Na Nihifadhi Abdulla Zanzibar, 
KAMA sehemu nyengine duniani, inakubwa na changamoto ya uhaba wa wanawake katika nafasi za maamuzi. Ingawa wanawake wamekuwa wakishiriki katika siasa, bado ni wachache ikilinganishwa na idadi ya wanaume katika nafasi za juu za kisiasa na za maamuzi. 

Hii inatokana na sababu mbalimbali, ikiwa ni pamoja na vikwazo vya kijamii,
 kiuchumi, na kiutamaduni vinavyowakumba wanawake.

Suala la rasilimali fedha,woga,familia na uthubutu nazo ni changamoto zinawarudisha nyumba wanawake waliopo kwenye siasa kusonga mbele na kujitokeza kwenye changuzi .Sensa ya 2022 unaonyesha kuwa idadi ya wakaazi wa Zanzibar ni 1.8 milioni, ambapo wanawake wakiwa na idadi kubwa,ikiwa ni takriban 51% ya watu wote kisiwani Zanzibar. Hii ina maana kwamba idadi ya wanawake inakaribia 974,281 mjini wakiwa 482,814 na kijijini ni 491,467.

Zanzibar ikiwa sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilisaini na kuingia kwenye makubalino ya mikataba ya kimataifa kama Mkataba wa Umoja wa Mataifa 1945 unaohimiza usawa wa wanaume na wanawake na kupiga marufuku ubaguzi kwa misingi ya jinsia. Kanuni hizi zimo pia katika tamko la Ulimwengu la Haki za Binadamu 1948 linalojumuisha haki sawa za wanaume na wanawake katika maisha ya kisiasa na ya umma.

Pia Tamko la Beijing na Jukwaa la Utekelezaji 1995 lililopitishwa katika Mkutano wa Nne wa Dunia wa Wanawake, kama ajenda kamili ya kimataifa ya usawa wa kijinsia, linazitaka nchi wanachama kuingiza mtazamo wa kijinsia katika sheria, sera za umma, programu na miradi, na kuchukua hatua katika maeneo kumi na mbili muhimu.

Rasilimali fedha yatajwa.
Pavu Abdallah ni mwanachama wa Chama cha ACT- WAZALENDO amekuwa kwenye majukumu ya kisiasa toka mwaka 2000 kwa sasa anahudumu kama Naibu Katibu,Haki za Binaadam.

Amesema upatikanaji wa fedha kwa wanawake ni changamoto kubwa kwa sababu wanawake waliopo kwenye siasa wengi wao wanajishughulisha na biashara ndogondogo hawana mitaji mikubwa ya kuwawezesha kufanya kampeni
kubwa za kisiasa.”Wakati mwengine hata pesa ya kuchukulia fomu inakuwa ni mtihani kwa mwanamke ,lakini pia anayegombea nae jimboni ni mtu anayejiweza amekuwa kwenye nafasi hio ya uongozi mwanamke hawezi kushinda” Amesema Pavu.

Kwa sasa ushauri pekee ambao anaona unaweza kusaidia wanawake  kwenye kupata pesa za uchaguzi na kampeni ni kujiunga katika vikundi vya ujasiriliamali na vyama kuwasaidia ili uwepo ushiriki wao kama ulivyo kwa wanaume.” Kuna mikopo kwenye vikundi wanawake wakipata hizo fedha, wataweza kuanza kwenye hatua za awali” Pavu amehitimisha.

Familia kutokuniamini
Kwa miaka zaidi ya 35 Naima Salum Hamad amekuwa kwenye harakati za kisiasa na sasa akiwa anashika cheo cha Katibu wa United Democratic Party -UNDP ,Mkoa wa Kaskazini Unguja amesema kuwa familia ni kikwazo kwake wakati alipokuwa akitafuta nafasi ya uongozi ndani ya chama. 

