📍 London, Uingereza
Tanzania imeendelea kuimarisha nafasi yake kama kitovu cha maendeleo ya Sekta ya Madini barani Afrika, kwa kuelezea mikakati madhubuti ya kuendeleza madini muhimu na mkakati yanayopatikana nchini.
Hayo yalielezwa Mei 20, 2025 na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Madini Msafiri Mbibo wakati akihutubia Mkutano wa kimataifa wa Uwekezaji katika Mnyororo wa Thamani Madini Muhimu nchini Tanzania (Investing in Tanzania’s Minerals Value Chain) unaofanyika Jijini London, Uingereza.
Mkutano huo umeandaliwa kwa lengo la kuhamasisha uwekezaji katika mnyororo wa thamani wa madini muhimu, uliwakutanisha Wawekezaji wa Kimataifa, Watunga Sera, Wataalam wa Sekta ya Madini, na Wawakilishi wa mashirika ya maendeleo kutoka pande mbalimbali za dunia.
Mbibo alieleza malengo ya Tanzania ya kuimarisha Sekta ya Madini kupitia ushirikiano wa kimataifa, teknolojia bunifu, na uendelezaji wa mnyororo wa thamani wa madini kwa njia endelevu.
Aliongeza kuwa, Tanzania ina fursa lukuki zinazopatikana nchini katika maeneo ya utafiti wa madini, uongezaji thamani kwa kutumia viwanda vya ndani, pamoja na usimamizi shirikishi unaojali mazingira na maslahi ya wananchi. Alisisitiza kuwa Tanzania imejaliwa kuwa na madini muhimu kama Nikeli, Kobalti, Lithiamu, Shaba, Kinywe (Graphite) , na madini adimu (Rare Earths Elements – REEs), ambayo ni nguzo muhimu katika mapinduzi ya nishati safi duniani.
Aidha, Mbibo alisisitiza kuwa, Serikali ya Tanzania imeweka mikakati thabiti ili kuhakikisha madini hayo yananufaisha taifa kwa:
• Kuimarisha uwekezaji katika utafiti na uchimbaji endelevu,
• Kukuza viwanda vya kuongeza thamani madini ndani ya nchi,
• Kuongeza uwazi katika mnyororo wa madini,
• Kuimarisha ushirikiano wa kimataifa unaozingatia Sera za kitaifa, na
• Kuboreshwa kwa uwezo wa taasisi zinasimamia Sekta ya Madini.
Mbibo aliishukuru Serikali ya Uingereza kwa kuratibu mkutano huo muhimu, na kumpongeza Balozi wa Uingereza nchini Tanzania, Mhe. Marianne Young, kwa mchango wake katika kuimarisha ushirikiano wa pande mbili za mataifa hayo.
Washiriki wa mkutano walionesha kuvutiwa na dhamira ya Tanzania ya kukuza Sekta ya Madini kwa njia jumuishi na endelevu, wakitambua umuhimu wa mchango wa nchi hiyo katika upatikanaji wa madini muhimu kwa ajili ya teknolojia ya kijani duniani.
Naibu Katibu Mkuu Mbibo anaongoza Ujumbe wa Tanzania katika Mkutano huo muhimu kwa mustakabali wa uwekezaji katika mnyororo wa thamani wa madini muhimu Tanzania.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...