NA WILLIUM PAUL, SAME.
MKUU wa wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro Kasilda Mgeni amewataka watendaji wa Serikali kuwajibika ipasavyo kwenye maeneo yao ya kazi na kueleza kuwa baadhi ya maeneo yamekuwa na changamoto kubwa zinazosababishwa na watendaji wa eneo hilo kutowajibika.
Kasilida amesema kuwa hali hiyo inasababisha serikali kupewa lawama kutoka kwa wananchi na changamoto zao kuwa kubwa zaidi kutokana na kutowajibika kwa baadhi ya watendaji hao ambapo amewataka kuheshimu majukumu waliyopewa.
Akizungumza jana na wananchi wa kata ya Maore wakati wa mkutano wa kusikiliza kero, malalamiko ya wananchi na kuyatafutia ufumbuzi Kasilda amesema kuwa zipo zinazosababishwa na kutokuwajibika ipasavyo kwa baadhi ya watendaji wa Serikali.
‘Kuna maeneo mengine changamoto zinakuwa ni kubwa ni kutokana na baadhi ya watedaji wa eneo hilo kutowajibika, hali ambayo inasababisha serikali kupewa lawama, kusababisha kero na malalamiko ya wananchi kutotatuliwa kwa wakati’. Alisema Kasilda.
Pia ameongeza kuwa ‘haiwezekani changamoto ndogo ambayo inaweza kutatuliwa ngazi ya kitongoji, kijiji au kata ikasubiri mpaka aje mkuu wa wilaya ndiyo ije itatuliwe’.
Aidha, alisema kuwa kuna maelekezo mengine ya serikali ambayo baadhi ya watendaji wanapewa kupitia ngazi ya wilaya kuyafikisha maeneo husika lakini bado baadhi ya watendaji hawafikishi maelekezo hayo na matokeo yake wananchi wanakuwa hawajui ni nini serikali imeelekeza.
Alisema ‘Maeneo ambayo yatakuwa na changamoto nyingi na watendaji wa serikali wapo pale, lazima hatua stahiki zichukuliwe juu yao na waeleze kwanini wanashindwa kuwajibika kwenye maeneo yao, na kama wanaona kazi ni ngumu waachie nafasi ili wanaoweza kufanya waje wafanye kazi hizo’.
Hali hiyo ya kutofikisha maelekezo ya serikali kwenye maeneo husika inasababisha pia wananchi kukosa haki zao kwa sababu wananchi hao wanakuwa hawana chochote wananchokifahamu kutokana na maelekezo hayo kuhusu haki zao.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...