Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) Wilaya ya Songea imewahimiza wananchi wote kujitokeza kuchukua vitambulisho vyao vya taifa ambavyo vimekamilika, ili kuepuka usumbufu unaoweza kujitokeza pale watakapohitaji huduma zinazohitaji kitambulisho hicho muhimu.

Afisa wa NIDA Wilaya ya Songea, Seif Mgonja, amesema kuwa ni vyema wananchi wakajiandikisha mapema na kufuatilia hatua zote za upatikanaji wa vitambulisho vyao, kwani kuchelewa kunaweza kuathiri upatikanaji wa huduma muhimu kama elimu au wanapotaka kwenda kujiunga na jeshi.

“Hakuna gharama zozote kwa ajili ya usajili mpya. Gharama hulipwa tu pale mtu anapopoteza kitambulisho chake ambapo atatakiwa kulipa Shilingi 20,000 kwa ajili ya kupata kipya,” amesema Mgonja.

Ameeleza kuwa huduma za kupiga picha na kuchukua alama za vidole zinatolewa ofisini kwao, na kila mtu anatakiwa kufika binafsi kwa ajili ya usajili  hivyo mzazi hawezi kumwakilisha mtoto.

Kwa mujibu wa maelezo yake, baada ya usajili, namba ya NIDA hutolewa ndani ya siku tatu hadi saba, na kitambulisho kinatarajiwa kuwa tayari ndani ya siku 14 endapo hakutakuwa na msongamano mkubwa wa maombi.

Aidha, ametoa wito kwa wale ambao maandishi kwenye vitambulisho vyao yameanza kufutika kuvirudisha ili wabadilishwe bila malipo.

Mgonja amekumbusha kuwa mchakato wa usajili huanzia kwa watendaji wa mitaa au vijiji ambako watatakiwa kuchukua fomu na kujaza, kwani NIDA haiwezi kusajili moja kwa moja bila taarifa rasmi kutoka kwao.

Katika hali ya kipekee, ameeleza kuwa mtu anaweza kuchukua kitambulisho cha ndugu au jamaa, mradi awe na nyaraka au uthibitisho unaokubalika.

Mwisho, amewataka wananchi kutosubiri hadi watapate matatizo ndipo waanze kufuatilia vitambulisho vyao, bali wajitokeze mapema kuhakikisha taarifa zao ziko sahihi na kupata vitambulisho vyao kwa wakati.



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...