NA MWANDISHI WETU, KYELA

SERIKALI imeipongeza Taasisi za NMB Foundation kwa kuendesha Mafunzo kwa Wakulima wa Zao la Kakao kutoka Vyama vya Msingi vya Ushirika wa Kilimo na Masoko (AMCOS) wilayani Kyela, mkoani Mbeya, na kwamba kilichofanywa na taasisi hiyo ni kuunga mkono juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan.

Mafunzo hayo yaliyolenga Kuongeza Thamani ya Zao la Kakao, Masoko na Uandaaji wa Mpango Biashara, yamefanyika kwa siku nne, yakihusisha washiriki 74 (kutoka AMCOS 37), na kufungwa na Mkuu wa Wilaya ya Kyela, Bi. Josephine Manase, ambaye alikabidhi vyeti kwa washiriki hao.

Akizungumza wakati wa hafla ya ufungaji wa mafunzo hayo, DC Manase aliipongeza NMB Foundation na Rabo Foundantion kwa kushirikiana na Chama Kikuu cha Ushirika wa Kilimo na Masoko Kyela (KYECU), kufanikisha mafunzo hayo kwa wadau wa mnyororo wa thamani wa zao la Kakao, kusapoti jitihada za Serikali.

“Ninaposimama hapa kufunga mafunzo haya, basi nianze kwa kuipongeza NMB Foundation na washirika wao Rabo Foundation kwa mafunzo haya, ambayo yanaakisi dhamira yenu ya dhati ya kuliongezea thamani zao la Kakao wilayani Kyela na kukuza uchumi wa wakulima na wadau wake wote.

“Katika hotuba zake nyingi, Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa akipongeza ubora wa Kakao ya Kyela, na hiki mlichofanya NMB Foundation, kinaenda kusapoti jitihada za Serikali Kuu na Serikali ya Wilaya ya Kyela katika kuongeza thamani ya zao hili, ambalo limekuwa na mchango mkubwa kiuchumi kwa taifa.

“Wito wangu kwa NMB Foundation na Washiriki, mafunzo haya yasiishie tu darasani, yakaakisi kile mlichojifunza kwa mamia na maelefu ya wanachama wa AMCOS mliowawakilisha, ili kufanikisha mada zilizotolewa hapa ikiwamo ya uchakataji wa Kakao na kuharakisha ukuaji kiuchumi,” alisema Manase.

Alibainisha ya kwamba – iwapo yatatumika vema, basi mafunzo hayo ni nyenzo muhimu katika kubadilisha maisha na uukuaji kiuchumi wa wakulima wilayani mwake, hasa ikizingatiwa aina ya mada zilizotolewa na wakufunzi kutoka NMB Foundation na Rabo Foundation.

“Kupitia mafunzo haya mmejifunza namna ya kuboresha zao la kakao ili kulipa soko la uhakika, kuongeza mapato kupitia uuzaji wa kakao iliyoboreshwa, kufungua fursa za ajira kwa vijana na wanawake walio kwenye mnyororo wa thamani wa zao hili na kupata elimu ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

“Zaidi ya hayo, kupitia jukwaa hili wakulima wamepata elimu ya fedha na kujua namna ya kupata mikopo nafuu na kunyanyua kilimo chao, namna usahihi ya matumizi ya mikopo hiyo kwa kunua mahitaji ya msingi ya zao husika na kukuza uzalishaji. Juhudi hizi za NMB Foundation zinapaswa kuigwa na kuendelezwa,” alisema.

Kwa upande wake, Mratibu wa NMB Foundation Kanda ya Nyanda za Juu, Rodgers Shipella, taasisi yake kwa kushirikiana na Rabo Foundation, wamebuni na kutekeleza mradi wa kuongeza thamani (semi-processing) ya zao la kakao kwa kujenga uwezo wa wakulima kupitia ushirika katika maeneo mbalimbali.

Shipella aliyataja maeneo hayo kuwa ni: “Elimu ya Ushirika, Uongozi Bora Ndani ya Ushirika, Ujasiriamali, Elimu ya Fedha na Usimamizivna Uendeshaji wa Mikopo, Kuongeza Thamani ya Zao, Uhakika wa Masoko ili Kuongeza Uzalishaji na Uchakataji wa Kakao Wilaya ya Kyela.

“NMB Foundation ilianza rasmi utekelezaji wa mradi huu Oktoba 2023 na tangu wakati huo hadi sasa tumefanikiwa kuwafikia wakulima 1,281, wakiwemo wanawake 314 na wanaume 967. Lengo kuu la mradi huu sio tu kuongeza thamani ya zao la kakao, bali pia kuweka uwiano sahihi wa bei.

“Pia mradi huu unalemga kuibua ajira za uchakataji wa kakao kwa vijana na wanawake, ili kutanua njia za makundi hayo kujiongezea kipato cha kila siku na mantiki hiyo, mradi huu sio tu utawanufaisha wakulima na vyama vyao, bali pia wadau wengine kama vile ushirika, Serikali na wanunuzi,” alisema Shipella.

Akifafanua, Shipela alisema wakati Mkulima atapata bei bora na yenye uwiano, uhakika wa soko, kuamsha ari na hamasa ya uboreshaji wa kakao na kuongeza kipato, Serikali za Mitaa na Serikali Kuu nazo zitanufaika kwa kuongeza kipato, kukuza na kuendeleza uzalishaji zao, Kodi ya Thamani (VAT) na PAY E na ajira kwa vijanana wanawake.

Kaimu Meneja wa Chama Kikuu cha Ushirika Wilaya ya Kyela (KYECU Ltd), Nabii Emmanuel Mwakyenda, aliishukuru NMB Foundation kwa kuwapiga msasa wanachama wa AMCOS 37 za wilaya yake, akiamini mafunzo na elimu waliyopata itakuwa chachu ya ustawi na uendelevu wa Kakao wilayani humo.

Akisoma risala kwa niaba ya washiriki, Evance Mwaipopo kutoka Mwabusye AMCOS, aliipongeza NMB Foundation kwa uendeshaji wa mafunzo, ambayo yamewamenufaisha kupitia mada mbalimbali zikiwamo za Uongezaji Thamani wa Kakao, Kilimo cha Kakao Bila Kukata Miti na Ujasiriamali na Mpango Biashara.

Washiriki wakaiomba NMB Foundation kuendelea kuwajali na kuwathamini wakulima wa kakao Kyela, huku wakiitaka Serikali kwa upande wake izitupie macho barabara zinazoingia na kutoka Kyela, ambazo ni chakavu, ili kurahisisha usafirishaji wa mazao mbalimbali, ikiwemo kakao.





Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...