Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), Salim Msangi amefungua rasmi kozi ya pili ya cheti kwa Wakufunzi wa Usalama wa Anga (AVSEC Instructors Certification Phase Two Course) katika Chuo cha Usafiri wa Anga Tanzania (CATC), kilichopo jijini Dar es Salaam.
Kozi hiyo imewakutanisha washiriki 20 kutoka nchi 13 mbalimbali zikiwemo Tanzania, Misri, Côte d’Ivoire, Uganda, Zambia, Tunisia, Somalia, Visiwa vya Shelisheli, Kenya, Botswana, Eswatini, Sierra Leone, Qatar, na Iran.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kozi hiyo, Bw. Msangi alisema mafunzo hayo yanakusudia kuwajengea wakufunzi uwezo wa kutoa mafunzo ya usalama wa anga kwa viwango vya kimataifa. “Hii ni sehemu ya juhudi za Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Anga (ICAO) kuhakikisha kuwa dunia inakuwa na wakufunzi wa kutosha, waliobobea na kuthibitishwa, ili kuimarisha usalama wa anga kimataifa,” alisema.
Kwa upande wake, Mkuu wa CATC, Bw. Aristide Kanje, alieleza kuwa wahitimu wa kozi hiyo wataweza kutoa mafunzo ndani na nje ya nchi zao. Aliongeza kuwa CATC imepokea tuzo ya Outstanding Performance kutoka ICAO, ikiwa ni chuo pekee barani Afrika na cha nne duniani kwa ubora wa utoaji wa mafunzo ya usalama wa anga. “Tunaendelea kujenga wataalamu mahiri kwa ajili ya sekta ya anga duniani,” alisema Bw. Kanje.
Kozi hiyo ni mchango muhimu katika kuimarisha usalama wa anga na kuchochea maendeleo ya sekta hiyo kwa nchi shiriki, sambamba na kuongeza uwezo wa kitaifa na kikanda wa kutoa mafunzo ya kitaalamu.
Mkuu wa Chuo cha Usafiri wa anga Tanzania (CATC) Aristid Kanje akizungumza jambo wakati wa ufunguzi wa Kozi ya pili ya cheti kwa Wakufunzi wa Usalama wa Anga (AVSEC Instructors Certification Phase Two Course).
Baadhi ya washiriki wa Kozi ya pili ya cheti kwa Wakufunzi wa Usalama wa Anga (AVSEC Instructors Certification Phase Two Course) wakisikiliza hituba ya mgeni rasmi Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), Bw. Salim Msangi alipokuwa anafungua kozi hiyo.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...