*DKT. DORIYE AVISHA VYEO VYA KIJESHI MAAFISA 145 NA ASKARI 476 WA NCAA NA KUSISITIZA UCHAPAKAZI, NIDHAMU, MAADILI NA UZALENDO KATIKA ULINZI WA RASILIMALI


Na Kassim Nyaki, NCAA.
KAMISHNA wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro (NCAA) Dkt. Elirehema Doriye leo tarehe 12 Mei, 2025 amevisha vyeo jumla ya watumishi 621 ikijumuisha Maafisa 145 na askari 476 wa jeshi la Uhifadhi.

Akizungumza na watumishi hao baada ya kuwaapisha na kuwavisha vyeo Dkt. Doriye amewasisitiza maafisa na askari wa jeshi la uhifadhi kuzingatia kiapo walichoapa na kuzingatia maadili ya utendaji kazi, kuzingatia sheria, ushirikiano, upendo na kujiepusha na rushwa katika maeneo ya kazi.

“Leo mmeapa na kuvishwa vyeo vya kijeshi, mnapaswa kuonesha dhamira ya dhati ya kulinda Hifadhi ya Ngorongoro na rasilimali zote za uhifadhi, vyeo mlivyovishwa vinakuja na majukumu makubwa ambayo yanahitaji kujituma na kuwajibika ipasavyo, hakikisheni mnakuwa mfano bora kwa jamii kwa kuzingatia maadili, nidhamu, sheria, uaminifu, uzalendo kwa rasilimali za nchi, kujiepusha na vitendo vya rushwa na kufuata miongozo ya jeshi la Uhifadhi” alisisitiza Dkt. Doriye.

Kamishna Doriye amewakumbusha watumishi hao kuwa, kupanda cheo ni kuongezewa majukumu ya kiuongozi katika usimamizi wa shughuli za uhifadhi, utalii, ulinzi, maendeleo ya jamii na urithi wa asili na utamaduni uliopo hifadhi ya Ngorongoro na kusisitiza kuwa suala la mafunzo ya kijeshi kwa watumishi wa NCAA litakuwa endelevu ili kuendelea kujenga utimamu wa mwili kwa afisa na askari.

Awali akizungumza katika tukio hilo Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi (SACC) anayesimamia Idara ya Rasilimali watu na Utawala Salma Chisonga ameeleza kuwa tukio la kuvishwa vyeo watumishi hao ni utekelezaji wa vibali vya kupandisha vyeo watumishi ambavyo vilitolewa na Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, kwa nyakati tofauti kati ya mwaka 2021/2022 hadi mwaka 2024/2025.

SACC Chisonga amebainisha kuwa maafisa 145 waliovishwa vyeo wamegawanyika katika ngazi mbalimbali ambapo Maafisa uhifadhi Wakuu daraja la kwanza ni 5, Maafisa uhifadhi Wakuu daraja la II ni 21, Maafisa uhifadhi waandamizi ni 31, Maafisa uhifadhi daraja la I ni 56 na Mafiasa uhifadhi daraja la II ni 32.

Ameongeza kuwa askari 476 aliovishwa vyeo wamegawanyika katika ngazi mbalimbali ambapo askari wa uhifadhi mkuu daraja la I ni 39, askari wa uhifadhi wakuu daraja la II ni 54, askari wa uhifadhi Waandamizi ni 70, askari wa uhifadhi daraja la kwanza ni 86 na askari wa uhifadhi daraja la II ni 227.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...