Naima amesema kuwa alifika hadi hatua ya kutalikiwa na mume wake baada ya kwenda kwenye kikao kazi cha Chama Jijini Dar -es Salaam.”Mimi binafsi ilishawahi kunitokea mara moja nilikwenda kwenye mkutano mkuu,niliporudi nikaandikiwa talaka na mume wangu”.

Naima ameendelea kusema kwamba ikiwa mwanamke mwengine anaona hali hii haitakuwa rahisi wao kushiriki kwenye siasa.” Kuna familia bado wanaona suala la wanamke kuingia kwenye siasa ni uhuni tu na ndio maana ukakuta hawakubali kabisa ulete siasa kwenye familia “Amemaliza Naima

Suala la woga na hofu.
Asiata Said Aboubakar, ni muweka hazina kanda ya Unguja kutoka Chama Cha Demokrasia na Maendeleo,alianza siasa zake mwaka 1995 hadi sasa.

Asiata amesema hofu na woga ni vikwanzo wanavyopitia wanawake ambao wako kwenye siasa na hasa wale wanaoanza kuingia kwenye siasa. “Ni wanawake wachache sana ambao unaweza kukutana nao wenye nguvu na ari ya kujitoa na kujipambania” Amesema Asiata ambaye anaona kuwa kunatakiwa juhudi za makusudi kuwasaidia wanawake kupunguza hofu.“Wapewe elimu na kuwepo kwa mpango mathubuti wa elimu ya kujitambua na ulinzi wao pale wanapoaamua kuingia kwenye siasa na uchaguzi” Asiata amehitimisha.


Wadau wanena.
Wanaharakati wa masuala ya kisiasa na utawala bora Zanzibar Almas Ali amesema licha ya kuwepo kwa vikwazo hivyo ila kikwazo kingine ambacho kinaweza kuwa kwenye ni malezi katika familia maana wasichana hawalelewi kama wanaume kuwa kiongozi.”

 Malezi ya kuwa kiongozi yaanza nyumbani na pale ndipo viwanda vya uongozi vinapoanza ikiwa suala hilo halitakuwepo basi vikwazo hivyo vitaendelea kuwatafuna wanawake”. Almas 

Ameongeza kuwa katika sehemu kama Madrasa ni vyema sana walimu wawajenge wasichana uwezo wa kuwa viongozi na sio kuwarudisha nyuma kwenye suala hili. “Walimu wa madrasa nao wasisahau jukumu hili la kuwasaidia wasichana na wanawake kuwapatia elimu ya dini kwenye uongozi maana ni haki yao kugombea ,kuchagulia na kusikika”Amemaliza Almas.

Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Zanzibar TAMWA – Z ni Taasis isiyo ya kiserikali inayojikita katika kutetea haki za wanawake,watoto na watu wenye ulemavu wamekuwa wakitekeleza mradi wa Kuwajengea uwezo wanawake katika uongozi,huku hadi wanawake zaidi ya 300 kutoka katika vyama 19 wamepatiwa mafunzo wakiwemo wanafunzi kutoka vyuo vikuu.

Saphia Ngalapi ni Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano kutoka TAMWA – Z amesema kuwa kuna umuhimu wa wanawake wanaochipukia na wale waliopo kwenye siasa kuendelea kushikwa mkono ili wajitokeze kwenye kuwania nafasi za uongozi. “Tunakutana nao na kuwapatia mafunzo yanayohusisha ujasiriamali, matumizi ya mitandao ya kijamii, na mikakati ya kupata fedha kwa ajili ya kampeni, ambapo mafunzo haya yanaweza kuwasaidia”Amesema Ngalapi huku akiongoza kuwa ni vyema familia ianza kuona suala la usawa wa kijinsia katika malezi. “Watoto wakilelewa kwa usawa kwenye kushirikia masuala ya kujisimamia na kugaiwa majukumu kwenye familia itasaidia suala la kujitambua na kujitokeza kwenye masuala ya uongozi.” Amemaliza Ngalapi.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...