika na uwekezaji uliofanywa na serikali yao.

“Kwa mfano kiliniki hii ya mpito ni ya kwanza kabisa hapa nchini, itakuwa inahudumia vijana wenye umri wa miaka 18 hadi 25 ambao wanahitaji uangalizi na ushauri tofauti ukilinganisha na wagonjwa waliopo katika makundi mengine” Dkt. Faraja Chiwanga

Kwa upande wake Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Kisukari na Homoni, Dkt. Aidan Banduka amesema kumekuwa na ongezeko la wagonjwa wanaohudumiwa katika kliniki hiyo kutokana na ubora wa huduma zinazotolewa ambapo kwa siku wanaona kati ya wagonjwa 80 hadi 160 ambapo kuanzia tangu Disemba, 2022 hadi mwaka 2024 wamehudumia wagonjwa zaidi ya 30,000 ambapo kati ya hao 6,535 ni wapya.

Dkt. Banduka ameongeza kuwa jamii inapaswa kujikinga na ugonjwa huu kwa kufuata mtindo bora wa maisha kwa kuzingatia lishe bora, kupunguza matumizi ya chumvi, mafuta, kuacha matumizi ya tumbaku na unywaji wa pombe uliopitiliza na kufanya mazoezi mara kwa mara.

Uzinduzi wa huduma hizo umeenda sambasamba na maadhimisho ya siku ya kisukari duniani ambayo huadhimishwa Novemba 14 kila mwaka ambapo kauli mbiu ya mwaka huu 2024 ni kisukari na afya bora, ikihimiza kuongeza ufahamu wa athari za kisukari kwa afya ya mwili na akili kwa wagonjwa wenye kisukari.




Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...