Mhandisi Charles Kitavile wa Kitengo cha Uzalishaji na Usambazaji Maji katika Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Songea (SOUWASA), amewataka wananchi kuhakikisha wanatunza vyanzo vya maji kwa ajili ya usalama wa huduma hiyo muhimu.
Kitavile amesema kwa sasa huduma ya maji inapatikana kwa asilimia 92 ndani ya Manispaa ya Songea, amebainisha kuwa changamoto za upatikanaji wa maji zipo katika baadhi ya maeneo, lakini zinatafutiwa suluhu kupitia Mradi Mkubwa wa Maji wa Miji 28 unaotekelezwa mpaka hivi sasa unaogharimu zaidi ya Shilingi bilioni 145.Aidha, ameeleza kuwa zaidi ya Shilingi milioni 900 zilitumika kulipa fidia kwa wananchi waliokuwa wakiishi pembezoni mwa vyanzo vya maji, hivyo ni muhimu kuacha kufanya shughuli za kibinadamu katika maeneo hayo ili kulinda mazingira na kudhibiti uchafuzi.
Kwa maeneo kama Mtaa wa Bombambili na Sokoine ambayo bado yanakumbwa na changamoto ya upatikanaji wa huduma, Mhandisi Kitavile amewataka wananchi kuhifadhi maji wanapoyapata ili kuepuka usumbufu wakati wa upungufu, huku juhudi zikiendelea kuimarisha upatikanaji wa huduma hiyo.
Wito huo wa Mhandisi Kitavile unaungwa mkono na hatua za SOUWASA katika kutoa elimu kwa wananchi kuhusu matumizi sahihi ya miundombinu ya maji taka, ambapo Kaimu Meneja wa Kitengo cha Majitaka na Usafi wa Mazingira Mhandisi Rosemary Mshanga, alieleza kuwa mamlaka hiyo inaendelea kuwahamasisha wananchi kuacha kutupa taka kwenye mitandao ya maji taka kwa kuwa ni kinyume cha sheria na kunahatarisha afya pamoja na miundombinu.
Kwa upande wake, Meneja wa Huduma kwa Wateja, Jumanne Gayo, alisema mamlaka imekuwa ikipokea na kushughulikia kwa haraka malalamiko ya wananchi na kuendelea kutoa elimu kupitia mikutano ya mitaa na vyombo vya habari.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...