Na Karama Kenyunko Michuzi Tv 

SERIKALI kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imetangaza kuanzisha mpango wa mikopo nafuu kwa wabunifu nchini kupitia  ushirikiano na Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) pamoja na Benki ya CRDB .

Hatua hiyo imekuja kufuatia Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) kwa kushirikiana na CRDB Bank Foundation kusaini mkataba wa shilingi bilioni 2.3 kwa ajili ya kuziwezesha biashara changa za vijana wabunifu nchini.

Akizungumza Jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya utiaji saini kati ya  COSTECH na CRDB kwa ajili ya mikopo nafuu ya wabunifu kwa Tanzania  Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda amesema  serikali imejipanga kuinua bunifu zinazoweza kuchangia uchumi kwa kuzisaidia kuingia kwenye mnyororo wa thamani na kuleta matokeo chanya kwa taifa.

Amesema, mikopo hiyo inalenga wabunifu walioko kwenye hatua za mwisho za kuingiza bidhaa na huduma sokoni lakini wanakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa mitaji.

“Serikali imejipanga kuinua bunifu zinazoweza kuchangia uchumi kwa kuzisaidia kuingia kwenye mnyororo wa thamani na kuleta matokeo chanya kwa taifa,” amesema Prof. Mkenda.

Mkenda amesema kwa mwaka wa fedha 2025/2026 wizara imetenga kiasi cha Sh bilioni tano kwa ajili ya kuipatia COSTECH ili iweze kusomesha vijana wanaomaliza kidato cha sita kuhusu akili mnemba pamoja na Sayansi ilikusaidia nchi kwenda na teknolojia.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa COSTECH, Dkt. Amos Nungu amebainisha kuwa mkopo huo utawanufaisha moja kwa moja wabunifu waliothibitisha uwezo wa kuzalisha bidhaa au huduma zenye tija kwa jamii.

 "Makubaliano tunayoyasaini leo yanahusu Serikali yetu kuweka tengeo la awali la kiasi cha fedha za Kitanzania, TSh bilioni 2.3 kama dhamana katika Benki ya CRDB. Fedha hizi zitamwezesha CRDB kutoa mkopo nafuu mara mbili ya hiki kiwango kilichowekwa na Serikali kama dhamana. Hii inamaanisha kwamba, kuanzia sasa, wabunifu wa Kitanzania wana fursa ya kuomba mikopo nafuu kupitia Benki ya CRDB hadi kufikia fedha za kitanzania TSh bilioni 4.6 kwa ajili ya kuingiza bidhaa na huduma bunifu sokoni."

"Tunawapa kipaumbele wabunifu ambao tayari wana bidhaa au huduma zenye tija lakini wanakosa mtaji wa mwisho ili kuingia sokoni. Lengo ni kukuza ubunifu wa ndani na kusaidia juhudi za serikali za kuujenga uchumi wa viwanda kupitia teknolojia na ubunifu,” amesema Dkt.  Nungu.

Naye, Mkurugenzi Mkuu wa CRDB Foundation Tullyether Mwambapa amesema Benki hiyo imetenga bilioni 2.3 kwa ajili ya kutoa mikopo nafuu kwa wabunifu walioko chini ya Costech pamoja na kuwapatia usimamizi wa mafunzo miradi ya biashara zao.

Amesema,  benki hiyo imejipanga kuhakikisha mikopo hiyo inaleta matokeo chanya kwa kuwajengea wabunifu uwezo wa kitaaluma na kibiashara.

“Tumejipanga kutoa si tu mikopo, bali pia mafunzo ya usimamizi wa biashara na ujasiriamali kwa wabunifu hawa ili miradi yao iwe endelevu na yenye tija,” amesema Mwambapa.

Mpango huu unatajwa kuwa sehemu ya mkakati wa serikali wa kuifanya sekta ya ubunifu nchini kuwa chombo muhimu cha kukuza uchumi, ambapo serikali imesisitiza kuwa itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha wabunifu wanapata mazingira bora na rasilimali muhimu kwa ajili ya kuendeleza kazi zao.

Aidha, wabunifu waliopo chini ya COSTECH wameahidi kutumia mikopo hiyo kwa uangalifu mkubwa na kuhakikisha inakuwa chachu ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii kupitia ubunifu wao.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...