JESHI la Polisi Mkoa wa Mbeya linawashikilia watuhumiwa wawili kwa tuhuma za mauaji ya aliyekuwa Mwenyekiti wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi Tawi la Machinjioni Kata ya Bwawani Michael Andarson Kalinga [36] mkazi wa Makongolosi Wilayani Chunya kwa kumpiga na kitu butu kichwani.
Katika taarifa iliyotolewa leo Desemba 04, 2024 na Kaimu Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Mbeya, Wilbert Siwa – ACP imeeleza kwamba Desemba 02, 2024 saa 5:30 usiku huko Mianzini, eneo la Mikoroshini, Wilaya ya Chunya Michael Andarson Kalinga [36] alikutwa amefariki dunia na mwili wake kutelekezwa porini umbali wa mita 250 kutoka barabara ya Makongolosi kuelekea Lupatingatinga baada ya kupigwa na kitu butu kichwani sehemu ya utosini na watu ambao hawakufahamika kabla ambao pia walifanikiwa kumpora Pikipiki yenye namba za usajili MC.464 ELL aina ya Kinglion.
“Jeshi la Polisi lilifanya msako mkali ambapo Desemba 03, 2024 huko Mlowo Wilaya ya Mbozi mkoani Songwe lilifanikiwa kuwakamata watuhumiwa hao ambao wanatuhumiwa kuhusika na tukio hilo wakiwa na Pikipiki waliyopora kutoka kwa Michael Andarson Kalinga [36]. Upelelezi wa shauri hili unaendelea ili hatua nyingine za kisheria zifuate.” Imeeleza
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linatoa onyo kwa baadhi ya wananchi ambao wanaendelea kujihusisha na vitendo vya uhalifu kuacha mara moja kwani uhalifu haulipi na badala yake wajihusishe na shughuli halali za kujipatia kipato.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...