Mgeni rasmi katika uzinduzi huo alikuwa Mhe. Anthony Mavunde (Mb.), Waziri wa Madini, ambaye aliipongeza kampuni hiyo kwa uwekezaji wake na kusisitiza dhamira ya Serikali ya kuunga mkono viwanda vya ndani.
“Uwekezaji katika kiwanda hiki ni wa kimkakati na umekuja katika wakati muafaka. Mbali na kuboresha ukuaji wa viwanda nchini, kiwanda hiki kinaunga mkono ajenda ya kitaifa ya kuongeza mchango wa sekta ya madini katika Pato la Taifa,” alisema Waziri Mavunde. “Tunakaribisha mchango wa Solar Nitrochemicals na tunahimiza kampuni nyingine kuiga mfano huu ili kupunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje ya nchi.”
Kiwanda hiki cha kisasa kimejengwa mahsusi kwa ajili ya uzalishaji wa vilipuzi vinavyotumika katika uchimbaji wa madini, uchorongaji wa miamba, ujenzi na tafiti za kijiolojia kwa kutumia mitetemo (seismic exploration). Kikiwa kimejengwa jirani na mikoa yenye shughuli za uchimbaji wa madini, kiwanda hiki kitahakikisha upatikanaji wa haraka wa bidhaa, kupunguza gharama za usafirishaji, na uhakika katika mnyororo wa usambazaji katika sekta za uchimbaji hapa nchini.
Mbali na uwezo wake wa uzalishaji, kiwanda hiki kipya kinatarajiwa kuleta matokeo chanya kijamii na kiuchumi. Kiwanda kinakadiriwa kuzalisha ajira za moja kwa moja zipatazo 300 na zaidi ya ajira 1,000 katika mnyororo wa thamani. Kiwanda hicho kinatarajiwa kukuza mchango wa kampuni hiyo katika mapato ya Serikali kupitia kodi na tozo mbalimbali. Tangu kuanza kwa shughuli zake mnamo Novemba 2021, kampuni ya SNCL imechangia kiasi cha Shilingi Bilioni 17.104 katika mapato ya Serikali kupitia kodi mbalimbali, na mchango huu unatarajiwa kuongezeka maradufu ifikapo mwaka 2030.
Vilevile, kiwanda hiki kitawezesha matumizi ya teknolojia mpya na kukuza utaalamu kwa Watanzania. Kwa kuzalisha bidhaa hizi muhimu hapa nchini, SNCL italiwezesha taifa kupunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje na hivyo kukuza uwezo wa Tanzania kujitegemea katika vifaa muhimu kwenye sekta ya madini.
“Madhumuni ya Solar Nitrochemicals ni kuchangia jitihadi za maendeleo ya taifa kupitia uzalishaji wa ndani. Kiwanda hiki ni kielelezo cha dhamira yetu ya muda mrefu ya kuchangia katika maendeleo ya Taifa sambamba na kuzalisha bidhaa salama, za uhakika na zenye gharama nafuu” alisema Bwana Milind Deshmuk, Mkurugenzi Mtendaji wa Solar Group.
Solar Nitrochemicals ambayo ni sehemu ya kampuni mashuhuri na mzalishaji mkubwa zaidi wa vilipuzi nchini India, imeanza shughuli zake nchini Tanzania tangu mwaka 2021, na inaendelea kuwa mshirika muhimu katika uzalishaji wa vilipuzi salama na vya bei nafuu. Kiwanda hiki kipya ni hatua nyingine muhimu katika mkakati mzima wa kampuni ya kupanua shughuli zake barani Africa na kuunga mkono maendeleo endelevu katika nchi zilizoko Mashariki na Kusini mwa Afrika.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...