Na Mwamvua Mwinyi, Pwani Mei 22, 2025
Mkoa wa Pwani umejipanga kushinda katika mashindano ya kitaifa ya UMISSETA na UMITASHUMTA, yanayotarajiwa kufanyika mkoani Iringa kuanzia Juni 8 hadi Julai 4, 2025.
Akizungumza wakati wa kupokea msaada wa vyakula kwa ajili ya wanamichezo watakaoshiriki katika kambi ya maandalizi ya siku 14 katika Shirika la Elimu Kibaha, kutoka kwa mdau wa maendeleo na michezo dkt Charles Mwamwaja, Ofisa Elimu wa Mkoa wa Pwani, Mwl. Jimmy Nkwamu, amesema mkoa huo unalenga kurudi na ushindi.
"Tumejipanga kushinda, kunyakua vikombe na medali, kwakuwa hatuko kushiriki bali kwenda kushinda washindi wa kwanza kama si wa pili, alisema Nkwamu .
Kwa mujibu wa Nkwamu, kamati maalum iliundwa kwa ajili ya maandalizi ya mashindano hayo, ambapo imefanikiwa kuwashirikisha wadau mbalimbali na kupata misaada ya jezi, vyakula kama mchele, unga na maharage kutoka kwa wahisani katika halmashauri na wilaya.
"Leo tumepokea msaada mwingine kutoka kwa mwakilishi wa Dkt. Charles Mwamwaja, mdau wa maendeleo na michezo mkoani hapa, ambaye amechangia mchele kilo 200 na unga kilo 100, Tunashukuru sana kwa mchango huu wenye lengo la kuwaweka watoto wetu fit wakiwa kambini,"
Nkwamu alieleza, zoezi la kuchuja timu za halmashauri linaelekea ukingoni, kwani mashindano yalianza Mei 18 kwa lengo la kupata wachezaji bora wa kuunda timu ya mkoa, Tarehe 22 Mei, 2025, wachezaji watakaochaguliwa kuonekana mahiri wataingia kambini kwa maandalizi ya siku 14.
"Tutakuwa na mechi za majaribio dhidi ya timu mbalimbali kabla ya kuondoka Juni 6 mwaka huu kuelekea mkoani Iringa kwa ajili ya mashindano," alifafanua Nkwamu.
Nae Bi. Caroline Malekela, akimwakilisha Dkt. Mwamwaja wakati wa kukabidhi msaada huo, amesema walipokea ombi kutoka kwa kamati ya UMITASHUMTA na wameamua kulitekeleza kwa dhati.
"Tunatambua umuhimu wa michezo katika maendeleo ya vijana wetu, na ndiyo maana tumejitokeza kusaidia," alieleza Caroline.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...