Zanzibar. Tarehe 21 Mei 2025: Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi ameipongeza Benki ya CRDB kwa jitihada zake za kusaidia utekelezaji wa miradi ya maendeleo baada ya kusaini mkataba wa mkopo nafuu wa takriban Euro milioni 80 (shilingi bilioni 240). 

Akizungumza kwenye hafla ya kutiliana saini mkopo huo kati ya Benki ya CRDB na Wizara ya Fedha na Mipango Zanzibar, Rais Dkt. Mwinyi amesema maendeleo ya taifa yanahitaji ushirikiano wa serikali na sekta binafsi na Benki ya CRDB imekuwa ikionyesha hilo kwa vitendo kwa kujitoa kwake kila inapohitajika kufanya hivyo. 
“Mkopo wa Euro milioni 79.962 utatusaidia kujenga shule 23 za ghorofa mbili. Shule hizi zitajengwa Pemba na Unguja hivyo kusaidia kutatua uhaba wa vyumba vya madarasa kwa kiasi kikubwa. Lengo letu ni kuwaona vijana wetu wanasoma katika mazingira rafiki ya kukua kiumri na kielimu,” amesema Rais Dkt. Mwinyi. 

Uboreshaji huu wa mazingira ya shule, Rais amesema ni muhimu ili kuwapata viongozi bora, madaktari, wahandisi, wahasibu, wanasheria na wasomi wengine mahiri hivyo ni lazima kuwekeza kwenye elimu. 
“Kila mtu mwenye maono mazuri anatambua umuhimu wa elimu hivyo mkopo huu utakaoboresha miundombinu, umekuja kwa wakati sahihi sasa hivi. Nawapongeza Wizara ya Elimu kwa kulifanikisha hili kwani ilikuwa nikipita wananchi wanaomba shule ya ghorofa kila mahali mpaka kule Tumbatu. Sasa suala hilo limekamilika na fedha za ujenzi wake ndio hizi hapa,” amesema Rais Mwinyi. 

Benki ya CRDB imetoa mkopo huo kwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ikishirikiana na Benki ya Deutsche ya nchini Hispania kwa malengo ya kufanikisha ujenzi wa shule hizo zitakazokuwa na madarasa ya kisasa, vyoo bora, bustani za kuvutia, ofisi nadhifu za utawala, maabara na maktaba za kisasa pamoja na viwanja safi vya michezo. 
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Adulmajid Nsekela amesema kwa muda mrefu wamekuwa wadau muhimu wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayosimamiwa na Serikali zote yaani ile la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa lengo la kuboresha maisha ya wananchi wanaoishi mjini au vijijini. 

“Kwa hatua tuliyofikia, kwa sasa pande zote yaani Benki ya CRDB, Benki ya Deutsche na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar tunakamilisha masharti ya awali ya mkopo kwa ajili ya kuanza utekelezaji wa miradi kusudiwa. Ni matumaini yetu kuwa masharti haya ya awali yatakamilishwa kabla ya mwishoni mwa mwezi ujao hivyo kuwezesha kuanza haraka iwezekanavyo utekelezaji wa mradi huu,” amesema Nsekela. 
Nsekela ameongeza kuwa mkopo huo unajumuisha Euro milioni 69.312 sawa na asilimia 85 utakaotolewa kwa ushirikiano wao na Benki ya Deutsche huku kiasi kilichobaki cha Euro milioni 10.65 sawa na asilimia 15 kitatolewa na Benki ya CRDB peke yake suala lililopata baraka zote za SMZ kupitia Wizara ya Fedha na Mipango. 

Nsekela pia amempongeza Rais Dkt. Mwinyi kwa juhudi zake za kuimarisha uchumi wa Zanzibar ikiwamo uuzaji na uorodheshaji wa Hatifungani ya Sukuk iliyotolewa na SMZ mapema mwaka huu na kukusanya shilini bilioni 381 kwa ajili ya ujenzi wa miradi ya maendeleo kwa kufuata misingi ya dini ya Kiislamu. 
Benki ya CRDB imekuwa mdau mkubwa wa maendeleo visiwani Zanzibar ikishiriki kufanikisha miradi yenye thamani ya shilingi bilioni 130. Kwa mkopo uliosainiwa, unaifanya Benki ya CRDB kufikisha jumla ya shilingi billion 375 ya uwezeshaji wa miradi inayosimamiwa na SMZ.







Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...