Na Mwandishi Wetu
WAZIRI wa Ujenzi Abdallah Ulega, amewataka wakandarasi nchini kutekeleza miradi kwa weledi na kwa kuzingatia viwango, ili kuleta tija kwa taifa.
Akizungumza leo Dar es Salaam wakati akifungua mkutano wa mashauriano na wadau wa sekta ya ujenzi, Waziri Ulega amesisitiza umuhimu wa wakandarasi kutekeleza kazi zao kwa kuzingatia masharti ya mikataba, maslahi ya wananchi pamoja na taifa kwa ujumla.
Kwa mujibu wake, wakandarasi wana mchango mkubwa katika kuinua uchumi wa nchi. Amesema wanaposhindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo hukwamisha utoaji huduma kwa wananchi, hivyo kusababisha hasara kwa Serikali.
"Tutawachukulia hatua za kisheria wakandarasi wazembe wanaokiuka makubaliano ya mikataba. Serikali ipo pamoja nanyi kwa kuhakikisha kunakuwa na mazingira bora ya kazi, lakini hatutasita kuwawajibisha ikiwa mtakwenda kinuume na makubaliano," amesema Waziri Ulega.
Wakati huo huo, Baraza la Taifa la Ujenzi (NCC) limebuni mfumo mpya wa uchakataji viwango vya bei za ujenzi na matengenezo ya barabara, lengo likiwa kuisaidia sekta ya ujenzi kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.
Akiwasilisha mfumo wa uchakataji wa viwango vya bei za ujenzi na matengenezo ya barabara katika mkutano huo, Mha. Tumaini Lemunge wa NCC, amesema mfumo huo umetengenezwa kwa ushirikiano na wadau mbalimbali wa sekta ya ujenzi.
Mha. Lemunge amesema mfumo huo utaaidia taasisi, wahandisi washauri, na wakandarasi kufanya makadirio sahihi ya gharama.
“Mfumo huu utawasaidia watumiaji kuandaa makadirio ya gharama kwa miradi mbalimbali ya ujenzi na matengenezo ya barabara, pia utasaidia kulinganisha bei ya mzabuni na bei halisi ya soko, ili kuhakikisha utekelezaji wa mradi unakuwa na tija,” amesema.
Ameongeza kuwa mfumo huo utapunguza changamoto ya utoaji wa bei zisizoendana na uhalisia wa gharama za miradi, jambo ambalo limekuwa likikwamisha utekelezaji bora wa miradi ya ujenzi.
“Natoa mwito kwa wakandarasi wote kuwasiliana na NCC ili waanze kutumia mfumo huu kwa ajili ya kupata bei halisi za zabuni, jambo ambalo litawasaidia kupanga kazi kwa ufanisi,” amesisitiza.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...