• Ushindi huu umetokana na ubora, ukubwa, na uongozi wa huduma ya Stanbic Private Banking kwa wateja maalum wa hadhi ya juu (high-net-worth individuals).


• Huduma hii uwapa wateja hawa vigogo masuluhisho ya kifedha ya ziada, ikiwa ni pamoja na ushauri wa kifedha, usimamizi wa mali, uwekezaji, na mikopo ya kipekee.


 Benki ya Stanbic Tanzania imetangaza kushinda Tuzo ya ‘Benki Bora ya Kimataifa ya Kuwahudumia Wateja Maalum’ nchini Tanzania katika Tuzo za Euromoney Private Banking Awards 2025. Tuzo hii inatambulika duniani kama kipimo cha ubora na uongozi katika usimamizi wa mali za wateja binafsi wa hadhi ya juu.

Ushindi huu unathibitisha uongozi wa Benki ya Stanbic katika kutoa huduma maalum za kifedha kwa wateja wake wenye ukwasi mkubwa na wajasiriamali wa hadhi ya juu kupitia huduma ya Stanbic Private Banking. Huduma hii huwapatia wateja usimamizi wa mali, ushauri wa kifedha wa kitaalamu, mikopo ya kibinafsi, na masuluhisho mengine yanayozingatia mahitaji yao binafsi.

Sherehe ya tuzo hizo ilifanyika London tarehe 27 Machi 2025 na Stanbic iliwakilishwa na Omari Mtiga, Mkuu wa Wateja Binafsi na Huduma Maalum, pamoja na Shangwe Kisanji, Mkuu wa Private Banking. Walisema kuwa tuzo hii ni uthibitisho wa imani kubwa ya wateja wao na dhamira ya benki kuendelea kutoa huduma bora za kifedha zinazolinda na kukuza mali za wateja.

Mtiga na Kisanji walisisitiza kuwa Stanbic imejipanga kuhakikisha huduma zake zinaendelea kuwa bora, zikiwemo usimamizi wa urithi wa mali, elimu ya kifedha kwa familia za wateja, na huduma za masoko ya kimataifa kupitia mtandao wa Standard Bank Group. Hii inalenga kuhakikisha kuwa mali za wateja zinatunzwa na kuendelezwa kizazi hadi kizazi.

Mafanikio haya yamekuja wakati Benki ya Stanbic ikiadhimisha miaka 30 tangu kuanzishwa kwake nchini Tanzania. Kwa kipindi hicho, imejijengea heshima kama mshirika anayeaminika katika kutoa huduma za kifedha zenye mwelekeo wa maendeleo, uvumbuzi, na matokeo kwa wateja wake.

Mkurugenzi Mtendaji wa Stanbic, Manzi Rwegasira, alisema tuzo hiyo inaonesha dhamira ya benki kuendelea kuwa mshirika muhimu wa maendeleo ya taifa. Aliweka wazi kuwa mkakati wa benki unalenga kumuweka mteja katikati ya maamuzi yote ya biashara na kuendeleza huduma zinazoendana na mahitaji ya soko.

Fredrick Max, Mkuu wa Biashara kwa Wateja wa Kibiashara, aliongeza kuwa ushindi huo ni kielelezo cha dhamira ya kusaidia biashara za ndani kufanikisha maendeleo kupitia huduma zilizobuniwa kwa mahitaji yao.

Mbali na Tanzania, Stanbic Group pia ilishinda tuzo za Afrika kwa kuwa Benki Bora ya Wateja Maalum na Benki Bora ya Elimu kwa Wateja katika Global Finance Awards 2025.

Andrei Charniauski wa Euromoney alihitimisha kwa kusema kuwa washindi wa mwaka huu wameweka viwango vipya vya ubora, ubunifu, na uongozi wa huduma za kifedha barani Afrika.

Mkuu wa Kitengo cha Wateja Binafsi na Huduma Maalum wa Benki ya Stanbic Tanzania, Omari Mtiga na Mkuu wa Kitengo cha Wateja Binafsi, Bi.Shangwe Kisanji wakiwa na viongozi wengine wakati wa hafla ya utoaji wa tuzo za Euro Money Private Banking jijini London, Uingereza, wiki iliyopita. Benki ya Stanbic Tanzania ilitunukiwa Tuzo ya Benki Bora ya Kimataifa ya huduma za Private Banking nchini kutoka Jarida la Euro Money la nchini Uingereza

Mtendaji Mkuu wa Benki ya Stanbic Tanzania, Manzi Rwegasira (kushoto) akipokea Tuzo kutoka kwa Afisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Wateja Maalum wa Benki ya Stanbic, Omari Mtiga (kulia) na Mkuu wa Kitengo cha Wateja Binafsi Shangwe Kisanji (katikati). Tukio hili lilifanyika katika hafla fupi ya kusherehekea tuzo hiyo jijini Dar es Salaam, mwishoni mwa wiki hii. Benki ya Stanbic imetunukiwa Tuzo ya Benki Bora ya Wateja Maalum nchini Tanzania kutoka Jarida la Euro Money la nchini Uingereza.



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...