Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imeandaa ziara maalum kwa Jumuiya ya wanadiplomasia nchini kutembelea vivutio vya utalii kwa madhumuni ya kutangaza sekta ya utalii nchini.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Shaib Mussa aliwambia waandishi habari kuwa ziara hiyo itakayofanyika kuanzia Aprili 11 hadi 15, 2025 ni utekelezaji wa mpango wa Serikali wa kuitangaza Tanzania kama kituo bora cha utalii na uwekezaji duniani.
Katika ziara hiyo wanadiplomasia hao watapata fursa ya kutembelea Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Bonde la Ngorongoro na visiwa vya Zanzibar ambavyo vimebarikiwa kuwa na fukwe nzuri na bora duniani.
Wakiwa Zanzibar wanadiplomasia hao watapata fursa ya kushiriki hafla ya chakula cha jioni itakayoandaliwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ambapo tuzo ya Rais ya Utalii itatolewa ikiwa ni sehemu ya kusherehekea uhusiano wa karibu kati ya Tanzania na Jumuiya ya Kimataifa.
Balozi Mussa alieleza kuwa kupitia ziara hiyo, makala fupi na filamu za utaliii zitaandaliwa na kugaiwa kwa wanadiplomasia ili wazitumie kutangaza vivutio vya utalii kupitia majukwaa mbalimbali vikiwemo vyombo vya habari vya nchi zao.
Balozi Mussa aliongeza kuwa mpango huo unaotarajiwa kuongeza idadi ya watalii, kukuza uchumi na kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia unatekelezwa kwa ushirikiano baina ya Wizara na wadau mbalimbali wa sekta ya utalii, wakiwemo Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Kamisheni ya Utalii Zanzibar (ZCT) na kampuni binafsi zinazohusika na biashara ya utalii.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...