WAZIRI wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb.), ameongoza Mkutano wa Dharura wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini Mwa Afrika (SADC-Organ) uliofanyika tarehe 17 Novemba , 2024 jijini Harare, Zimbabwe.

Waziri Kombo ameungana na Mawaziri wenzake wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kujadili hali ya usalama Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) pamoja na njia mbalimbali za kurejesha amani nchini humo.

Akizungumza katika Mkutano huo, Balozi Kombo amebainisha kuwa Tanzania inaunga mkono juhudi zote zinazofanyika katika kurejesha amani Mashariki mwa DRC.

Aidha, Balozi Kombo amezisisitiza Nchi za SADC kushirikiana ili kutafuta suluhu ya kudumu ya kurejesha amani Mashariki mwa Nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

"Ni jukumu la kila Nchi Mwanachama kushirikiana kwa pamoja katika kurejesha amani na usalama kwa nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC)," alisema Waziri Kombo.

Viongozi wengine kutoka Tanzania walioshiriki Mkutano huo ni: Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mhe. Dkt. Stergomena Tax, Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jenerali Jacob Mkunda, Katibu Mkuu Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Faraji Mnyepe na Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kikanda katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Talha Waziri.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...