Mbinga-Ruvuma.

Wakulima wa zao la kahawa wanaohudumiwa na Chama cha Msingi cha Ushirika KINJOLU AMCOS kilichopo kata ya Kikolo na Kihungu, Halmashauri ya Mji Mbinga mkoani Ruvuma, wameiomba Serikali kuchukua hatua madhubuti kukomesha vitendo vya wafanyabiashara wanaonunua kahawa kwa magendo au wakiwa bado mashambani.

Mwenyekiti wa chama hicho, Bosco Turuka, amesema kuwa wafanyabiashara hao wamekuwa wakipita mashambani kila msimu wa mavuno na kuwarubuni wakulima kwa kuwanunulia kahawa kwa bei ya chini wakitumia vipimo visivyo halali maarufu kama “magoma”. Ametoa rai kwa Serikali kusimamia kikamilifu suala hilo kwani linawanyima wakulima mapato stahiki na kuwazuia kupiga hatua kiuchumi.

Turuka amesema kuwa juhudi za Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, kupitia mpango wa ruzuku ya mbolea, zimeongeza uzalishaji wa kahawa kutoka tani 93 msimu wa 2022/2023 hadi kufikia tani 192 msimu wa 2024/2025.

Ameeleza kuwa ruzuku hiyo imesaidia kuboresha maisha ya wakulima kwa kuwawezesha kujenga nyumba bora, kununua vyombo vya usafiri, kusomesha watoto na kuongeza idadi ya wanachama wa chama hicho kutoka 93 hadi kufikia 300.

Pia ameipongeza Serikali kwa kusimamia mfumo wa stakabadhi ghalani ambao umewezesha wakulima kupata bei nzuri ya kahawa msimu huu wa 2024/2025, tofauti na hali ingekuwa iwapo kahawa ingenunuliwa moja kwa moja na watu binafsi mashambani.

Hata hivyo, Turuka ameomba Serikali kutenga bajeti ya matengenezo ya barabara ili kurahisisha usafirishaji wa mazao kutoka mashambani kwenda sokoni, akisema hali mbaya ya barabara huwapa nafasi wafanyabiashara kununua kahawa kwa bei ya chini moja kwa moja vijijini.

Kwa upande wake, mkulima Gotan Komba amepongeza juhudi za Serikali ya awamu ya sita kwa kufufua na kuimarisha sekta ya ushirika, hatua ambayo amesema imeongeza tija kwenye kilimo cha kahawa. Amesema ruzuku ya mbolea imesaidia kupunguza gharama za uzalishaji na kuongeza ukubwa wa mashamba yao.

Komba ameomba mpango wa ruzuku uendelezwe na kupanuliwa ili kujumuisha pembejeo nyingine kama dawa za kuua wadudu, jambo litakalosaidia kuwavutia wakulima wengi zaidi kujikita kwenye kilimo cha kahawa – zao linalotajwa kuwa uti wa mgongo wa uchumi wa Wilaya ya Mbinga na Mkoa wa Ruvuma kwa ujumla.

Naye Hilda Komba, mkulima kutoka kijiji cha Kikolo, amemshukuru Rais Samia kwa kutambua mchango wa wakulima wa kahawa kwa kuwapatia ruzuku ya mbolea pamoja na miche bora ya kahawa kupitia Wizara ya Kilimo, hatua ambazo amesema zimeongeza uzalishaji na kuchochea maendeleo ya wakulima na uchumi wa taifa.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...